TAIFA la Tanzania lina mtaji wa dola za Marekani bilioni 29 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 43.5) ambao haujathamanishwa kutokana na maeneo mengi ya ardhi kutopimwa na biashara nyingi kutokuwa rasmi nchini.
Aidha, endapo hilo likifanyiwa kazi kupitia Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) kwa asilimia 40 ardhi na asilimia 50 biashara, katika kipindi cha miaka sita kuanzia sasa, itapata mtaji hai wa dola bilioni tisa (sawa na zaidi ya Sh trilioni 13.5).
Hata hivyo, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali katikati ya mwaka wa fedha ujao (2012/13), inatarajia kuanzisha Mfuko wa Urasimishaji Ardhi katika kila wilaya ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mkurabita.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa Mkurabita, Ofisi ya Rais, Mhandisi Ladislaus Salema mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza na gazeti hili.
Salema alieleza kuwa utafiti na uchanganuzi wa faida za Mkurabita walioufanya kwa nyakati tofauti tangu mpango huo kuanza, Novemba mwaka 2004 umeonesha kuwa Serikali kwa kipindi cha miaka 10 imepoteza dola za Marekani milioni 337 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 505.5) kutokana na watu wengi kutorasimisha rasilimali na biashara zao.
Alisema mpango huo wa kutekeleza angalau asilimia 40 ya ardhi iwe rasmi na asilimia 50 ya biashara za wanyonge ziwe rasmi kufikia mwaka 2017 na 2018, unahusisha uanzishwaji wa Mfuko huo katika kila wilaya, utawezeshwa kwa sehemu na Serikali Kuu huku halmashauri za wilaya kwa kushirikiana na wananchi, zikiendelea kuukuza.
Katika hilo, Salema alisema, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa huduma kwa jamii kama shule, afya na maji na kupima maeneo, lakini migogoro imekuwa mingi na kwamba mpango huo kama lilivyo lengo kuu la Mkurabita, utawezesha wananchi wenyewe kutenga na kupima maeneo yao na kupata hospitali, shule na barabara.
Aidha, alisema wananchi wamekuwa wakitoa michango mbalimbali na imekuwa ikiingizwa katika mfuko wa pamoja na maendeleo wa wilaya na kutokana na vipaumbele vya Wilaya, Mkurabita imekuwa ikikwama kiutendaji, lakini kupitia mfuko huo, itaongeza kasi.
“Hivi sasa tupo katika hatua ya awali, na tayari tumeteua Mtaalamu Mshauri anayeendelea na mchakato wa uanzishwaji wa mfuko huo, hatujajua fedha kiasi gani tutachangia kama Serikali Kuu, lakini baadaye itafahamika, ila tutatoa pia mafunzo kwa halmashauri na wananchi na watauendesha wao sisi tukiwa wasimamizi,” alisema Salema.
Salema alisema katika bajeti ya Mkurabita mwaka huu wa fedha ya Sh bilioni sita, wanataendelea na kurasimisha rasilimali za wanyonge katika wilaya nyingine 24 baada ya 24 za awali kufikiwa.
Tangu Mkurabita ianze, hati 17,000 zimeandaliwa katika maeneo ya vijijini na mashamba 51,000 yamepimwa na hati zaidi ya 13,000 zilitolewa na kwa upande wa mijini, hati 5,000 zimeandaliwa na tayari 1,000 zimetolewa.
No comments:
Post a Comment