WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema hali ya kuvunjika kwa umoja wa Watanzania inayojionesha Tanzania Bara inamwogofya.
Ametoa mfano wa shughuli za kijamii kama maziko zinazofanyika kisiasa kuwa ingawa ni za jamii, lakini vyama vya siasa vinapoingilia, vinasababisha jamii yenye itikadi tofauti kushindwa kushiriki.
Warioba alisema hayo juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV kila Jumatatu na kutoa mfano wa maziko ya diwani wa Shinyanga bila kumtaja jina, ambayo yaliendeshwa kichama.
Maziko hayo ni ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Masekelo katika Manispaa ya Shinyanga, Philipo Shelembi (Chadema), Aprili ambapo Chadema walimzika kichama.
Mbali na Chadema, hata CCM wamekuwa na utaratibu wa kuzika makada wake wakiwamo viongozi waliochaguliwa na wananchi katika nafasi mbalimbali kwa heshima za chama, ikiwemo kufunika jeneza kwa bendera ya chama na watu waliovalia sare za chama kubeba mwili.
Warioba alisema mazishi ni shughuli za kijamii na zinapaswa ziendeshwe kijamii, lakini hali ya sasa ya vyama kuingilia shughuli hizo kisiasa, inasababisha jamii yenye itikadi tofauti ya kisiasa kuacha kushiriki.
“Lazima Watanzania tutafakari, hili ni jambo la hatari katika umoja wetu ni kama ilivyokuwa Zanzibar, watu walisusiana harusi na mazishi, sasa inaanza kuoneka Bara, inaniogopesha,” alisema Warioba.
Alizungumzia tuhuma za udini na kufafanua kuwa zinatolewa na wanasiasa hasa wakati wa uchaguzi, lakini wananchi katika hali yao ya kawaida, wanaishi bila tofauti hizo na kusisitiza umuhimu wa kuweka mambo ya umoja kutochezewa kisiasa.
Pia alitofautiana na mitazamo ya wanasiasa kuita Serikali ya chama; kama CCM wanavyosema kuwa Serikali iliyoko madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi na kuhoji iliko Serikali ya Tanzania.
Alifafanua kuwa, vyama vya siasa ni utaratibu tu wa kuwapa Watanzania viongozi, lakini kiongozi atakayeshinda katika uchaguzi, anaacha kuwa wa chama na badala yake anakuwa wa Watanzania.
Pia alipinga mamlaka ya vyama vya siasa kuadhibu viongozi waliochaguliwa na Watanzania: “Wakati wa mjadala wa Katiba mpya, itabidi Watanzania wajadili madaraka yako wapi? Kwenye vyama au kwa wananchi?” Alihoji.
Alitoa mfano wa uamuzi wa madiwani wa Chadema Arusha kufikia mwafaka na wenzao wa CCM lakini Chadema ikaagiza waachie madaraka; na kusema waliowachagua ni wananchi kwa nini chama kiwanyang’anye madaraka ambayo si ya chama?
Kuhusu kero za Muungano, Warioba alisema walioungana ni Watanzania, lakini itabidi wakati wa mjadala wa Katiba mpya, hilo lijadiliwe kama zilizoungana ni Serikali au Watanzania.
Alitoa mfano wa mambo ambayo viongozi wamekuwa wakisema yaliongezwa katika orodha ya Muungano na kuongeza kwamba ingawa ardhi si sehemu ya mambo ya Muungano, lakini Watanzania wa upande wowote wa Muungano wanaweza kudai ardhi kama haki yao na kuipata.
Alisema hata biashara si jambo la Muungano, lakini Watanzania kutoka upande wowote, wanaweza kudai haki yao ya kufanya biashara sehemu yoyote ya Muungano na kupewa.
No comments:
Post a Comment