Thursday, November 5, 2009

Mrejesho wa GDSS: Tathimini ya Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa DSM

Demokrasi Bila Wanademokrasia?: Tathimini ya Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa jijini Dar es salaam 2009.

Mwezi uliopita ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na vijiji. Pamoja na mapungufu kadhaa yalijitokeza uchaguzi huo umefanyika na viongozi wamepatikana iwe kwa hila ama halali. Walioshinda wanasema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na walioshindwa wanadai uchaguzi ulikuwa sio huru.

Takribani wagombea 20 walioshiriki kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo walitoa maoni yao juu ya zoezi zima la uchaguzi huo lilivyofanyika. Wakiongea katika mfufulizo wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS), walieleza mchakato wa uandikishaji, kampeni, upigaji kura, na utangazaji wa matokeo ulivyoendeshwa katika baadhi ya mitaa ya jiji la Dar es Salaam. Wengi wao wakiwa ni akina mama na vijana, ikionyesha kuwa ni mwamko mpya kwa wanawake na vijana kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi. Kwa maneno yao wao wenyewe walieleza mapungufu yalijitokeza katika uchaguzi huo bila kujali itikadi ya kichama. Washiriki hao waliweza kueleza dazeni kadhaa ya kasoro na mapungufu zilizojitokeza katika uchaguzi huo.

Kwanza, wananchi wengi hawakujiandikisha kupiga kura kwa kudhani kuwa watatumia vitambulisho vyao vya awali kupigia kura katika uchaguzi huo. Wizara ya Tamisemi inayosimamia mchakato mzima wa uchaguzi ilishindwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na hivyo wengi kushindwa kupiga kura. Pili wakati wa uandikishwaji hakukuwa na vitambulisho vya udhibitisho, kitu kilichopelekea watu kutumia majina ya watu wengine siku ya upigaji wakura.

Wakati wa upigaji kampeni, pia zoezi hili lilitawaliwa na vituko vingi, na mapungufu yalijitokeza ni pamoja na baadhi ya wagombea kutumia lugha za matusi na vitisho badala ya kunadai sera za vyama vyao. Kampeni za ushabiki zilitawala, wagombea wengine hawakutoa nafasi ya kuulizwa mswali, kulikuwepo na ubaguzi wa wazi wa kijinsia, na kifedha, ambapo vyama vya upinzani vilikosa fedha za kutosha ukilinganisha na chama tawala.

Siku ya upigaji kura yenyewe viroja viliongezeka zaidi. Mashuhuda wanasema katika baadhi ya maeneo, vituo vilichelewa kufunguliwa ama kufungwa mpaka saa moja usiku, huku maeneo mengi yakionenkana kuwa na upungufu wa vifaa muhimu vya kupigia kura kama karatasi na wino. Katika baadhi ya mitaa kura zilizohesabiwa zilizidi maradufu idadi ya watu walijioandikisha! Ukiachilia hiyo, maeneo mengine kura hazikuhesabiwa, na polisi kutumia nguvu na kuondoka na masandaku ya kura bila kuhesabiwa. Katika mtaa wa mbagala, sanduku la kura lilikutwa limetelekezwa katika nyumba mbovu huku likiwa na kura! Matukio ya watu kukamatwa na karatasi za kupigia kura ama kurudia kupiga kura zaidi ya mara mbili yalikuwa ni mengi katika mitaa mingi.

Baadhi ya wagombea na wapambe wao walionekana katika baadhi ya vituo wakiwashinikiza wapiga kura kwa kuwavuta-vuta wawachague. Baadhi ya mawakala wa vyama vya upinzani walinunuliwa na chama tawala na kukubali kuwasaliti ndugu zao kwa kiasi kidogo tu cha fedha, na hivyo kuruhusu udanganyifu kufanyika katika zoezi zima la upigaji kura.

Inaelezwa katika utangazaji wa matokeo, baadhi ya maeneo matokeo hayakutangazwa na wananchi kuyasubiri mpaka saa tisa usiku. Na maeneo mengine matokeo hayakutangaza kabisa na jeshi la polisi kutumika kuondoa kwa nguvu masanduku ya kura bila kuhesabiwa! Katika mitaa mingine washindi walitangazwa bila kuwepo kwa mchanganuo wa ushindi huo. Maeneo mengine kutokana kuwepo kwa makosa makubwa kura zinatarajiwa kurudiwa tena katika tarehe za usoni.

Hakika uchaguzi huu unatupa picha ya kile -kama hali hii isipozibitia- kinachoweza kutokea katika uchaguzi mkuu mwakani. Inavyoonekana bado demokrasi yetu ina upungufu wa wanademokrasia ambao ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba mfumo huu unafanya kazi ipasavyo. Wananchi wanshindwa kuelewa, hapa tunachokishabikia sio chama, bali ni maendeleo ya kweli ya nchi yetu tunayoipenda. Tamisemi wanayo mengi sana waliyojifunza na ya kurekebisha. Kila la kheri kwa walioshinda na walioshindwa bado nafasi zingine zipo wajipange zaidi, ama la wasubiri wananchi watakapo elewa zaidi juu ya demokrasi na wanademkrasia.

No comments: