BUNGE litaendelea na vikao vyake leo ambapo baada ya kipindi cha maswali na majibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda atawasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Lakini macho na masikio ya Watanzania wiki hii yataelekezwa bungeni Ijumaa wakati Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja atakapowasilisha hotuba ya makadirio ya Wizara yake.
Kati ya wizara nne zitakazowasilisha hotuba zao wiki hii, Wizara ya Ngeleja inasubiriwa kwa hamu kuliko nyingine kutokana na hali ya sekta ya madini kushindwa kuchangia mapato
serikalini kama inavyotarajiwa na hali mbaya ya upatikanaji wa umeme nchini.
Tayari hali mbaya ya upatikanaji wa umeme, imeshasababisha Ngeleja kushinikizwa kujiuzulu; si na wabunge tu, bali pia na vyama vya upinzani huku sekta binafsi, ambayo ni
injini ya uchumi ikilalamikia kupunguza uzalishaji kutokana na upatikanaji usioaminika wa umeme.
Mbali na mgawo huo wa umeme kuzorotesha shughuli za kiuchumi mitaani mpaka viwandani, inatarajiwa Kambi ya Upinzani itarudia mwito wake wa kumtaka Ngeleja
ajiuzulu huku pia wabunge wa CCM wakimbana Waziri huyo kuwahakikishia lini kadhia hiyo itakwisha.
Lakini mara kadhaa, Ngeleja ameeleza msimamo wake kwamba hatajiuzulu wadhifa huo na kwamba tatizo la umeme linashughulikiwa na Serikali kwa mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
Mwishoni mwa wiki akiwa katika kutembelea mabanda ya Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alisema kiini cha matatizo ya umeme nchini ni ukame unaosababishwa na ukosefu wa mvua za kutosha na kuwatetea Ngeleja pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania, William Mhando.
Rais Kikwete alisema kutokana na ukame huo, Serikali inachokifanya sasa ni kutafuta mbadala wa nishati hiyo.
“Tatizo la umeme nchini sio, Ngeleja wala Mhando, kiini haswa ni ukame ambao mvua haijazi maji kwenye mabwawa yanayozalisha nishati hiyo, lakini sasa tunaangalia nishati mbadala wa umeme,” alisema Rais.
Wizara nyingine zitakazowasilisha makadirio yao wiki hii ni Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
itakayowasilisha Jumatano na Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia itakayowasilisha Alhamisi kabla ya Ngeleja kufunga wiki na makadirio yake.
Katika hotuba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, moja ya mambo yanayotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na ufanisi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) pamoja na mkakati kabambe wa ujenzi wa zahanati katika kila kijiji.
Pia wabunge wanatarajiwa kujadili kwa undani hali ya afya ya wajawazito na watoto ikiwemo kuwakinga dhidi ya malaria na kuzuia watoto wasiambukizwe Ukimwi kutoka kwa mama.
Katika Wizara ya Ulinzi na JKT, Serikali inatarajiwa kuelezea hali ya usalama wa nchi, lakini moja ya hoja zitakazotawala ni usalama wa wananchi walio pembezoni na makambi ya jeshi na hali ya uvamizi wa maeneo ya Jeshi la Ulinzi na la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, moja ya hoja zinazotarajiwa kutawala ni kuhusu hisa za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) katika Kampuni ya Celtel Tanzania na hisa za Zain ambayo sasa ni Airtel, kwa kampuni hiyo ya simu ya umma.
No comments:
Post a Comment