Tuesday, November 3, 2009

Waliomua Albino Kunyongwa

WATU wanne wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya kukusudia dhidi ya albino Lyaku Willy (50) yaliyotokea Bariadi mkoani hapa, Desemba mwaka jana.

Hiyo ni hukumu ya pili kutolewa kwa washtakiwa wa mauaji ya albino baada ya watatu kuhukumiwa kunyongwa Septemba mwaka huu kwa kosa la kumuua Matatizo Dunia, albino aliyekuwa akiishi Bukombe.

Waliotiwa hatiani jana, tarehe 2/11/09 na Mahakama Kuu Shinyanga ni Mboje Mawe, Chenyenye Kishiwa, Sayi Gamaya na Sayi Mafizi, ambao walihusika kumkata mapanga mlemavu huyo na kuufunga mwili wake kwenye sandarusi kisha kuutupa Mto Kidamlida.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo kutoka Mahakama Kuu Tabora, Gab Mjemasi, alisema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 11 vilivyotolewa mahakamani hapo.

Jaji Mjemasi alisema ametupilia mbali maelezo ya mshtakiwa namba moja, licha ya kukana maelezo yake ya awali ya ungamo aliyotoa katika kituo cha Polisi kuwa alipigwa na Polisi ikabidi akubali kuhusika na mauaji hayo.

Alisema hakuna sababu za msingi za mshtakiwa huyo kukana maelezo yake aliyoyatoa kwa madai aliogopa kufa kwani ni dhahiri alihusika na tukio hilo la mauaji ya kikatili.

Pia alisema kulingana na ushahidi uliotolewa na shahidi wa nane, ambaye ni Mkemia wa Serikali, Gloria Mchemve, aliyepima panga linalodaiwa kutumika kumkata Willy na jambia na kukuta vinasaba vya marehemu; ni dhahiri washtakiwa wana hatia.

Alisema pamoja na Mkemia, pia ushahidi unathibitisha kuwa kisu hicho kilitumika kumkata Willy sehemu za mwili wake, ikiwa ni pamoja na shingo, miguu na mikono hivyo washtakiwa hao walikuwa na kesi ya kujibu.

Aidha, Jaji Mjemasi alisema vielelezo vyote vilivyotolewa na upande wa mashtaka vilikuwa ni vya kweli na hakuna sababu ya washtakiwa hao kukataa kuwa hawakuhusika na tukio hilo.

Alitupilia mbali ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi kuwa washtakiwa hawakuhusika na tukio hilo na walikubali kuhusika baada ya kipigo walichopata kutoka kwa askari Polisi.

Jaji huyo aliwataka washtakiwa hao kukata rufaa iwapo wataona kuwa wameonewa, kwani wana haki ya kujitetea upya. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwanzoni mwa Agosti mwaka huu, kwa upande wa Jamhuri walitoa mashahidi 14 na utetezi mashahidi saba.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Albino mkoani Shinyanga, Unice Zabron alimwomba Rais Jakaya Kikwete afanye jitihada za haraka za kusaini hukumu ili hatua ya kunyongwa kwa watu hao itekelezwe.

Alipingana na watetezi wa haki za binadamu kuwa kunyonga mtu ni kunyima haki, akisema hata albino wenzao wana haki ya kuishi kama walivyo binadamu wengine.

No comments: