HUENDA katika siku 90 zijazo, wananchi wa jimbo la Igunga mkoani Tabora , wakaingia kwenye uchaguzi mdogo, baada ya Mbunge wao mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM ukiwamo ubunge.
Mbali na ubunge wa Igunga mkoani Tabora alioushikilia kwa miaka 18, Rostam pia ameachia ngazi nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM akiwakilisha mkoa huo.
Hatua yake imekuja siku moja baada ya kukamilika kwa siku 90 ambazo baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya CCM walidai zimetolewa kwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kupima mwenyewe uamuzi wa kujivua gamba.
Hata hivyo, wakati akizungumza na wazee wa Igunga jana, Rostam aliyewahi pia kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema kujiuzulu kwake hakuna uhusiano wowote na kujivua gamba.
“Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa, kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu,” Rostam aliwaeleza wazee wa Igunga.
Alisema CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, iliamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, anasema mabadiliko hayo ambayo Rais Kikwete aliyafananisha na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘kujivua gamba,’ licha ya kuungwa mkono na wajumbe wa iliyokuwa Kamati Kuu akiwemo yeye, yalipotoshwa na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti mpya ya CCM.
“Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye,” alieleza Rostam na kuongeza:
“Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku 90 wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.
“Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.
“Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu, kuwa ndio ambao walikuwa wakilengwa na uamuzi huo.
“Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.”
Rostam alisema mshangao na mshituko wake haukusababishwa na kutajwa kwa jina lake, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ “ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.
“Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa, kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC, uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
“Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti, wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi, umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.”
“Wazee wangu, ninyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa,” alisema Rostam mbele ya wazee hao.
“Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.
“Sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara.
“Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi, kwa sababu tofauti na wengine wengi nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa,” alieleza.
Hivyo, alisema amefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wake ambao anaamini baada ya kujitoa, watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizonazo za kuiongoza CCM na nchi kupitia Serikali yake.
“Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.
“Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alifafanua Rostam aliyechaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1994, akiziba nafasi ya marehemu Charles Kabeho.
Kwa upande mwingine, alisema uamuzi wake anaona ni fursa kwa viongozi wa CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama hicho, ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.
Alisema pia ana imani thabiti kwamba, uamuzi wake wa kubaki kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM, utakuwa chachu kwa chama hicho na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.
Hata hivyo, alisema anaondoka Igunga akiacha mafanikio makubwa katika jimbo hilo na mkoa wa Tabora kwa jumla.
“Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani hapa, lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya,” alisema Rostam.
Lakini pia alimpongeza Rais Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanyia nchi. “Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania.
“Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa jumla; tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndizo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo,” aliomba.
Rostam amekuwa miongoni mwa wanasiasa maarufu wa Tanzania tangu aliposhinda ubunge mwaka 1994 na mwenye nguvu ndani ya chama hicho, kiasi cha kuweza kushinda ujumbe wa NEC mwaka 2007 na kuwamo katika timu ya kampeni ya Rais Kikwete mwaka 2005.
Hata hivyo, pamoja na mchango wake mkubwa katika kampeni hizo, hajapata kupewa nafasi yoyote ya uwaziri naye mara zote ameridhika akielekeza zaidi nguvu katika biashara zake kama alivyobainisha hayo jana katika hotuba yake.
Katika Sekretarieti ya Kwanza ya CCM baada ya Uchaguzi Mkuu alikuwa Mweka Hazina wa Chama, kabla ya mabadiliko yaliyomtupa nje na kumbakiza na wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu hadi kujiuzulu Aprili.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, amehusishwa na kashfa mbalimbali nchini zikiwamo za ufisadi, yeye na mawaziri wawili wa zamani, Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa na Andrew Chenge ambaye pia alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Watatu hao wamekuwa wakitajwa katika kashfa za Richmond, EPA na rada na majina yao yalitajwa na akina Nape na Chiligati, kuwa wanapaswa kujivua gamba.
Hatua ya kujiuzulu jana, sasa inafanya macho na masikio ya wengi kuelekezwa kwa watuhumiwa wenzake hao, Lowassa na Chenge, ambao nao kama Rostam walipewa na CCM muda wa kupima.
Akizungumzia kujiuzulu kwa Rostam, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi, alisema kuachia ubunge kwa Rostam hakutoathiri chama hicho na kwamba ni haki yake na demokrasia inayotekelezwa nchini.
“Jimbo la Igunga halitoathirika na kujiuzulu kwake, CCM tunaamini jimbo hili likitangazwa kuwa liko wazi, tunao watu wengi wenye sifa ambao wanaweza kulirejesha kwa chama chetu,” alisema.
Alisema hata Rostam mwenyewe alipojiuzulu aliweka bayana kuwa atasaidia kuhakikisha kuwa jimbo hilo linabaki CCM, hivyo chama hicho kitajipanga wakati ukifika, kuhakikisha kuwa hilo linawezekana.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alisema demokrasia ya Tanzania inatoa uhuru kwa mtu au kiongozi kutoa uamuzi kama wa Rostam pale atakapoona inafaa, hivyo uamuzi wa kujiuzulu kwa mbunge huyo ni haki yake.
Alisema kinachofuata sasa ni kwa mbunge huyo kufuata taratibu ambazo ni kuandika barua ya kujiuzulu kwa Ofisi ya Bunge ili jimbo hilo lijulikane liko wazi na kwa mujibu wa sheria, uchaguzi mdogo unatakiwa kufanyika siku 90 baada ya kutangazwa kuwa wazi.
Naye aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, alisema Rostam amejiuzulu nafasi zake zote za ubunge na chama kwa nia safi na ni habari njema kwa chama.
“Unajua kama kiongozi umekuwa ukisemwa kwa muda mrefu kwa mabaya ni vyema ukajiuzulu ukapisha wengine nao waongoze na kuonesha uwezo wao,” alisema Kimiti.
Hata hivyo, alionya haitakuwa busara iwapo mbunge huyo atakuwa amejiuzulu kwa nia mbaya na kuanzisha makundi ndani ya chama, lakini alipongeza uamuzi wa kiongozi huo na kuuita wa hekima.
Hussein Bashe, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema falsafa ya kujivua gamba inatumika vibaya na kusema nchi ina mambo mengi lakini siasa za chuki zinapewa kipaumbele na ndiyo sababu hata bungeni zimeingia na watu wanasema ovyo ovyo.
No comments:
Post a Comment