KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, amepewa likizo kuanzia leo ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili na kupata ukweli kabla ya hatua zingine kuchukuliwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, alisema jana mjini Dodoma kwamba, yeye ndiye mwenye mamlaka ya nidhamu na kwa kuwa tuhuma zinazomhusu Jairo ni za fedha, amemteua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kumpa siku 10 afanye uchunguzi wa awali.
Luhanjo alisema, ndani ya siku kati ya mbili na tatu, atakuwa amemteua mtu wa kukaimu nafasi hiyo, wakati Jairo akiwa katika likizo hiyo ambayo ni ya malipo. “Siku mbili, tatu mtasikia nani nimemteua,” alisema Luhanjo.
Katibu Mkuu Kiongozi alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na kusema tuhuma dhidi ya Jairo ni nzito hali ambayo imemlazimu kuamua aende likizo licha ya kwamba Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, inaruhusu mtuhumiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa.
Kwa mujibu wa Luhanjo, tuhuma zinazochunguzwa ni zilizotolewa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini.
Baadhi yao ni pamoja na kuzitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo, zichangie Sh milioni 50 kila moja, ili fedha hizo zitumike kulipa wabunge na kufanikisha mawasilisho ya makadirio hayo.
Tuhuma zingine ni za kulipa masurufu ya safari watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walishalipwa na wizara na taasisi hizo.
“Hataendelea na kazi kipindi cha uchunguzi. Hatua zaidi zitategemea uchunguzi huo wa awali… nimeamua niseme, msianze kubashiri, kwamba tunamsubiri Rais aliyemteua, mimi ndiye mwenye mamlaka … nikipata taarifa ya uchunguzi wa awali, nitampa notisi ya matokeo ya awali,” Luhanjo aliwaambia waandishi wa habari.
Uamuzi wa kusisitiza kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka, unatokana na vyombo vya habari jana kuchapisha taarifa zikimkariri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa uamuzi juu ya Jairo unamsubiri Rais Jakaya Kikwete.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari ambao Luhanjo alifuatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo na waandishi wa Waziri Mkuu, Luhanjo alitoa somo kwa waandishi wa habari juu ya utaratibu wa kushughulikia tuhuma dhidi ya mtumishi wa umma.
Luhanjo alisema kulingana na Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, mwenye mamlaka ya nidhamu kwa mtumishi yeyote wa umma anayetuliwa na Rais kasoro wanasiasa, mawaziri na wakuu wa mikoa, ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Alisema katika kushughulikia tuhuma zinazomkabili mtumishi wa umma, lazima uchunguzi wa awali ufanyike kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, ili kubaini kama mtumishi husika ametenda kosa la kinidhamu.
“Katika kipindi cha uchunguzi, mtumishi anayetuhumiwa, anaweza kupewa likizo ya malipo ili kupisha shughuli za uchunguzi au akaruhusiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa,” alisema Luhanjo.
Alifafanua kwamba kama uchunguzi wa awali dhidi ya Jairo, utabaini makosa ya kinidhamu, Mamlaka ya Nidhamu itampa taarifa za tuhuma ambazo zitaambatana na hati ya nashitaka, itakayoelezea kwa ufupi kosa alilotenda na ni lini anapaswa awe amejibu tuhuma husika. Mtuhumiwa anapaswa asimamishwe kazi na kulipwa nusu mshahara.
“Mtuhumiwa atatoa maelezo yake kwa mujibu wa hati ya mashitaka aliyopewa. Anaweza kukataa au kukubali. Akikubali, Mamlaka ya Nidhamu itaendelea kutoa adhabu kulingana na uzito wa kosa. Adhabu inaweza kuwa kufukuzwa kazi, kupunguzwa cheo au kupunguzwa mshahara ama adhabu nyingine iliyoelekezwa na Sheria ya Utumishi wa Umma.
“Iwapo atakana mashitaka, Mamlaka ya Nidhamu itaunda Kamati ya Uchunguzi itakayopewa hadidu za rejea ambazo pamoja na mambo mengine, zitaeleza muda wa uchunguzi huo kukamilika. Taarifa ya kamati itawasilishwa kwa Mamlaka hiyo, ikiwa na mapendekezo.
Ikumbukwe kuwa Kamati hii haitoi adhabu kwa mtuhumiwa isipokuwa inatoa mapendekezo tu,” Luhanjo alisisitiza. Baada ya taarifa ya kamati ya uchunguzi, Luhanjo alisema Mamlaka itaendelea kutoa adhabu kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo. Kama adhabu itakuwa ni kuvuliwa madaraka, Mamlaka ya Nidhamu itawasiliana na Mamlaka ya Uteuzi kuhusu kutekeleza suala hilo.
Hata hivyo, Luhanjo alisema iwapo mtuhumiwa hajaridhika na uamuzi unaoishia kwa Mamlaka ya Nidhamu, sheria zinampa fursa ya kukata rufaa kwa Rais. “Rais ana mamlaka ya kuthibitisha au kukataa uamuzi wa Mamlaka ya Nidhamu,” alisema.
Tuhuma dhidi ya Jairo ziliibuliwa Julai 18 bungeni na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM). Jana katika maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF) alihoji sababu za uamuzi wa kumwajibisha Jairo kumsubiri Rais Kikwete wakati yupo Makamu wa Rais anayefanya kazi kwa niaba yake.
Mbunge huyo alisema kufanya hivyo ni kinyume na Katiba ambayo katika Kifungu cha 47 (1) (c) ana mamlaka ya kufanya kazi zote za Rais anapokuwa amesafiri nje ya nchi. “Ulitoa kauli bungeni kwamba huna mamlaka ya kumwajibisha Katibu Mkuu, unamsubiri Rais. Je huoni kwa kufanya hivyo umekiuka kanuni za Katiba?” alihoji Abdallah.
Akijibu, Pinda alisema kulingana na Katiba, si kila jambo wanaopewa dhamana wanapaswa kutoa uamuzi.
Alisema pamoja na kwamba Katiba inaelekeza pia Waziri Mkuu kupewa mamlaka iwapo Makamu wa Rais hayupo, wana kikomo cha madaraka. “Tusitafsiri kipengele hiki kwamba Rais akiondoka ndio sasa umepewa unga,” alisema Pinda.
Pinda aliwaambia wabunge kuwa suala hilo angeliwasilisha kwa Rais Kikwete aliyekuwa ziarani Afrika Kusini kwa kile alichosema ndiye mwenye uamuzi, kwa kuwa ndiye aliyemteua.
Juzi Waziri Mkuu akawaambia tena waandishi wa habari kuwa alipowasiliana na Rais, alimwambia asubiri arejee nchini ndipo uamuzi utolewe kuhusu sakata hilo.
No comments:
Post a Comment