WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaita kwa faragha na kuwafokea wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaodaiwa kuomba rushwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Tanga kabla suala hilo kutolewa uamuzi rasmi na Spika, Anne Makinda, Raia Mwema, imeelezwa.
Wabunge wanaodaiwa kuomba rushwa, kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, (NCCR-Mageuzi) ni Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Zabein Mhita (Kondoa Kaskazini) na Omar Badwel (Bahi). Wote ni wabunge kutoka CCM. Pinda ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wote wa CCM.
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili kutoka katika duru za kibunge zinaeleza kuwa Pinda alikutana na wabunge hao siku kadhaa baada ya suala lao kuingizwa bungeni na Kafulila, wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
“Waziri Mkuu amewaita (wabunge watuhumiwa) amekuwa mkali na amewafokea. Imebainika hili suala lina uzito, baada ya kufuatiliwa kwa kina zaidi. Lakini amewafokea bila kueleza hatua zitakazochukuliwa dhidi yao na pengine amefanya hivyo kwa sababu hilo ni suala la Spika...limebeba taswira ya Bunge, japo Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM na anahusika na masuala ya serikali za mitaa kwa maana ya halmashauri, ikiwamo iliyoombwa rushwa,” alisema mtoa habari wetu.
“Hata wabunge wa CCM walikutana kujadiliana suala hili na kwa kweli limekuwa gumu kutolewa uamuzi wa moja kwa moja, isipokuwa kuna dalili za kutaka kulidhoofisha kwa sababu nyingi tu.
“Kama litashughulikiwa vizuri maana yake linaweza kufikishwa mahakamani na huko ni dhahiri linaweza kutusogeza katika uchaguzi mdogo kwenye majimbo hayo na wasiwasi ni kwamba upepo wa kisiasa haujatulia kwa CCM bado na suala la fedha ni gumu serikalini kwa sasa, unapofanya uchaguzi mdogo ni lazima fedha zitumike kuandaa, kusimamia na hadi kutangaza matokeo,” kilieleza chanzo kingine cha habari.
Taarifa zaidi zilizotufikia kuhusu suala hili zinaeleza kuwa Waziri Mkuu Pinda licha ya kuwa mkali kwa kuwafokea wabunge hao lakini amewaacha katika kitendawili juu ya hatima yao.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Pinda amefanya hivyo ili kutoingilia moja kwa moja mamlaka ya Spika, ambaye ndiye aliyeombwa mwongozo bungeni juu ya suala hilo ambalo pia limekwishafikishwa katika Kamati ya Uongozi ya Bunge, inayoundwa na wenyeviti wote wa kamati za kudumu za Bunge.
Wabunge hao watatu ambao wote ni kutoka CCM wanadaiwa kuomba rushwa katika Halmashauri ya Handeni, Tanga, wakiwa ni sehemu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema.
Hata hivyo, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliwahi kuzungumzia suala hilo bungeni muda mfupi baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kutoa tuhuma hizo alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Katika maelezo yake, licha kukanusha kuhusika, Zambi alisema ni mbinu za kumchafua kisiasa tu, yeye pamoja na chama chake (CCM) na kushinikiza aombwe radhi na Kafulila, ambaye hata hivyo, hakuomba radhi na kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa Spika, Anne Makinda.
Taarifa nyingine zinabainisha kuwa suala hilo pia limepokewa kwa shingo upande na baadhi ya wabunge wakiwamo wa Kambi ya Upinzani, wakieleza kuwa Kafulila ‘alifyatua’ suala hilo bila kuwajulisha wabunge wenzake wa Upinzani na zaidi, wajumbe wa kamati yake.
Hata hivyo, mara kwa mara Kafulila amekuwa akieleza kuwa mara baada ya kubaini tukio hilo la rushwa, aliripoti kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema, ambaye naye hakuweka nguvu ya kutosha katika kulishughulikia.
Mrema anadaiwa kulifikisha suala hilo katika Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo Mwenyekiti wake ni Spika na huko ndiko lilikokwama hadi sasa.
Wabunge hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa niaba ya baadhi ya wabunge wenzao katika kamati ya Mrema ili kufumbia macho ubadhirifu katika halmashauri hiyo ya Handeni.
Suala hilo la wabunge hao wa CCM linajitokeza katika wakati ambao chama hicho kipo kwenye mchakato wa kujisafisisha katika mfumo uliobatizwa jina la “kujivua gamba.”
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment