WAKATI Rais Jakaya Kikwete akitaka kuwapo kwa sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha za uchaguzi na kutenganisha biashara na siasa, Serikali imetajwa kuendelea kupata wakati mgumu katika mchakato wa kufikia kilele cha utekelezaji wa azma hiyo ya kulenga kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha kwenye uchaguzi pamoja na muswada wa sheria ya kutenganisha shughuli za biashara na uongozi wa kisiasa, Raia Mwema imethibitishiwa.
Taarifa zinaeleza kuwa kumejitokeza upinzani katika kufikia azima hiyo kwa kuibuliwa hoja mbalimbali ambazo ni pamoja na kiwango gani cha fedha kinachostahili kutumiwa na mgombea wa nafasi kama ubunge na urais, lakini pia ikielezwa kuwa kiwango cha fedha kitakachotamkwa kimlenge zaidi mgombea na si chama cha siasa.
Wanaotaka alengwe mgombea katika kudhibitiwa wanaeleza kuwa hakuna mantiki iliyojitosheleza kama vyama vya siasa vitawekewa kiwango maalumu cha matumizi ya fedha kwa kuwa vipo vyama kama CCM ambavyo vitakuwa na uwezo wa kusimamisha wagombea nchi nzima na kwa hivyo kuwa na bajeti kubwa tofauti na vyama vingine vitakavyoshindwa kufikia hatua hiyo.
Lakini pia taarifa hizo zinaeleza kuwa matumizi ya fedha kati ya eneo moja la nchi na jingine ni tofauti na hasa kati ya maeneo ya vijijini na mjini kwamba kwa kawaida kiwango cha bajeti kwa mgombea wa mjini kuendesha kampeni zake ni lazima kiwe tofauti na mgombea wa kijijini, lakini pia kigezo cha ukubwa wa jimbo la uchaguzi pia si suala la kupuuza.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye suala la udhibiti wa matumizi ya fedha katika mapendekezo ya kutenganisha siasa na biashara hali nayo inatajwa kuwa tete kukijitokeza upinzani mkali wa chini kwa chini kwa hoja kuwa udhibiti wa maadili ya viongozi suluhu yake si kuwaengua wafanyabiashara kwenye siasa bali ni kusimamia kwa kina Sheria ya Maadili ya Umma ambayo inawalazimu viongozi kutangaza mali na wanaosema uongo kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Unaweza kuwa na sheria hii ukasema mfanyabiashara kabidhi biashara zako ili uingie kwenye siasa lakini pia unaweza kuwa na mtu ambaye si mfanyabiashara akaingia kwenye siasa na kuanza biashara akiwa ndani ya uongozi wa kisiasa. Lakini pia ipo mifano ya wafanyabiashara ambao wana mafanikio kwenye biashara zao lakini pia ni wanasiasa wazuri wanaotumikia taifa kwa uaminifu,”
“Kwa hiyo issue si fulani kuacha biashara ili awe mwanasiasa bali ni namna gani maadili yatadhibitiwa kwa viongozi waliopo madarakani bila kujali ni wafanyabiashara au la. Na suluhu hapa ni kurejea na kuheshimu na kuitekeleza bila kigugumizi Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayowalazimisha kutangaza mali wanazomiliki na kukaguliwa na inapobainika hakuna maelezo yaliyojitosheleza kuhusu upatikanaji wa mali hizo au mhusika kandanganya sheria za adhabu lazima zitekelezwe,” alisema ofisa mmoja mwandamizi wa serikali anayeamini sheria hiyo mpya si suluhu.
Hata hivyo, kwa upande mwingine wapo wanaoamini kuwa sheria hiyo itaondoa mkanganyiko wa sasa ambapo viongozi hutumia madaraka yao kuimarisha biashara wanazomiliki ikiwa ni pamoja na kujipatia tenda za serikali ndani ya idara au wizara wanazoongoza kwa kuwa hufahamu vigezo vya utoaji tenda vilivyowekwa na bodi husika.
Kutokana na utata huu, Raia Mwema ilizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ambaye licha ya kukiri kuwapo kwa changamoto hizo alisema ndani ya serikali miswada hiyo haina upinzani kwa kuwa ni mapendekezo ya serikali lakini alionyesha kushindwa kujua namna itakavyopokelewa mbele ya umma na hasa wabunge ambako watalazimika kuijadili kwa kina wakiwa wahusika wakuu kwa namna fulani na hasa wale ambao wataendelea kuwania ubunge mwakani.
Kuhusu muswada wa sheria ya matumizi ya fedha, Waziri Chikawe alisema changamoto kubwa iliyojitokeza hata katika wigo wa mjadala serikalini ni kiwango rasmi cha fedha ambacho mgombea ubunge kwa mfano, atapaswa kukitumia kwenye kampeni pamoja na kujaza fomu ya kutangaza kiasi hicho cha fedha na kilichopo kwenye akaunti yake.
“Kimsingi huu ni muswada wa serikali na huko hakuna tatizo lakini hatuwezi kujua kuhusu mjadala utakavyokuwa kwa wananchi na wabunge kwa ujumla ambao ndiyo wadau wakuu. Kwa mfano kumejitokeza hoja kwamba ni kiasi gani cha fedha za mgombea kitambuliwe na kuruhusiwa kutumika kwenye kampeni, labda unasema kiwango kiwe si zaidi ya milioni 50 na mhusika atangaze kiwango hicho,” alisema Chikawe akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuweka mfumo wa kudhibiti fedha na kujua zinakotoka.
Kuhusu muswada wa sheria ya kutenganisha biashara na siasa, Waziri Chikawe alisisitiza kuwa bado dhamira ya serikali ni kuweka taratibu zenye maslahi zaidi kwa taifa na si maslahi zaidi kwa mtu mmoja mmoja.
Katika hotuba yake ya Desemba 30, 2005, wakati anazindua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Rais Kikwete pamoja na mambo mengine alizungumzia umuhimu wa kuwa na mfumo wa kudhibiti matumizi ya fedha kwenye chaguzi akihofia kuwa isipokuwa hivyo, siku moja kutakuwa na kundi la viongozi walionunua uongozi na walionunuliwa.
Alisema; “Ni kweli nchi yetu sasa ni ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania.
“Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na viongozi wake, ikiwemo wale wa Chama Tawala.
“Tusipofanya hivyo na dalili zimeanza kuonekana, wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali nchi mliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.”
“Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali.
“Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa. Katika mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie.”
Source: www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment