Friday, July 29, 2011

Lissu, Lema wafukuzwa bungeni

SARAKASI za wabunge bado zinaendelea bungeni mjini Dodoma, jana ilikuwa zamu ya wabunge watatu wa Chadema kutolewa nje ya kikao.

Wabunge hao Godbless Lema wa Arusha Mjini, Tundu Lissu wa Singida Mashariki na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini, walitolewa nje ya ukumbi na Naibu Spika, Job Ndugai, muda mfupi baada ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kumaliza kusoma hotuba yake.

Lema alikuwa akichangia Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, aliyoitoa jana kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2011/12, akiomba Bunge limwidhinishie matumizi ya Sh bilioni 482.3.

Baada ya Lema kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama akiomba kutoa taarifa na pia kuomba Mwongozo wa Naibu Spika kutokana na hotuba ya Lema.

Lukuvi alisema Watanzania wamekuwa wavumilivu, hivyo kutokana na hotuba ya Lema aliyoeleza ilijaa uchochezi, wapime wenyewe na kwamba hotuba hiyo ina matatizo na inashangaza mbunge aliyechaguliwa na wananchi kutoa maneno ya uchochezi na yasiyo ya kistaarabu.

“Mbunge unaweza kusema Tanzania si nchi ya haki… watawala wanatesa wananchi, uchaguzi wa meya Arusha ni batili … polisi wasitii maagizo ya makamanda wao, hotuba hii kwa kweli imejaa uchochezi mkubwa kwa nchi,” alisema Waziri Lukuvi na kushangiliwa na wabunge.

Hata hivyo, wakati Lukuvi akiendelea kuzungumza, Lema, Lissu na Msigwa kwa nyakati tofauti walitaka nao kuzungumza ili kumkatisha Lukuvi, lakini Naibu Spika aliwaambia wakae chini amalizie na wavumilie.

Naibu Spika alitamka mara kadhaa kuwataka Lissu, Lema na Msigwa wazime vipaza sauti, lakini hilo halikuwezekana, hali iliyomlazimu kuchukua hatua ya kuwatoa nje kwa kukiuka kanuni ya Bunge ya kuzungumza bila ruhusa.

Tofauti na ilivyokuwa juzi wakati Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema) alipotolewa nje na Mwenyekiti wa Bunge pia kwa kuvunja kanuni kama wenzake wa jana, lakini hali ilikuwa tofauti kwani Lissu na wenzake walitolewa na askari nje kabisa ya lango la Bunge na kupanda gari wakaondoka eneo hilo.

Kwa mujibu wa Naibu Spika, taratibu ndivyo zinavyotaka, si kwamba Mbunge anatolewa kwenye jengo la Bunge na kukaa maeneo mengine bali anatolewa nje kabisa hadi siku inayofuata atakaporuhusiwa kuingia tena bungeni.

Akifafanua baadaye, Ndugai alisema wananchi hawapendi ubabe na kuwaonya wabunge kwamba miaka mitano si mingi bungeni. Alisema alitumia kanuni ya 60(2) kuwatoa nje wabunge hao, ambapo kanuni hiyo inaeleza kwamba mbunge hataruhusiwa kuzungumza hadi aitwe kwa jina au wadhifa.

Kuhusu hotuba ya Lema, alisema Serikali ilionesha uvumilivu mkubwa kwa kumsubiri mpaka amalize, licha ya kuwapo maneno ambayo hayakuwa ya kiungwana, lakini wapinzani wao walishindwa kumsubiri Waziri Lukuvi amalize kuzungumza.

Pia alisema sera za matumizi ya hoja ya nguvu Afrika hairuhusiwi na Katiba na kwamba masuala mengine ambayo pia yalizungumzwa kwenye hotuba hiyo kama jambo halina uthibitisho, ni vema pia wahusika wakaliacha.

Alimshangaa Msigwa kwamba wakati Lema akizungumza, yeye alikuwa akishangilia kwa nguvu wakati hakupaswa kufanya hivyo kwa vile ni mtumishi wa Mungu.

Aliwaomba wabunge wajitahidi kutumia ishara ya kuhamasisha amani na kueleza kuwa kwa kawaida, hotuba inamfikia Spika siku moja kabla, lakini kanuni hazimpi nafasi ya kuzuia kutolewa, isipokuwa kwa baadhi ya vifungu na si hotuba yote.

“Ndiyo maana leo nilimzuia kusoma aya hii katika hotuba yake, ambayo inasema: ‘Serikali inayohubiri amani kila kukicha kwa kutumia vyombo vyake vya mabavu, imekuwa inakamata wananchi wasio na hatia na kuwabambikizia kesi za uongo pale wanaposhindwa kutoa rushwa katika vituo vya Polisi na mahakamani,” alisema Naibu Spika na kueleza kuwa jambo hilo halina uthibitisho, hasa kwa kuhusisha mhimili mwingine wa Dola kwa maana ya Mahakama.

Pamoja na mambo mengine katika hotuba yake, Lema alieleza kuwa pengine wapinzani walikuwa dhaifu kudhibiti hujuma na dhuluma walizofanyiwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini sasa hawatakuwa tayari kuhujumiwa uchaguzi wowote ujao ukiwamo wa Igunga.

“Mifano hiyo michache inaonesha nchi hii haina amani ya kweli, kilichopo si amani bali utulivu unaojengwa na nidhamu ya uoga. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahadharisha kuwa utulivu wa nchi hii upo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu kuu mbili.

“Kwanza ni kuongezeka kwa matabaka ya Watanzania wengi walio masikini na Watanzania wachache matajiri na wawekezaji wanaopata zaidi haki kwa sababu ya uwezo wao wa kifedha.

“Iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa, basi dalili zipo wazi kuwa uvumilivu wa Watanzania wengi masikini sasa umefika mwisho na lolote linaweza kutokea.

“Amani ya nchi hii ipo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu ya mtazamo potofu wa serikali yetu, kuamini kuwa njia sahihi ya kudumisha amani ni kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwafyatulia risasi, mabomu ya machozi na kuwapiga virungu.

“Hata hivyo sasa wananchi wameanza kuzoea hali hiyo na ni dalili mbaya kwa utawala, ni lazima Serikali ikaelewa kuwa umma wa Watanzania milioni 40 kamwe hauwezi kusambaratishwa na risasi za Jeshi la Polisi ambao idadi yao ni takribani 50,000.

“Kambi Rasmi ya Upinzani kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania, inaionya Serikali inayoongozwa na CCM, kwamba amani ya nchi hii kamwe haiwezi kulindwa na FFU wala majeshi,” alisema Lema na kuwataka polisi nchini wasitii maagizo yoyote katili ya makamanda wao.

Awali katiba hotuba yake, Waziri Vuai alisema hali ya nchi inaendelea kuwa ya amani na utulivu, lakini baada ya uchaguzi uliopita, zimeanza kuonekana dalili za uvunjifu wa amani zikichangiwa na viongozi wa kisiasa.

Alisema baadhi ya viongozi hao wanaandaa maandamano na mikutano ya mara kwa mara, hali inayowanyima wananchi fursa ya kushiriki shughuli za maendeleo na miradi ya kuwapunguzia umasikini.

Alisema muda unaotumika kuandaa maandamano kama ungetumika kwa shughuli za maendeleo bila shaka Tanzania ingepunguza umasikini kwa kiasi kikubwa. Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abadallah (CCM) akichangia hotuba hiyo, alisema kilichozungumzwa na wapinzani si sahihi, kwani haki bila wajibu ni fujo na kwamba watu wanatakiwa kutii mamlaka.

Alisema kama Serikali ikiwa haiwachukulii watu hatua, itaonekana legelege na kwamba lazima polisi waendelee kufanya kazi zao vizuri na kueleza kuwa anashangaa mbunge anaweza kutoa maneno makali na wananchi wakaunga mkono.

“Nauliza kuna kiongozi gani amewahi kuumia katika maandamano? Kuna kiongozi aliwahi kuwaambia wanawake miaka ya nyuma wavue nguo ili kuonesha malalamiko yao, nikawaambia mwambieni aanze mkewe.

“Kupinga kila kitu si ushujaa, uchaguzi umekwisha aliyeshinda kashinda, tusiwe kama Savimbi (Kiongozi wa zamani wa chama cha Unita cha Angola ambaye ni marehemu), yeye akishindwa anasema kaibiwa kura,” alisema Mbunge huyo.

No comments: