Tuesday, July 19, 2011

Makadirio ya Ngeleja yakwama, apewa wiki tatu

MAKADIRIO ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/12 imekwama na hivyo kuahirishwa baada ya wabunge kuigomea.

Imeahirishwa kwa wiki tatu kutokana na ombi lililowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Hii ni mara ya kwanza kwa Makadirio ya Serikali kukataliwa bungeni wakati wa mjadala, ingawa huko nyuma makadirio hayo yalikwama katika ngazi ya Kamati za Kudumu za Bunge.

Kwa mujibu wa Pinda, Serikali itahakikisha inashirikisha Kamati ili yatakaporudishwa bungeni, makadirio hayo yajibu matakwa ya wabunge na yawe yanayotekelezeka hususan katika kukabili tatizo la umeme linaloonekana kukera zaidi wawakilishi hao wa wananchi kwa jumla.

Baada ya Pinda kutamka hoja hiyo iahirishwe, ukumbi wa Bunge uliokuwa umesheheni tofauti na siku zingine, ulilipuka kwa makofi na vigelegele, bila kujali itikadi za vyama ingawa zilisikika baadhi ya sauti kupitia vipaza sauti zikisema, ‘CCM, CCM na wengine wakisema ‘Peoples Power (Nguvu ya umma)’ ambayo ni salamu ya Chadema.

Kuhusu suala la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Pinda alisema, “ni kweli kawaudhi, kawatibua kweli. Lazima nikiri hata mimi nilishituka kweli sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi, hakuna namna ya kutetea.”

Aliendelea kusema: “kikwazo pekee ni kwamba Rais hajatua Afrika Kusini na ndiye mwenye mamlaka ya kuteua makatibu wakuu. Nikisema mimi nichukue uamuzi nitakuwa naingilia maeneo yasiyo yangu. Mnipe Baraka, akifika leo nitawasilisha haya kwake.”

Spika wa Bunge, Anne Makinda akiunga mkono uamuzi wa kuahirisha makadirio hayo, alisema suala la umeme limevuta hisia za Watanzania wengi.

“Nakubali hoja ya wiki tatu wajipange vizuri Serikali ije na kitu kinachotekelezeka na kinacholeta matumaini kwa Watanzania. Kamati ya Uongozi itapanga tarehe,” alisema Spika Makinda na kutangaza kikao cha Kamati ya Uongozi kukutana jana kupanga tarehe mpya.

Akizungumza nje ya Bunge baada ya kuahirishwa kwa hoja yake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema anakubaliana na michango ya wabunge, na kwamba hali hii ya umeme, inatokana na fedha kidogo zilizotengewa Wizara hiyo.

Hali ilianza kuwa mbaya katika michango ya jana asubuhi, wakati ilipoelezwa kuwa Wizara imechangisha takribani Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake ili kufanikisha uwasilishaji wa makadirio ya matumizi yake bungeni.

Alikuwa Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), wakati akichangia mjadala huo, aliwasilisha barua bungeni inayodaiwa kuwa iliandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara, David Jairo, ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo zichangie Sh milioni 50 kila moja, kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa makadirio hayo.

Mbunge huyo pamoja na wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.

Sehemu ya barua hiyo yenye saini ya Jairo kwenda kwa idara na taasisi hizo, inasema, “ili kufanikisha mawasiliano ya hotuba hiyo ya bajeti, unaombwa kuchangia jumla ya Sh 50,000,000.

“Fedha hizo zitumwe Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye akaunti Namba 5051000068 NMB tawi la Dodoma. Baada ya kutuma fedha hizo, wizara ipewe taarifa kupitia ofisi ya DP kwa uratibu.”

Barua hiyo ambayo hata hivyo haikufafanua fedha hizo ni kwa ajili gani, sehemu nyingine ilisema kawaida wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti Dodoma, maofisa wa taasisi zilizo chini yake, huambatana na viongozi waandamizi kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

Hata hivyo, Sendeka alisema watendaji wanaohudhuria si wengi kiasi cha kutumia fedha hizo.

Sendeka alimwomba Waziri Mkuu amwelekeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa dharura kubaini kama fedha hizo zimo kwenye akaunti hiyo.

Wakati hilo likiibuliwa, wabunge wengi waliochangia, walijenga msimamo wa kutounga mkono hoja.

Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla (CCM) aliwashawishi wabunge wote wasikubali kuunga mkono hoja wakati nchi ikiwa imetanda giza kutokana na mgawo wa umeme.

“Naomba nitumie fursa hii kuwashawishi wabunge wenzangu, msiunge hoja. Waliotufikisha hapa wanajulikana na hawachukuliwi hatua,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema ,waliokubali kuingia mikataba kandamizi ya kuuza migodi, wanafikiri kwa matumbo badala ya vichwa. Alisema inashangaza kuona watu hao baadhi wako bungeni na wengine wanaendelea kuwa kwenye mfumo wa Serikali, bila kuchukuliwa hatua zozote.

Spika Anne Makinda aliingilia kati kwa kumtaka kutumia lugha ya kawaida badala ya kusema wanatumia matumbo, lakini mbunge huyo aliendelea kusisitiza kuwa wahusika wanafikiri kwa matumbo, kutokana na kuingia mikataba kwa maslahi binafsi na si kwa uzalendo.

“Wangetumia vichwa, wasingesaini. Unasaini mkataba unaoruhusu ardhi kuuzwa na wewe unajengewa nyumba Mbezi!” alisisitiza kwa mshangao.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, kwa niaba ya Mnadhimu wa Bunge, aliomba mwongozo wa Spika na kusema kauli ya kujengewa nyumba Mbezi Beach ni ya kuudhi.

Alimtaka Mbunge huyo kama ana ushahidi auwasilishe kwa Spika, kuliko kusema jambo hilo, ambalo linadhalilisha mawaziri wote.

Spika alimwunga mkono na akawataka wabunge wasiseme kwa hamasa, akisisitiza kwamba kauli kama hiyo inamvunjia heshima pia mtoa hoja.

Wakati huo huo, suala la kampuni ya Symbion kuchukua mitambo ya Dowans lilionekana kuguswa na baadhi ya wabunge; huku baadhi, akiwamo Sendeka, wakielezwa kushangazwa na ukimya uliogubika baada ya kampuni hiyo kuchukua mitambo hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rebeka Mngodo (Chadema), alitaka kufahamu walioridhia Symbion ichukue mitambo hiyo, huku akisema Katiba inaelekeza Bunge lijadili na kuridhia mikataba.

Akizungumzia tatizo la umeme, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alishauri iundwe kamati ndogo ya wabunge tisa ikimshirikisha Rais ambaye ni sehemu ya Bunge, kutafuta suluhisho la haraka.

Alisema Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ilipokwenda Malaysia, Balozi wa Tanzania nchini humo, aliwaambia kwamba aliiandikia Serikali kuhusu IPTL kwamba ina hali mbaya na mradi pekee ambao kampuni hiyo inao, ni uliomo nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walisema lengo si kumsulubu Waziri Ngeleja isipokuwa walimhadharisha kuwa watendaji na viongozi wake ndiyo wanaomsulubu.

Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Amar (CCM), pamoja na kusisitiza kuwa haungi mkono hoja hadi kieleweke, alimwambia waziri, kwamba wanaomsulubu ni watendaji wake ambao wamekuwa wakiingia mikataba isiyo na maslahi kwa Taifa.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvester Koka, akizungumzia tatizo hilo ambalo lilionekana kumsulubu zaidi Waziri Ngeleja, alisema, “hili si suala la Ngeleja. Serikali haikuwekeza vya kutosha katika nishati.”

Mbunge wa Bahi, Omary Badwel (CCM) pamoja na kuikosoa wizara kwa kusema wananchi hawataki maneno bali vitendo, pia alimtetea Ngeleja kwa kusema, “tutamlaumu Ngeleja, lakini hana jinsi, fedha anazopewa ni kidogo. Serikali haipeleki fedha za kutosha kama zinavyopitishwa na Bunge”.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), ambaye pia hakuunga mkono hoja ya wizara kwa kile alichosema wananchi wamechoshwa na orodha ya miradi, alisema bajeti haioneshi kama umeme ni kipaumbele.

Alisema kati ya Sh bilioni 58 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka jana, Sh bilioni 13 pekee ndizo zilipatikana.

Baada ya kubainika kuwa wabunge wengi waliochangia wamekataa kuunga mkono hoja, Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CCM), aliomba Mwongozo ili Bunge liamue kuondoa hoja ya wizara kabla ya muda wa kamati ya matumizi kukaa.

Aliomba hilo lifanyike kwa kile alichosema wizara ipewe muda irekebishe matatizo yaliyo katika bajeti yake, ili kuepuka aibu ya kukataliwa na wabunge.

Hata hivyo, Spika alisema kwenye kanuni hakuna utaratibu wa namna hiyo. Makinda alisema kuanzia muda huo wa mchana hadi saa 11 jioni, marekebisho yatakuwa yamekamilika.

Shelukindo aliwataka wabunge bila kujali itikadi zao, warudishe imani kwa wananchi kwa kukataa kupitisha hoja hiyo.

Alilitaarifu Bunge kuwa angewasilisha hoja baadaye ya kutaka hoja hiyo ya waziri irudishwe ifanyiwe kwanza marekebisho kwa takribani wiki mbili, ndipo iletwe bungeni kwa mara nyingine.

No comments: