Friday, July 1, 2011

Madiwani jino kwa jino na Dk. Slaa

MADIWANI wa Chadema katika Manispaa ya Arusha, wamesema chama hicho ‘hakina ubavu’ wa kuwafukuza kwa kuwa kufanya hivyo, kitakuwa kinacheza mchezo wa pata potea.

Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina gazetini baada ya kuonywa kutozungumzia mgogoro wao na uongozi wa chama hicho Taifa, madiwani hao walisema wanaamini Kamati Kuu ya chama hicho haiwezi kufanya kosa hilo.

‘’Hili suala linapaswa kuamuliwa kwa hekima na busara, kunifukuza mimi ama madiwani wote hapa kuna mambo mawili; moja Chadema kupoteza viti vyote ama kupata na hiyo ni bahati nasibu na sidhani kama Kamati Kuu italikubali hilo,’’ alisema mmoja wa madiwani hao.

Juni 29 Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alikaririwa akisema chama hicho kiko tayari kuwatimua madiwani wake wote wa Arusha kwa madai kuwa wamekisaliti chama baada ya kufikia muafaka wa Arusha kwa maslahi ya mkoa huo.

Dk. Slaa alikaririwa, akisema uamuzi wa madiwani huo, kumpata meya na naibu wake Arusha ambao ulipongezwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), hawautambui kwa madai una upungufu ukiwamo wa kukosa barua ya Chadema ya kukubali maridhiano.

Baada ya kauli hiyo ya Dk. Slaa, iliyotolewa baada ya kauli nyingine ya Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, kwamba hatambui maridhiano hayo ya amani na yenye lengo la kuharakisha maendeleo ya Arusha, madiwani hao Juni 30 waliweka kikao katika hoteli moja
kubwa mjini hapa kujadili kauli hizo.

Baada ya kikao hicho, diwani mwingine alisema Dk. Slaa amewatumia ujumbe kwa njia ya mtandao wa intaneti na kuwaamuru waache kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya habari.

Alisema hata hivyo, kikao chao kimesisitiza kuwa muafaka waliofikia na madiwani wenzao wa CCM, ni sahihi uliofuata taratibu zote kwa maslahi ya chama na si uamuzi wa mtu binafsi wenye uroho wa madaraka na kamwe hawakukurupuka.

‘’Tumefikia muafaka kwa maslahi ya Chadema pia, hatukufanya hivyo kwa uroho wa kutaka vyeo katika kamati ndani ya Halmashauri.

Kauli kwamba tuliamua kwa uroho wa madaraka ni kutaka kuupotosha umma na kauli hizo hazifai kutamkwa na kiongozi kama Lema,’’ alisema diwani huyo.

Alisema wanawaheshimu sana viongozi wao wa juu, lakini na wao ni viongozi waliochaguliwa na wananchi kama Lema na uamuzi waliochukua Lema anaujua, lakini inasikitisha kuona madiwani wakiamua ni kosa, wakati ni kwa maslahi ya wakazi wa Arusha.

Diwani huyo alidai Lema anajua kila kitu, kwa kuwa katika mchakato wa awali, alishirikishwa na kuambiwa kila kitu kinachoendelea, lakini hakutoa uamuzi ila kinachoonekana ni ubinafsi wake na huo ndio unaosumbua ndani ya Chadema.

‘’Hapa suala ni kutoa uamuzi kwa maslahi ya chama na si mtu binafsi; hilo halitawezekana, kwani kila mmoja anapaswa kuheshimiwa na kusikilizwa katika kutoa uamuzi na wasitokee baadhi ya watu ndani ya chama kuonekana miungu watu,’’ alisema.

Mbali na Dk. Slaa na Lema, pia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alinukuliwa kwa nyakati tofauti akipinga muafaka huo.

No comments: