MBUNGE wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (CHADEMA) amelalamikia wabunge wanawake kudhalilishwa bungeni kwa kuitwa kuwa ni mzigo.
Bila kutaja chanzo cha kauli hiyo, Gekul katika swali la nyongeza, amesema, udhalilishaji wa wanawake haufanyiki katika maeneo ya stendi na sokoni, bali hata bungeni ambako alisema walisikika viongozi (bila kutaja majina) wakisema wabunge wanawake ni mzigo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani amesema leo bungeni mjini Dodoma kuwa, katika makosa ya namna hiyo, lazima awepo mlalamikaji.
Ameshauri kwamba, kama wanawake wameona wamedhalilishwa, waungane waende kwenye vyombo vya Dola kushitaki.
“Kama tumeona tumedhalilishwa ni vyema tukaenda kwenye vyombo vya Dola tukashitaki. Siwezi kuamuru kwamba wakamatwe. Kama tunaona tunadhalilishwa tuungane kwa pamoja tupeleke suala hili mahakamani,” amesema Kombani.
Awali, katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Mallac (Chadema), lililoulizwa na Gekul kwa niaba yake, alihoji sababu za sheria zinazodhibiti matusi kushindwa kuchukua mkondo wake kwa watu wanaotoa matusi hadharani.
Amesema, ingawa kutoa matusi hadharani ni kosa, imekuwa ni jambo la kawaida katika maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi hususani wapiga debe, vijiwe vya vijana kuwadhalilisha akinamama na watoto wa kike.
Akijibu swali hilo, Waziri Kombani alisema kutoa matusi hadharani ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi.
Amesema, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za nchi, imeweka makosa ya aina tatu yanayohusu utoaji wa matusi.
Katika kifungu cha 89 cha sheria hiyo inatamkwa kwamba mtu yeyote anayetumia lugha ya kudhalilisha aidha kwa kutamka au kwa ishara dhidi ya mtu yeyote katika hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani, atakuwa ametenda kosa la jinai na anapotiwa hatiani, atatumikia adhabu ya kifungu cha miezi sita jela.
Waziri amesema, katika kifungu cha 135 cha sheria hiyo, inatamka kwamba mtu yeyote atakayemdhalilisha mwenzake kwa kumbughudhi aidha kwa kutumia maneno, sauti au ishara au kitu kitakachoashiria matusi, akipatikana na hatia, atapewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano au kulipa faini ya Sh 300,000 au adhabu zote kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Waziri, katika kifungu cha 138D ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kufanya udhalilishaji wa kijinsia kwa mtu mwingine. Akitiwa hatiani, atapewa adhabu ama kifungo miaka mitano au kulipa faini Sh 200,000 au kupewa adhabu zote.
Hata hivyo, amesema, pamoja na makosa yanayohusu lugha ya matusi kuwemo katika sheria za nchi na adhabu zilizopo, bado sheria haiwezi kufanya kazi bila ya mtu aliyetendewa kosa au makosa ya aina hiyo kutoa taarifa kwenye vyombo vya Dola vyenye mamlaka ya kushughulikia makosa hayo.
“Napenda kushauri kwamba ili vyombo vya Dola ziweze kufanya kazi zake ipasavyo, tuwaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye vyombo vya Dola vinavyoshughulikia makosa ya jinai ili waweze kupata haki yao kwa wahalifu kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Waziri Kombani.
No comments:
Post a Comment