Tuesday, July 5, 2011

Mishahara juu

ILI kukabiliana na mfumuko wa bei, Serikali imetangaza kupandisha mishahara ya watumishi wa umma nchini katika mwaka wa fedha wa 2011/12 ulioanza mwezi huu.

Licha kukwepa kutaja nyongeza hiyo kitakwimu zaidi ya kusema ni kufanya marekebisho ya mishahara, Serikali imebainisha kuwa itatumia Sh trilioni 3.2 kugharimia mishahara, upandishaji vyeo na kulipia madai ya malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, serikali za mitaa, wakala na taasisi zake.

Akiwasilisha jana Makadirio na Matumizi ya Fedha ya mwaka 2011/12 ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Hawa Ghasia, alisema, marekebisho hayo yamezingatia kasi ya mfumuko wa bei, uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa umma.

"Kiasi hiki cha fedha kilichotengwa kimeongezeka kwa Sh bilioni 938 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 40.2 ya fedha zilizotengwa kugharimia malipo hayo katika mwaka 2010/11," alisema.

Aliongeza kuwa "katika jitihada za kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, Serikali itaendelea kutekeleza sera ya malipo ya mishahara na motisha, katika utumishi wa umma ya mwaka 2010. Mkakati wa utekelezaji wa sera hiyo umeandaliwa".

Alisema, Bodi ya Maslahi ya Tija katika utumishi wa umma itaanza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka huu wa fedha.

Waziri alisema mwaka huu Serikali itapandisha vyeo watumishi 80,050 wa kada mbalimbali.
Hata hivyo, alisema ofisi yake itasimamia mfumo wa mishahara serikalini ambapo kutafanyika ukaguzi wa mara kwa mara wa orodha ya malipo ya mishahara na matumizi ya rasilimaliwatu, ili kuhakikisha watumishi waliopo wanatumika kwa ukamilifu na wanalipwa mishahara kulingana na stahili zao.

Sambamba na hayo, alisema Serikali itaajiri watumishi wapya 64,024 kipaumbele kikiwa kwa sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.

"Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma, itaendesha mchakato wa ajira hizo kwenye wizara , idara zinazojitegemea na wakala za serikali 9,655, sekretarieti za mikoa nafasi 1,514, mamlaka za serikali za mitaa nafasi 48,720, taasisi za Serikali 3,592 na wakala wa serikali 543," alisema.

Kwa upande wa upinzani, katika hotuba yao iliyomwa na Msemaji Mkuu wake, Susan Lyimo, ulieleza kuwa fomula zinazotumika kwa sasa kuongeza mishahara ya watumishi ni za kibaguzi na upendeleo kutokana na kufuata kiwango cha asilimia sawa kwa watumishi wa aina zote, hali inayowapendelea zaidi wenye mishahara ya juu na kuongeza pengo la mshahara kati ya watumishi wa kada za juu na za chini.

Kambi hiyo ilipendekeza kima cha chini ya mshahara kipande kutoka Sh 135,000 hadi Sh 315,000 ambapo alifafanua: "Ili Serikali iweze kuongeza kima cha chini, ipunguze posho na huduma za kulipia watumishi wa ngazi za juu mfano maji, umeme na simu".

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, alishauri Sekretarieti ya Ajira iwe na kanzidata (database) ambayo itaweka kumbukumbu ya watumishi wote walioachishwa kazi, ili kuzuia uwezekano wa kuajiriwa tena watumishi waliofukuzwa kazi kutokana na makosa kama ya ubadhirifu wa mali za umma.

No comments: