Thursday, November 19, 2009

Mawaziri wanane wazidiwa

-Maofisa wa wizara husika wawalalamikia
-Mmoja adaiwa kujikita zaidi CCM kuliko serikalini
-Kikwete atakiwa kusuka au kunyoa

WAKATI Rais Kikwete ametimiza mwezi huu miaka minne kamili tangu alipoingia madarakani, hali ya utendaji kazi wa baadhi ya mawaziri wake si nzuri na angalau wanane wanalalamikiwa na wafanyakazi wa wizara hizo.

Raia Mwema limetajiwa na wafanyakazi hao jina la waziri mmoja, John Chiligati ambaye inadaiwa hutumia muda mwingi zaidi wa kazi katika shughuli za chama (CCM) ambako ana wadhifa wa kitaifa.

Mawaziri wanaozungumzwa na watendaji waandamizi kwenye wizara zao katika tafsiri ya kutakiwa kuwajibika mbali na Waziri huyo wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, ni Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya na Naibu wake, Dk. Makongoro Mahanga, Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsha Mwangunga na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora, Sophia Simba.

Uchunguzi wa Raia Mwema uliohusisha mazungumzo na baadhi ya watendaji waandamizi wa wizara hizo na baadhi ya wabunge, kwa wiki kadhaa sasa, umebaini kuwa Waziri John Chiligati ndiye mwenye wakati mgumu zaidi mbele ya watendaji kwa kuwa kabla yake, Wizara hiyo ilikuwa na Waziri John Magufuli ambaye anatajwa na watendaji wa chini kuwa ni mchapakazi hodari na alikuwa kipenzi kwa watendaji wengi wizarani.

Kwa mujibu wa mazungumzo hayo kati ya Raia Mwema na watendaji wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, ambayo inasimamia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Chiligati anatajwa kutumia muda wake mwingi zaidi katika shughuli za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako ni Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho-Itikadi na Uenezi.

“Kwetu hapa wizarani na hata wenzetu wa NHC (Shirika la Nyumba la Taifa) tunamwona Mheshimiwa Chiligati kama mwanasiasa zaidi na anatumia muda mwingi kwenye vikao na safari za CCM. Si mtu wa ku-concentrate na masuala ya wizara kama ilivyokuwa kwa Waziri Magufuli, isipokuwa mara chache tu.

“Mambo yamerejea kuwa ya kawaida mno baada ya Magufuli kuondolewa hapa. Kwa kweli Magufuli alikuwa kipenzi cha wafanyakazi wazalendo waliojitoa mhanga kutumikia nchi…hapa mambo yamekuwa ya kawaida sana,” alisema ofisa mmoja mwandamizi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye kwa sababu zilizo wazi hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.

Kwa upande wake, ofisa mwingine kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) amelieleza gazeti hili kuwa ili mambo yaweze kwenda sawa na kwa uhakika ndani ya shirika hilo anahitajika Mkurugenzi mpya wa shirika ambaye ni mzalendo na mchapakazi kwa kuwa tayari kuna pengo la kuwa na waziri mfuatiliaji wa karibu wa majukumu yake katika shirika hilo.

“Tunaye Waziri anayefanya kazi yake kwa kawaida mno bila kasi yoyote na kwa kweli tunazo sababu za kufanya hivyo na hasa tunapomlinganisha na Magufuli. Sasa katika mazingira kama haya ni wazi shirika linahitaji mtu makini na mzalendo zaidi ili aweze kuipa image (taswira) wizara,” alisema ofisa huyo.

Hata hivyo, Raia Mwema ilizungumza na Chiligati kuhusu maoni hayo na alisema ya kuwa “hawezi kufanya mtihani na kujisahihishia mwenyewe.”

“Hayo maoni ya watu siwezi kuyaingilia, mimi siwezi kufanya mtihani na kujisahihisha mwenyewe lakini naamini watendaji ofisi wanajua naingia ofisini saa ngapi na natoka saa ngapi,” alisema Chiligati na alipoulizwa kuhusu shughuli za chama kuingilia majukumu ya serikali, alisisitiza kutotaka kujisahihishia mtihani.

Kutokana na maoni haya, tayari kuliwahi kujitokeza mapendekezo kutoka kwa baadhi ya wabunge na viongozi wa CCM kwamba, viongozi wa serikali, na hususan mawaziri wasiwe viongozi wa chama na hata wajumbe wa Halmashauri Kuu au Kamati Kuu ya chama hicho.

Kati ya wabunge waliowahi kutoa ushauri au mapendekezo hayo kupitia mahojiano na gazeti hili ni Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe ambaye aliweka bayana kuwa kuna mgongano wa maslahi kwa waziri kuwa kiongozi wa kitaifa wa chama.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, ripoti za utendaji wa mawaziri hupaswa kuwasilishwa kwenye kamati kuu au halmashauri kuu ya chama hicho na huwasilishwa na waziri na kwa hiyo mjadala hauwezi kuwa wa haki au ukosoaji kwa kuwa waziri ni sehemu ya uongozi wa chama aliyeteuliwa na Rais.

Lakini maoni mengine nje ya hayo ya Mpendazoe yaliyowahi kutolewa ni kwamba hata na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapaswi kuwa Mwenyekiti wa chama tawala kwa maslahi na ustawi wa chama hicho kwani akiwa kama mwenyekiti hataweza kuongoza kwa uhuru vikao vya kamati kuu au halmashauri kuu vinavyoweza kuibua ukosoaji mkali dhidi yake au serikali yake.

Mbali na Chiligati, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja naye upepo ndani ya wizara yake na hususan Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) haumwendei vizuri mbele ya wananchi. Anaonekana kutotimiza wajibu wake kwa kasi inayostahili na msingi mkuu ni kuonekana kushindwa kuzuia kitisho cha Mkurugenzi wa TANESCO, Dk. Idriss Rashid kuwa nchi itaingia gizani, kitisho ambacho Rais alikipuuza lakini kilitimia; huku Ngeleja akiendelea kuwa waziri hadi sasa.

“Tunamwona Ngeleja kama Waziri ambaye amechangia kuwapo kwa mgawanyiko na hata mgongano baina ya wajumbe fulani wa bodi ya TANESCO na menejimenti ya TANESCO. Kuna mpasuko fulani kwenye bodi na wajumbe wengi wa bodi wako upande wake kuliko kuwa karibu na shirika.

“Ni waziri ambaye si mhimili wa wafanyakazi wa TANESCO, tunamwona kama yuko karibu zaidi na miradi ya umeme ya kampuni binafsi kuliko kuwekeza juhudi na maarifa yake karibu na wataalamu wa TANESCO ili kubaini kuikoa nchi na janga la ukosefu wa umeme. Ameridhika kukimbia huku na huko kwenye miradi midogo ya umeme lakini ukweli ni kwamba hakuna dira ya wazi zaidi ya mikakati kwenye makaratasi kuhusu umeme wa uhakika nchini.

“Watalaamu wanasema mabwawa yetu ya kuzalisha umeme yanahitaji ukarabati madhubuti lakini umesikia hivi karibuni huko Tanga mtambo umepata hitilafu ambayo chanzo chake ni uchakavu. Hii maana yake ama hakuna uratibu mzuri wa taarifa kati ya menejimenti ya TANESCO na Wizara au wizara na hasa waziri hana hamasa ya masuala ya umeme,” alisema mmoja wa maofisa waandamizi wa TANESCO.

Lakini mbele ya wananchi, kitisho cha Dk. Rashid kuwa nchi itaingia gizani na hatimaye ikaingia licha ya ahadi ya Rais kuwa haitafikia hali hiyo ni pigo kubwa kwa Waziri Ngeleja, ambaye pia anaonekana mbele ya wananchi kukimbia huku na huko kutokana na kile kinachotajwa kuwa shinikizo la Rais, kuwasha mitambo ya kampuni binafsi ya IPTL, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa wabunge, wanashindwa kuelewa ni kwa nini Waziri Ngeleja anashindwa kuwasilisha kwa wakati mapendekezo ya iliyokuwa kamati ya Jaji Mark Bomani kuhusu marekebisho ya mikataba na mambo mengine kwenye sekta ya madini nchini.

Kamati ya Bomani iliyoteuliwa na Rais kutoa mapendekezo kwenye sekta ya madini ili taifa linufaike kama ilivyo kwa wawekezaji wa kigeni (win-win situation) iliwashirikisha wabunge makini, kutoka CCM akiwamo Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na wabunge wa kambi ya upinzani, Zitto Kabwe wa Kigoma Kaskazini na John Cheyo wa Bariadi Mashariki.

Inaelezwa kuwa katika mapendekezo hayo, kamati iliweka bayana namna ambavyo taifa linapoteza kiasi kikubwa cha mapato na namna ambavyo hali hiyo inavyoweza kuzuiwa. Kwa kadiri muda unavyopotea ndiyo mapato hayo yanazidi kupotea mikononi mwa taifa.

Jinamizi la mgodi wa North Mara kutiririsha maji ya sumu kwenye Mto Tigithe, Tarime mkoani Mara bado linazidi kumtafuta Waziri Ngeleja akionekana kutojipanga au kupanga Wizara yake kuhakiki mara kwa mara usalama wa migodi na wakazi wanaozunguka, ingawa lawama hizi anapaswa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Dk. Batilda Burian.

Hata hivyo, Waziri Ngeleja hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi lakini Raia Mwema ilizungumza na Naibu Waziri wake, Adam Malima, ambaye hakuwa tayari kuelezea hayo akitaka aulizwe Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, naye anatajwa na baadhi ya watendaji makini wa wizara hiyo kuwa anaongoza ofisi yake katika utaratibu wa ‘business as usual” na hasa kushindwa kutoa mwongozo wa haraka katika masuala tata kama ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambako wafanyakazi waliamua kuchukua hatua ya kutangaza kutomtambua mwekezaji kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ubabaishaji wa mwekezaji huyo na hasa baada ya kutokuwapo kwa mabadiliko yoyote baada ya mwekezaji Railways Infrastructure, Transport and Economic Services (RITES) ya India, kusaini mkataba wa kuwekeza.

Mbali na reli, utata wa muda mrefu katika Bandari ya Dar es Salaam na hasa suala la msongamano wa bidhaa ni kati ya mambo yaliyomchukua muda mrefu Waziri Kawambwa kuamua kwa maslahi ya Taifa kiasi cha baadhi ya wasafirishaji wanaotumia bandari hiyo kudaiwa kuanza kutumia bandari jirani ya Mombasa, nchini Kenya.

Ingawa tayari wizara imefuta ukiritimba wa Kampuni ya Kupakua na Kupakia Mizigo (TICTS) kwa kuruhusu kampuni nyingine binafsi kufanya kazi hiyo, lakini bado wabunge wamekuwa wakipiga kelele kuwa kazi ya kuongeza ufanisi bandarini ni lazima iende sambamba na kuimarisha usafiri wa reli ili mizigo inayokwenda nchi jirani na maeneo mengine nchini iondoke kwa wakati na kasi inayohitajika na hasa ikizingatia kuwa Tanzania imezungukwa na nchi kadhaa zisizo na bandari.

“Waziri wetu na naibu wake ni watu wanaofanya kazi zao kwa kawaida mno, tangu kuwapo kwao hapa hakuna changamoto za wazi walizokuja nazo. Hakuna hamasa yoyote mpya. Hii wizara ndiyo inashughulika na barabara wakati wa awamu ya tatu, iliitwa Wizara ya Ujenzi na alikuwa Magufuli wewe mwenyewe unakumbuka utendaji makini na mbwembwe za Magufuli alipendwa na wahandisi karibu wote wizarani na hata mikoani,” anasema mmoja wa wafanyakazi waandamizi wa wizara hiyo tangu awamu ya tatu. Waziri Kawambwa naye alishindwa kupatikana kupitia simu yake ya mkononi.

Wimbi la vijana kuhama kutoka vijijini kuja maeneo ya miji mikubwa nchini kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na hasa maeneo ya migodi kunatajwa kuwa ni ishara ya kutosha ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya kuongoza wizara yake ili iwe kinara na mwongozo kwa vijana nchini.

Na katika hali isiyo ya kawaida, Wizara hiyo inayoongozwa na msomi kwa kiwango cha ‘profesa’ na naibu wake kiwango cha shahada ya uzamivu (Dk. Makongoro Mahanga), imepachikwa jina la Wizara ya Kuwasha na Kuzima Mwenge, kwa maana kwamba shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru huratibiwa na wizara hiyo.

Baadhi ya wabunge wameilalamikia wizara hiyo kuwa licha ya kuwa na fungu la fedha kwa ajili ya kukopesha vijana, lakini fedha hizo zimekuwa hazina matunda ya wazi kwa taifa na kinyume chake, vijana wamekuwa wakijiongoza wenyewe bila mwongozo wa wizara katika kujikimu kimaisha na kwa hivyo, wizara imechangia kukata mawasiliano kati ya serikali na vijana nchini.

“Naweza kusema bado wizara hii haijapata waziri anayejua awafanyie nini vijana wa Tanzania. Mawaziri na naibu wao karibu wote wamekuwa kama wapita njia wanaosubiri muda au siku yao ya kuondoka ifike, waondoke. Huyu Kapuya alikuwapo hapa awamu ya tatu, migogoro ya kazi ilikuwa mingi na vijana walikuwa wakijifanyia mambo yao wenyewe kwa kadiri ya uwezo wao, wakifika hapa labda wanahitaji sahihi au muhuri wa wizara.

“Umesikia Serikali ya Awamu ya Nne imetoa mikopo ya mabilioni kwa wajasiriamali bila kubagua iende kwa vijana au watu wa rika jingine lakini hapa Wizara na hasa Waziri hashituki na pengine hajui ni vijana wangapi na wa maeneo gani wamenufaika na hadi sasa maendeleo yao yamefikia wapi. Je, wamerejesha fedha au mkasa gani umewapata na msaada gani unatolewa na vijana kwao,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa ngazi ya chini wizarani hapo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha, naye si kiongozi wa kujivunia mbele ya watendaji wa chini yake, ikielezwa kuwa amekuwa akikabiliwa na upuuzwaji wa chini kwa chini na baadhi ya makamanda waandamizi kwenye Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji na kwamba Naibu Waziri, Balozi Khamis Kagasheki ndiye mwenye mvuto kwa kile kinachotajwa kuwa ‘ustaarabu na uungwana’ wake .

Hata hivyo, wakati mawaziri hawa wakionekana kufifia kiutendaji imebainika kuwa taswira bora ya wizara hiyo kwa sasa inabebwa kwa kiasi kikubwa na umakini wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Saidi Mwema. Baadhi ya maofisa waandamizi wa polisi wamekuwa wakimtii Mwema kwa nafasi ya Waziri kwa kuwa juhudi zake zimelenga kwa dhati kuboresha jeshi hilo.

Wizara nyingine ambazo mawaziri wake wapo kwenye hali tete ni Sophia Simba wa Utawala Bora, wizara ambayo vyombo vya Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) viko chini yake.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa tayari kuna mpasuko katika Idara ya Usalama wa Taifa na hasa mpasuko wa maslahi hali ambayo inatajwa kuhitaji Waziri madhubuti tofauti na Simba ambaye anadaiwa kufikia hatua ya kutetea baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Inaelezwa kuwa kupasuka kwa Idara ya Usalama wa Taifa kunathibitishwa na wizi wa mabilioni katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na wizi katika wizara za serikali na taasisi nyingine.

Inadaiwa kuwa baadhi ya maofisa waandamizi wa idara hiyo wamebainika kuwamo katika kashfa nzito nchini, zikiwamo za wizi BoT na kwamba hali inaweza kuwa tete kama watafikishwa mahakamani kwa kuwa wanafahamu siri za vigogo wengine waandamizi walioshirikiana nao kwenye wizi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, anaonekana kuwa makini zaidi akitumia vema Idara zenye mamlaka huru kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na ile ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo amekuwa akisisitiza ni ofisi huru kufikisha kesi mahakamani hali inayomwondoa kwenye kitanzi cha lawama kwa baadhi ya kesi za ufisadi kutofikishwa mahakamani.

Hata hivyo, alikuwa akibanwa na suala la nchi kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC), ambalo nalo limemalizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwamba katiba ya OIC inafanyiwa mabadiliko. Pia Waziri Chikawe amejivua kitanzi cha Mahakama ya Kadhi kwa maelezo ya serikali kwamba ni suala linalopaswa kuundwa ndani ya mfumo, uratibu na usimamizi wa waislamu.

Utata upo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambako Waziri wake Shamsha Mwangunga amewahi kukumbwa na ‘gharika’ la Bunge mara tatu. Mara ya kwanza, aliwahi kubanwa na Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya kuwa amekiuka maazimio ya Bunge kuhusu vitalu vya uwindaji, na ilipendekezwa apewe karipio, mara ya pili, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, kutishia kupinga bajeti yake kutokana na maofisa wake kughushi nyaraka na kuruhusu pembe za ndovu kutoroshwa kwa kutoa vibali kuwa ni kilichobebwa kwenye makontena ni taka za plastiki.

Tatu, ni suala la mgogoro kati ya mwekezaji kampuni ya Ortelo Business (OBC) na wananchi wa Loliondo, ambako Waziri huyo aliunda tume ya kuchunguza na alipotoa taarifa ya tume hiyo bungeni, Mbunge wa Simanjiro alitamka bungeni kuwa ripoti yake (waziri) kwa sehemu kubwa imejaa uongo.

Kutokana na ‘uongo’ huo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta amekwishaunda timu kwenda Loliondo kupata ukweli kwa kulinganisha na taarifa ya Waziri na hali halisi.

Waziri huyo sasa anaishi katika hofu akisubiri kamati ya bunge na bila shaka kama itabainika alitoa taarifa ya uongo bungeni, wito wa kuwajibika utaanza kumwandama.

Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, naye mbele ya wananchi yuko kwenye hali ngumu kwa kuwa licha ya Serikali kutimiza miaka minne bado nchi inakabiliwa na njaa ingawa pia Waziri huyo hakuingia moja kwa moja kwenye wizara hiyo ambayo awali katika serikali ya sasa ilikuwa ikiongozwa na Joseph Mungai. Wasira binafsi aliwahi kuzungumza na televisheni moja nchini na katika kujibu lawama kwamba kwa nini nchi inaingia kwenye njaa akasema; “mimi si waziri wa mvua.”

Kwa ujumla hali ni tete ndani ya wizara hizo na jambo la hatari zaidi watendaji waandamizi wameanza kutilia shaka uwezo wa baadhi ya mawaziri wao na wengine wakibaini kuwa tatizo si mawaziri wao bali ni bajeti finyu.

Hata hivyo, suala la bajeti finyu linapingwa na baadhi ya watendaji wanaodai kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoongozwa na Magufuli pia ina bajeti finyu lakini licha ya upya wake imefanya kazi inayoonekana tayari.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

No comments: