KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharrif Hamad, amesema, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika kama migogoro ya visiwani haitamalizika.
Kauli hiyo aliisema mwishoni mwa wiki wakati wa Baraza la Idd lililoandaliwa na chama hicho, mjini hapa.
Hamad alisema hatua waliyoichukua yeye na Rais Dk. Amani Abeid Karume, ina lengo la kuondoa migogoro ya Zanzizar ili kuimarisha zaidi Muungano.
Alisema amefurahishwa na hotuba mbalimbali za Rais Karume tangu wafanye mazungumzo rasmi na kumaliza tofauti zao hivi karibuni.
“Mpaka leo (juzi) sijasikia kitu chochote kinachokatisha tamaa kutoka katika kinywa cha Rais Karume katika juhudi mpya za kuunganisha Wazanzibari,” alisema.
“Tumedhamiria kuimarisha amani; hatuna ajenda nyingine yoyote ile iliyojificha.
Watanzania dharauni madai eti mimi na Rais Karume tuna ajenda dhidi ya Muungano. Wazanzibari wote wanaupenda muungano na utadumu,” alisema Hamad na kuendelea kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuunga mkono juhudi zao.
Alisema wale wote ambao wana husuda na muungano wa Karume na Hamad ni lazima wadharaulike.
Aliwataka Wazanzibari kusameheana kwa maslahi ya utaifa ili kuwa katika nafasi ya kudai haki zao kirahisi katika Muungano.
Akizungumza katika baraza hilo, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali alisema Wazanzibari wote wanatakiwa kuwa na matumaini mema hasa kwa sababu Karume na Hamad wana nia njema.
Machano alitaka kuwapo na umoja miongoni mwa Wazanzibari bila kubaguana.
Wakati huo huo, mmoja wa mashehe wa Zanzibar amesema, ni vyema viongozi wa Zanzibar wakajifunza kutoka kwa rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyewaunganisha wananchi wote wa Afrika Kusini bila kujali rangi wala kabila.
Akihutubia baraza hilo, Shehe Saidi Mwinyi alisema viongozi wengi wa Afrika wangeiga mfano wa kiongozi huyo kungelikuwa na utulivu.
No comments:
Post a Comment