Monday, July 4, 2011

Chadema macho yawatoka Arusha

MGOGORO uliofumuka baada ya mwafaka kati ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeziweka pande hizo mbili njia ya panda.

Tume iliyoundwa imegundua kwamba pande zote mbili zinazolumbana katika Chadema zinabeba aina fulani ya lawama katika mchakato wa mwafaka, mwafaka wenyewe na kutangazwa kwake.

Imebainika kwamba pamoja na kelele za Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, kuhusu mwafaka huo, inadaiwa kwamba yeye (Lema) ameamua kuwaruka tu viongozi wenzake wakati akijua fika juu ya maendeleo ya vikao hivyo na hatimaye kufika mwafaka huo.

Hivi karibuni, madiwani wa Chadema Arusha waliopinga kumtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo kwa madai hakuchaguliwa kihalali, waliamua kuondoa tofauti zao na kumtambua Lyimo na kueleza kuwa muafaka huo ni kwa maslahi ya wananchi wa kata zao.

Mwafaka huo ulipingwa vikali na Lema na kueleza kuwa ni batili na hauna baraka za viongozi wa juu wa Chadema; hatua iliyopingwa na madiwani hao na kudai kuwa kauli ya mbunge huyo ni batili yenye kulenga kutaka kuwachafua kwa wananchi.

Walidai kwamba Mbunge Lema na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho wana taarifa asmi ya tukio hilo la mwafaka.

Katika majumuisho ya Tume ya Chadema yenye wajumbe wanne iliyokuwa ikiongozwa na Mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando, imebaini mtafuruku huo na kusikitishwa kukuzwa kwa tatizo hilo na Lema kwa kukimbilia kutangaza kutoutambua mwafaka huo
wakati akijua wazi kuwa anajua kinachoendelea, hatua ambayo ilieleza kuwa kwa kiongozi kama yeye hakupaswa kufanya hivyo.

Tume hiyo iliyomaliza kazi yake Julai 2 kwa kuwahoji madiwani wote na baadhi ya viongozi wa Chadema Wilaya na Mkoa, inaelezwa kuwa ilibainika kupitia mahojiano na watendaji
hao kuwa kila kiongozi alikuwa akijua hilo ikiwemo vikao vya awali kabla ya kufikia mwafaka.

Aidha, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Tume imewalaumu madiwani wa Chadema waliofikia mwafaka huo wakiongozwa na Naibu Meya Estomih Mallah kwa kuwa na haraka ya kuutangaza bila kusubiri kauli ya mwisho ya viongozi wa juu wa Chadema Taifa.

“Ni kweli Tume tumebaini kila kitu kilikuwa kinajulikana kwa viongozi wa Chadema Wilaya, Mkoa na Taifa na hata Mbunge Lema, lakini mlipaswa kusubiri kauli ya mwisho kabla ya kuutangaza muafaka huo!

“Hilo hapo ni tatizo lazima mkubali mmekosea lakini tatizo hilo sio kubwa kama lilivyokuzwa,” alisema mtoa habari wetu akimkariri Marando wakati wa majumuisho ya
pamoja.

Katika kujitetea kwa mara ya mwisho mbele ya Tume hiyo, mmoja wa madiwani (jina tunalo), anakaririwa akisema walishindwa kusubiri kauli ya mwisho ya viongozi wa juu wa Chadema kwa madai ya kuwa wazito katika kutoa kauli ya mambo mengi ya kichama na ndio maana walitoa muda bila majibu na kuamua kuendelea na taratibu za muafaka.

Diwani huyo alidai hata Lema alipigiwa simu kuelezwa taratibu za mwisho zilipofikia juu ya mwafaka huo, na pia alikaa kimya.

“Mheshimiwa Mwenyekiti hapa nani wa kulaumiwa, ni sisi ama hao wanaopata taarifa, lakini wanashindwa kuzitolea maamuzi na kuzikalia?

Jibu, wa kulaumiwa juu ya mwafaka huu ni viongozi wa juu wa Chadema na Mbunge Lema,” alikaririwa akidai diwani huyo.

Taarifa ndani ya kikao hicho zilidai kwamba madiwani walieleza kuwa msimamo wao uko pale pale kwa maslahi ya wakazi wa Arusha na kueleza kuwa madiwani, viongozi wa chama hicho wa ngazi zote kuwa mstari wa mbele kueleza ukweli na sio kutaka kupotosha umma kwa kujitafutia umaarufu kwa njia ya upotoshaji.

Chanzo chetu cha habari kiliwakariri madiwani hao wakimtaka Marando kumuonya Mbunge Lema kuacha mara moja kutoa kauli za kejeli dhidi yao kuwa wamenunuliwa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ili waingie katika kamati mbalimbali za Jiji ili wawapitishie zabuni zao.

Madiwani hao walieleza kukasirishwa na kauli hiyo na haitavumiliwa na kumtaka mbunge
huyo akanushe, vinginevyo watapeleka katika vyombo vya sheria.

Baada kumalizika kwa majumuisho hayo na kila diwani kutoa kauli yake, Marando aliwaambia kuwa wamemaliza kazi na wanapeleka taarifa hiyo kwa viongozi waliowatuma ili waamue nini cha kufanya.

Julai 3 Marando alipopigiwa simu na gazeti hili kueleza walichokigundua Arusha baada ya kazi hiyo, alisema atafutwe Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kwani ndiye aliyewatuma.

No comments: