SHAHIDI wa tano katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Benki Kuu Tanzania (BOT), Amatus Liyumba, amedai kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo ilikuwa ikijadili katika vikao vya dharura mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki yaliyopo Dar es Salaam.
Liyumba anadaiwa kutumia madaraka vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh Bilioni 200. Kwa mujibu wa shahidi huyo wa Serikali, Dk.Natu Mwamba (48), bodi hiyo haikuwahi kujadili mradi huo katika vikao vya kawaida vya bodi.
Mjumbe huyo wa bodi ya BOT na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, mradi huo ulikuwa ukijadiliwa katika vikao vya dharura na si vya kawaida vinavyofanyika kila baada ya miezi mitatu.
Dk Mwamba ameieleza mahakama kuwa, hata kama katika ajenda za siku hiyo katika mikutano ya kawaida kulikuwa na suala la mradi huo, liliwekwa la mwisho na baada ya ajenda zote kwisha wajumbe ambao hawakuwa wakihusika na mradi walitakiwa kuondoka.
Alipoulizwa kama wajumbe hawakuona ni ajabu kwa nini iwe hivyo, alisema, mwenyekiti wa vikao hivyo ambaye ni Gavana wa BOT ndiye aliyekuwa akiamuru iwe hivyo.
Dk. Mwamba alidai kuwa, mabilioni hayo ya benki yanayodaiwa kuisababishia Serikali hasara yalikuwa yakitumika kwa ridhaa ya Gavana kwa kuwa ndiye mtendaji mkuu.
Amesema mahakamani kuwa,vikao hivyo vya bodi vilikuwa vikiandaliwa na BoT,wajumbe waliitwa katika mikutano ili kuidhinisha malipo, na kwamba, jambo halikuwa sahihi.
Alipoulizwa kwa nini wajumbe wa bodi hawakujiuzulu walipobaini utaratibu unakiukwa alisema,walilifikiria hilo ingawa hakufafanua ni kwa nini hawakufanya hivyo.
Amedai kuwa,walimtumia mjumbe mmoja kuwasilisha malalamiko kwa Waziri wa Fedha wa wakati huo, Basil Mramba, kuhusu matumizi mabaya ya fedha.
Katika mahojiano na mawakili wa mshitakiwa Dk. Mwamba amedai kuwa wajumbe wa bodi hiyo iliwabidi waidhinishe malipo hayo ya mabilioni kuhofia kuvunjwa kwa mkataba jambo ambalo lingesababisha Serikali ishitakiwe.
Hata hivyo amedai kuwa, hana kumbukumbu kamili kuwa ni Shilingi ngapi kwa sababu karatasi za taarifa ya mradi huo zilikuwa zikisomwa na kuachwa pale pale.
Amesema, kwa mujibu wa utaratibu ilitakiwa kuwa kabla matumizi hayajafanyika bodi ipitie na kutoa idhini ndipo jambo lianze kufanyika, na kwamba utaratibu ulikiukwa.
Dk Mwamba amesema, fedha zilitumika, na kisha bodi ya BOT iliombwa ridhaa ya malipo maada ya matumizi.
Amesema, aliyekuwa akiwasilisha taarifa hiyo alikuwa msimamizi wa mradi huo kwa niaba ya kurugenzi ya utumishi na utawala baada ya kupata idhini ya mwenyekiti wa kikao, taarifa ambayo ni ya menejimenti kuja kwenye bodi.
No comments:
Post a Comment