Wednesday, July 20, 2011

Posho elimu ya juu yapanda kwa Sh 2,500/-

SERIKALI itaongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutoka Sh. 5,000 ya sasa hadi Sh. 7,500 katika mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka huu.

Alisema, kiasi cha Sh. bilioni 77.8 kitatumika kwa suala hilo na wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo na kwa wanaosoma shahada za uzamili na uzamivu, wanatarajiwa kupewa mikopo kwa mwaka 2011/12.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) itaimarisha utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa kuainisha taarifa za wakopeshwaji na zile za Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Mitihani na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

Alisema pia Bodi hiyo itasogeza huduma za utoaji mikopo karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi ya kanda Zanzibar.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu wizara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta , alisema ili kuimarisha uwezo wa Serikali kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi, Kamati yake ilishauri Serikali itafute mbinu mbadala za kupata fedha ili kuinua uwezo wa kutoa mikopo mwaka hadi mwaka.

Alisema, ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2006, kiundwe chombo mahususi chini ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ili kufuatilia ukusanywaji wa marejesho ya mikopo iliyokwishatolewa.

Alisema, taarifa za mikopo husika zitambulike kwa walengwa ili kurahisisha ukusanyaji wa fedha hizo kwa ushirikiano wa mwajiri na Bodi ya Mikopo na kuwa fedha za marejesho ya mikopo hiyo zitambulike bayana, kwa kuonekana katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu kila mwaka.

Pia Kamati ilishauri utoaji vitambulisho vya Taifa ukamilike ili kutambua wanafunzi wanaokopa na waliokopa na uraia wao, ambapo pia Kamati ilishauri kuwapo udhibiti wa karo hasa katika vyuo visivyo vya Serikali.

Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM), alishauri kutokana na utata katika urejeshwaji wa mikopo, Serikali itoe fedha hizo bure kwa wanafunzi badala ya kuwakopesha.

Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo kwa Wizara ya hiyo Cristowaja Mtinda, alisema kutokana na muundo wa Bodi ya Mikopo na uendeshaji mbaya, kuna haja ikavunjwa kwani imeshindwa kuifanya elimu ya juu ipatikane kwa kila mwanafunzi anayestahili.

Alisema Bodi hiyo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 mwaka uliopita, lakini ilikusanya marejesho ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.9 kati ya Sh. bilioni 21 zilizotarajiwa kukusanywa.

“Kutokana na sababu hizo, Serikali iazimie kuivunja Bodi hii, pamoja na kufanya uchunguzi huru wa fedha zilizotumika chini yake hadi sasa na kujiridhisha kama waliopewa dhamana hii hawakutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi,” alisema.

Alisema baada ya Bodi hiyo kuvunjwa, Serikali iunde chombo kipya kitakachojulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (TAHEFA), ambacho kitachukua majukumu yote ya Bodi.

No comments: