Thursday, July 28, 2011

Si kweli kwamba hatuwezi kuchimba wenyewe madini

-Asema juhudi za kumchafua Mwalimu hazitafanikiwa
-Ashangaa viongozi kusaliti juhudi zake
-Atamba CHADEMA imebadilisha mambo Musoma Mjini

JULAI 3, mwaka huu, Mwandishi, Godfrey Dilunga wa Raia Mwema, alifanya mahojiano na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ni mbunge wa kwanza jimbo hilo kutoka Upinzani tangu Uhuru wa Tanganyika.

Raia Mwema: Jina la Nyerere linaashiria unatoka katika familia kubwa katika siasa za Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla; yaani familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tueleze uhusiano uliopo kati yako na Mwalimu Nyerere.

Nyerere: Kwanza nikueleze jambo ambalo wengi hawalifahamu. Jina langu mimi haswa si Vincent. Jina langu ni Nyerere tangu kuzaliwa, hili la Vincent ni jina la ubatizo. Ni sawa hata kwa Mwalimu Nyerere, jina lake la kuzaliwa ni Kambarage. Hili jina la Julius ni jina la ubatizo.

Kwa hiyo, Mwalimu Nyerere jina la Julius na Kambarage yote ni ya kwake. Hakuna jina la mzazi wake hapo. Julius jina la kubatizwa na Kambarage jina la kienyeji kabla kubatizwa.

Sasa kama ulivyoniuliza, mimi ni mtoto wa Josephat Nyerere ambaye yeye na Mwalimu Nyerere ni mtu na mdogo wake. Huo ndiyo uhusiano uliopo ndani ya familia yetu hiyo.

Raia Mwema: Familia ya Nyerere imejikita zaidi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ingawa wakati fulani Makongoro Nyerere aliwahi kuwa mbunge wa NCCR-Mageuzi Arusha. Wewe imekuwaje ujiunge na Upinzani, hususan CHADEMA?

Nyerere: Kwanza ni suala la kuelewa zaidi. Unajua hii ni nchi yetu sote, masuala ya vyama ni utaratibu tu lakini msingi mkuu ni uongozi utakaowaletea wananchi maendeleo kwa kadiri ya matarajio yao.

Mimi ni mkazi wa Musoma, nafanya shughuli zangu pale muda mrefu. Katika uongozi uliokuwapo (ubunge) nilikuwa naona mambo mengi hayaendi sawa; hasa masuala ya maendeleo na uhusiano wa kisiasa kati ya mbunge na sehemu kubwa ya wananchi.

Hali hiyo ilinishawishi kutaka kugombea ubunge na niliamini kwamba nitaweza kugombea na kwa kusaidiana na wakazi wenzangu wa Musoma Mjini ningeshinda na tungeshirikiana ili kushinda kwa pamoja kujiletea maendeleo.

Raia Mwema: Nani alikuwa wa kwanza kumdokeza wazo lako hili la kutaka kugombea ubunge?

Nyerere: Mtu wa kwanza kabisa ni kaka yangu Makongoro Nyerere. Nilimweleza dhamiri yangu, lakini hakutaka kuniunga mkono. Alinishauri niache masuala hayo kwa wakati huo, nijipe muda wa kutafakari zaidi. Lakini ushauri wake niliuheshimu japo sikuutekeleza kama alivyotaka.

Baadaye niliwaeleza pia baadhi ya wakazi wenzangu wa Musoma Mjini kuhusu suala hilo, wakiwamo pia rafiki zangu. Walishangaa na kuniuliza unazo fedha? Umezipata wapi?

Raia Mwema: Kwa nini walikuuliza suala la fedha?

Nyerere: Waliniuliza hivyo kwa sababu ilikuwa ni utamaduni, ukitaka kugombea ubunge na hasa Musoma Mjini lakini pia hata mbunge aliyekuwapo alikuwa na fedha nyingi. Kwa hiyo waliamini ili kushindana naye ni lazima nawe uwe na fedha za kutosha.

Kwa hiyo, fikra zilizokuwapo ni uchaguzi unaoongozwa na nguvu ya fedha na si masuala ya uadilifu au uwezo wa kuunganisha wananchi katika maendeleo.

Raia Mwema: Uliichukuliaje hali hiyo, uliogopa na kufirikia upya kukimbia uamuzi wako wa kutaka ubunge?

Nyerere: Haikunikatisha tamaa na kimsingi niliichukulia kama changamoto ya kufanikisha nia yangu, nikizingatia kuwa sehemu kubwa ya wananchi ambao ni wapiga kura hawana fedha kama ilivyo kwangu na pengine wengine hawana fedha zaidi....ni masikini.

Niliamini watu namna hiyo ndiyo mtaji wangu, nitawaelewesha na bila shaka watanielewa na kwa kweli walinielewa kila hatua niliyofanya waliniunga mkono hadi nikawa mbunge na kampeni zangu zilikwenda vizuri sana.

Raia Mwema: Mwanzo ulieleza mshauri wako wa kwanza alikuwa Makongoro Nyerere, kuna masuala fulani awali mliwahi kushirikiana hasa katika siasa? Nini kilishawishi hasa uanze kumfuata yeye ili umueleze wazo lako?

Nyerere: Ni kweli kwamba Makongoro amewahi kuwa mbunge wa NCCR-Mageuzi na anajua masuala haya, lakini pia mimi niliwahi kuwa kampeni meneja wake wakati anagombea uenyekiti wa CCM - Mkoa wa Mara.

Niliendesha kampeni zake vizuri na akashinda. Kwa hiyo, katika masuala ya siasa tuko karibu zaidi na hata masuala mengine.

Raia Mwema: Kumekuwapo na madai kwamba; ingawa yeye ni CCM lakini alikuwa akikusaidia kampeni zako za ubunge hadi ukashinda. Unazungumziaje hili?

Nyerere: Ukiliweka hivyo, unakuwa umekosea. Leo niseme wazi kwamba walionisaidia ni wana-CCM karibu wote wa Musoma Mjini, na walifanya hivyo kwa sababu maalumu, ukiwamo udhaifu wa mbunge aliyekuwapo na ambaye ndiye aliyepitishwa na chama chake kugombea ubunge.

Kwa hiyo, si Makongoro aliyenisaidia na kwa kweli yeye mwenyewe alikwishawahi kufanya kampeni dhidi yangu, akimnadi mgombea wa CCM. Ndiyo, alikuwa akifanya mikutano mbalimbali ya kampeni ya chama chake lakini mimi nilikuwa na wana-CCM wa kawaida, walinisaidia kwa hali na mali. Amewahi kufanya mkutano Shule ya Msingi Mkendo, akamnadi mgombea wa CCM sio mimi. Kwa hiyo, si kweli kwamba alinisaidia.

Na kwa kweli, hiyo imekuwa changamoto kubwa sana kwangu; kwa sababu hawa watu wote walionichagua wamekuwa na matarajio makubwa kwangu lakini nashukuru kazi yangu inakwenda vizuri na kumeanza kutokea mabadiliko makubwa ya maendeleo jimboni. Ni changamoto na nitahakikisha wana-CCM hao na wananchi wengine kwa ujumla hawajutii uamuzi wao huo hata siku moja.

Raia Mwema: Umezungumzia udhaifu wa mbunge aliyepita ndiyo sehemu ya nguvu zilizochangia ushindi wako. Ni udhaifu gani huo?

Nyerere: Hilo liko wazi, sio la kuficha ni suala linalojulikana Musoma Mjini. Huyo mbunge alihodhi biashara karibu zote kubwa Musoma Mjini, madiwani karibu wote wakati huo walikuwa wakandarasi. Kwa hiyo, miradi mingi ya Halmashauri ilikuwa ikizunguka katika ‘himaya’ yao. Wachache pale Musoma Mjini walionekana kuwa na maisha mazuri zaidi, kwa hiyo alijenga mtandao wake kwa kuhakikisha wenye maamuzi ndiyo wanaonufaika, akasahau wananchi wa kawaida.

Lakini pia hakuwa ametekeleza ahadi zake nyingi za maendeleo kwa wananchi wa jimbo la Musoma Mjini.

Raia Mwema: Katika akili ya kawaida, kuna mantiki mtu akisema jina kubwa la Mwalimu Nyerere limekusaidia pia kushinda. Unakubaliana na mantiki hii hasa ukizingatia siku hizi watoto wa wakubwa wamekuwa vinara wa mikakati ya kisiasa?

Nyerere: Unachosema wengi ndiyo wanachokizungumza ambacho si kweli kwangu na hata katika familia yetu kwa ujumla. Hili suala la kufanya siasa kwa kutumia surname (jina la ukoo) hazipo kwangu wala kwa yeyote kwetu na kimsingi sio siasa pekee, hata masuala mengine.

Mimi nimekuwa mfanyabiashara lakini sijawahi kufanya mambo yangu kwa kutumia nguvu za surname, na hivyo ndiyo malezi yetu yalivyokuwa.

Sisi tumekuwa tukiishi maisha ya kawaida, tumesoma shule za kawaida na mimi mwanangu anasoma shule hizo hizo. Kwa hiyo, hatufanyi siasa za surname.

Kwanza, mimi na wanafamilia wenzangu tunajivunia kuwa katika ukoo huo lakini hakuna anayetumia jina hilo kwa manufaa fulani binafsi. Hata wazazi wetu hawakuwa hivyo, kumbuka walikuwa watoto wa chifu, lakini hakuna aliyejigamba na cheo hicho. Hata maisha yetu, hatukutumia umaarufu wa Mwalimu Nyerere akiwa Rais na hata alipostaafu kwa manufaa yetu.

Hatukuwa tukiishi maisha ya ki-Ikulu-ikulu, wakati Mwalimu akiwa Rais. Tuliishi maisha ya kawaida na kusoma shule za kawaida ambazo zilikuwa bora zaidi.

Raia Mwema: Inaelezwa kwamba Mwalimu aliwekeza muda wake zaidi kutumikia nchi kuliko familia na watoto wake hakuwapa elimu nzuri nje ya nchi au popote na hakuiachia mtaji au raslimali nyingi kama ilivyo kwa marais wengi Afrika. Ukweli ukoje hapa?

Nyerere: Ni kweli Mwalimu Nyerere alitumia muda wake mwingi kutumikia nchi pengine ukilinganisha na masuala ya familia, na kwa kweli hilo ni jambo la kujivunia kwa sababu ni kigezo cha kiongozi bora katika uongozi wa juu wa nchi.

Ukitazama viongozi wengi waliotumia nafasi zao za uongozi kutumikia familia zao badala ya Taifa hawakufika mbali. Walijenga uadui mkubwa na wananchi wao na matokeo yake hata usalama wa familia zao unakuwa shakani. Wewe unajua kinachoendelea katika baadhi ya nchi Afrika, kama Misri na kwingine. Viongozi wamechuma mali nyingi, wamesahau wananchi wameondoka madarakani hawana heshima yoyote, lakini angalia Mwalimu Nyerere, katumikia wananchi na bado heshima yake ipo hadi leo.

Kuhusu hili suala la kutosomesha watoto wake, hebu niambie mtoto gani wa Mwalimu Nyerere hakusoma vizuri? Wote wamesoma vizuri. Pengine suala ni kwamba wamesoma katika shule za kawaida kama ilivyo kwa watoto wengine wa masikini hapa nchini. Mwalimu alisomesha watoto wake lakini katika shule za kawaida, si za kifahari.

Raia Mwema: Tueleze, uliingia CHADEMA ili kugombea ubunge...ulikuwa mwanachama wa muda gani kabla ya uchaguzi mkuu, na kabla ya hapo ulikuwa katika chama gani?

Nyerere: Kwanza sikuwa mwanachama wa chama chochote isipokuwa nilikuwa shabiki wa CCM. Hata nilipokuwa meneja wa kampeni za Makongoro nilikuwa shabiki mkubwa wa CCM.

Baadaye nilijiunga na CHADEMA Oktoba 20, mwaka 2008, miaka takriban miwili kabla ya uchaguzi.

Raia Mwema: Kwa nini hukujiunga rasmi na CCM na badala yake ukaenda CHADEMA?

Nyerere: Kwanza si kosa kujiunga na CHADEMA, na kwa kweli ni kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye Watanzania karibu asilimia 80 walitaka chama kimoja; yeye akashauri mfumo wa vyama vingi uanzishwe kwa sababu maalumu.

Kwa hiyo, nilifuatilia sera na misimamo ya CHADEMA ikaniridhisha kuwa naweza kuwa mwanachama wa chama hicho.

Lakini pia wengi walishangaa wakaanza kusema kuwa nakwenda CHADEMA kuharibu, kufanya kazi ya CCM. Kwamba eti mimi ni mamluki lakini kwa kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele walithibitisha si kweli.

Raia Mwema: Turejee jimboni, hali ikoje jimboni kwako. Kuna vikwazo vyovyote katika kufanya kazi yako, hasa ikizingatiwa ni mbunge wa Upinzani?

Nyerere: Kwanza nikueleze, Musoma Mjini kuna kata 13, CHADEMA tumeshinda kata nane kwa hiyo tunaongoza Halmashauri ya Manispaa.

Mimi mwenyewe mbali na ubunge ni diwani wa kata ya Mkendo; maana wananchi walitaka pia nigombee udiwani. Hii kata ndiyo yenye Ikulu ndogo, ofisi za serikali kama Mkuu wa Mkoa, magereza, polisi na mahakama.

Sasa katika utekelezaji, mwanzo tulipoingia madarakani watendaji wengi wa Halmashauri walituona kama maadui. Na kwa kweli tuligundua matatizo mengi. Kwa mfano, Halmashauri ilikuwa ikidai wafanyabiashara wengi ambao baadhi ni viongozi wakubwa CCM, yumo hadi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM-Taifa (NEC), Gachuma. Tunamdai fedha nyingi kwa muda mrefu na tuko imara kudai fedha hizi kwa wote wanaodaiwa na Halmashauri.

Tumekuwa tukipata hisia kwamba wengine wamekuwa wakifanya siasa ili wapate miradi ndani ya Halmashauri na kufanya mizengwe mingine ya kuikosesha Halmashauri mapato kwa wakati.

Lakini kwa sasa watendaji wengi wa Halmashauri wamegundua kuwa sisi ni wenzao katika kupigania maendeleo ya jimbo na wanatuunga mkono; japo wapo wachache wenye wasiwasi na inawezekana ndiyo waliokuwa wakinufaika na uongozi mbovu uliopita.

Hali ya miundombinu tumeanza kurekebisha, mifereji inazibuliwa na kujengwa, barabara zinafanyiwa kazi na tumeagiza makandarasi wawe wanatoa taarifa kwa mwananchi yeyote atakayewauliza.

Raia Mwema: Wapo wanaosema Mwalimu Nyerere alikuwa mdini, ukiwa ndani ya familia, hili umewahi kulibaini?

Nyerere: Hapana, Mwalimu hakuwahi kuwa mdini na alikuwa mpinzani nambari moja wa udini. Aliamini udini unaweza kuangamiza taifa na ushahidi uko wazi. Leo hii sheria za nchi zinazuia viongozi kuchaguliwa na kuongoza kuzingatia matakwa ya dini zao.

Na sijui alikuwa mdini kwa dini ipi. Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kwenda Libya kwa Gaddafi na akaulizwa apewe msaada gani kwa wanakijiji wenzake Butiama, akitambua kuwa hapakuwa na msikiti bora na mzuri, aliomba fedha za ujenzi wa msikiti na ulijengwa na sasa ndiyo msikiti bora zaidi mkoani Mara.

Kama angekuwa mdini, na hasa kama anapendelea dini yake angeomba fedha za upanuzi wa kanisa au hata ujenzi wa shule kijijini, lakini alijua kijiji si cha Wakristo pekee; bali hata pia Waislamu. Na hata katika elimu, leo kuna maprofesa wamesoma wakati wa Mwalimu Nyerere, tena wakiwa dini tofauti na Mwalimu. Haya ni maneno ya kumchafua, ambayo hata hivyo, wananchi wanaujua ukweli.

Raia Mwema: Nilikuuliza utendaji wako kama mbunge una vikwazo gani jimboni na hata mkoani kwa ujumla na una shauri nini?

Nyerere: Kuna mambo hayapaswi kuendelea na kwa kweli ni lazima tuhakikishe tunatenga shughuli za kiserikali na shughuli za chama. Tuondoe utaratibu wa Mkuu wa Mkoa kuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa au Mkuu wa Wilaya kuwa Mjumbe wa Kamati ya siasa ya CCM. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka ya kiserikali. Chama kifanye shughuli zake na serikali ifanye shughuli zake.

Raia Mwema: Binafsi ndoto yako ni ipi katika mustakabali wa Tanzania?

Nyerere: Kwa kweli ndoto yangu ni siku moja kuona Tanzania yenye uongozi bora zaidi. Naitamani Tanzania ya namna hiyo, yenye uongozi unaoaminika na wananchi wote, usio na mianya ya ufisadi, nchi isiyo na ukatili kati ya raia kwa raia kama mauaji ya albino.

Raia Mwema: Kwa maelezo yako, huridhiki na mwenendo wa uongozi uliopo. Nini tatizo?

Nyerere: Kuna matatizo mengi, sehemu ya uongozi imeanza kumeguka na kusaliti juhudi za Mwalimu Nyerere. Wameingia katika harakati za udini, lakini pia masuala ya msingi kama kilimo bado hayana mpango mahsusi wa kuridhisha. Kilimo kimechukuliwa kama tukio na si mchakato wa kuikomboa nchi. Kilimo ni kama tukio kama kuwa na sikukuu ya Krismasi na ikiishi basi.

Leo kuna kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, lakini tangu utekelezaji uanze bado unasikia maeneo mengi ya nchi yanakumbwa na njaa, wabunge wengi wameomba msaada wa chakula kiende kwenye majimbo yao. Sasa tukiendelea kuchukulia kilimo kama tukio na si mchakato, tunaweza kumaliza Kilimo Kwanza tukawa na Kilimo Mbili, Kilimo Tatu hadi 100, lakini nchi itaendelea kukumbwa na njaa.

Lakini pia kuna suala la uvunaji wa raslimali za nchi kama madini. Uvunaji umekuwa wa ovyo, nchi hainufaiki vya kutosha na vurugu zimekuwa zikitokea maeneo ya migodi.

Raia Mwema: Huoni kwamba wawekezaji wa nje wanasaidia uvunaji ambao tumeshindwa kwa kukosa teknolojia na fedha za kutosha, kama wanavyoeleza viongozi watetezi wa wawekezaji?

Nyerere: Naamini kwanza si kweli hatuna fedha za kununua mitambo ya uchimbaji madini kama ambavyo wawekezaji wa kigeni wamefanya. Kama nchi inaweza kununua ndege za kivita kwa mabilioni au kufanya mambo mengine, ingeweza kufanya uamuzi mgumu kununua mitambo ya kuchimba madini, na kama hatuna raslimali watu wenye taaluma husika tungeweza kukodi menejimenti.

Kwa nini hatufanyi hivyo? Ndiyo maana nasema uongozi bado haujafanya kazi yake vizuri. Na kwa ujumla, hakuna nidhamu katika udhibiti wa raslimali za nchi.

Raia Mwema: Wabunge mnaweza kujadili suala la ‘chenji ya rada’, nini msimamo wako?

Nyerere: Katika suala hili, msimamo ni kwamba watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani kwanza. Hatuwezi kuendelea na mijadala kila kukicha wakati wahusika wakiendelea kubaki mtaani, wakiendelea kugombea nafasi za uongozi, wakiendelea kushika nafasi za uongozi katika vyama vyao na kwa ujumla wakiendelea na maisha ya kawaida kama vile hawakufanya uovu wowote dhidi ya nchi na wananchi. Jambo la muhimu hapa ni kuchukua hatua kwanza.

Raia Mwema: Suala la posho limeanza kuwagawa wabunge wa CHADEMA, John Shibuda, mbunge mwenzenu amepinga wazi wazi. Utata huu unauzungumziaje?

Nyerere: Niseme tu kwamba, kabla ya kujiunga na chama chochote kila mtu anakuwa na malezi yake kisiasa. Hata mimi kabla ya hapo nilikuwa na mambo yangu mengine, lakini unapoamua kujiunga na chama fulani maana yake unakubaliana na msimamo ya kisera na kikatiba na unaposhindwa ni bora kutoka.

Sasa, mimi si msemaji wa chama, na kwa kweli si adui wa Shibuda; bali ni mwenzangu, ni kiongozi mwenzangu, na tunaheshimiana sana, lakini pia mimi ni mtiifu kwa misimamo ya kisera na kikatiba katika chama chetu.

Raia Mwema: Mwanzo umesema ulikuwa shabiki wa CCM, unakizungumziaje chama hicho?

Nyerere: Nadhani wanawajibika kujiweka sawa na kwa kweli inashangaza chama kama hicho kinakuwa na kurugenzi ya propaganda. Kwa wananchi wengi, propaganda ni uongo na kwa hiyo chama kama hicho kinapokuwa na kurugenzi ya propaganda; maana yake ni chama chenye idara maalumu ya kusema uongo kwa jamii. Hili nadhani sio jambo zuri.

Raia Mwema: Umepanga kuendelea na siasa katika maisha yako yote?

Nyerere: Suala la kuendelea katika siasa ni wananchi wenyewe wataamua, hao ndiyo wapiga kura. Wakiamua miaka mitano waliyonipa inayosha basi nitawaheshimu. Na kwa kweli hakuna haja ya kupigania huu ni uamuzi wa wananchi, wapo wenzangu wanasema mimi kijana siwezi kuondoka katika siasa wakati huu, mimi nadhani kuondoka katika siasa si suala la uzee au ujana; bali ni uwezo wa kutumikia wananchi.

No comments: