Wednesday, July 20, 2011

Ngeleja, Malima watakiwa kujiuzulu

MBUNGE wa Arusha, Godbless Lema (CHADEMA) jana aliomba Mwongozo wa Spika akitaka Waziri na Naibu Waziri wa Nishati na Madini wawajibike katika sakata la wizara hiyo kuchangisha Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa Bajeti.

Lema aliomba Mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 68(7) kwa kusema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, asingeweza kuwa na ujasiri wa kuchangisha fedha hizo bila mawaziri husika kuwa na taarifa.

Mbunge huyo ambaye alitaja moja kwa moja bungeni kwamba Katibu Mkuu huyo alijihusisha katika vitendo vya rushwa kutokana na fedha hizo, alihoji kama kweli ndiye anapaswa kuwajibika pekee na si pamoja na Waziri mwenye dhamana, William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima.

Spika Anne Makinda hakukubaliana na hoja ya Lema kutokana na kile alichosema kwamba mjadala wa suala hilo umewekwa pembeni kutokana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuliomba Bunge juzi kwamba anakwenda kulifanyia kazi. “Naomba waendelee kufanya inavyostahili kiutawala,” alisema Makinda.

Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), ndiye aliyeibua hilo sakata wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kabla haijaondolewa bungeni juzi.

Shelukindo aliwasilisha barua bungeni iliyoandikwa na Katibu Mkuu Jairo ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo kila moja ichangie Sh milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.

Mbunge huyo wa Kilindi pamoja na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.

Pinda katika hoja yake bungeni alikiri kwamba Jairo kawaudhi na kuwatibua wabunge na akaahidi kuwasilisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete aliyemteua ili achukuliwe hatua.

“Lazima nikiri hata mimi nilishtuka kweli sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi hakuna namna ya kutetea,” alisema Pinda.

Wakati huo huo, baadhi ya wadau wa umeme nchini wamewatupia lawama watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa ndiyo chanzo cha matatizo ya umeme kutokana na kutotekeleza kivitendo, mipango ambayo ingesaidia kuondokana na tatizo hilo.

Watendaji hao pia wameshutumiwa kuwa mabingwa wa kupiga maneno na kufanya ujanjaujanja katika kushughulikia tatizo la umeme.

Pia wameshutumiwa kuwa wanapuuzia mchango wa sekta binafsi wakati ndio watumiaji wakubwa wa umeme.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema kinachokosekana kwa watendaji hao ni akili na ubunifu, badala yake alisema wanatanguliza ujanjaujanja na ni werevu wa kupiga maneno.

“Tatizo letu tunakwepa kuwatumia wataalamu katika masuala haya; badala yake tunawatanguliza wachekeshaji na wapiga porojo … katika hali ya namna hii, kamwe hatuwezi kuondokana na tatizo la umeme,” alisema Dk Semboja. Alisema kwa sasa suala si fedha bali ni akili ya kubuni mikakati ya kuondokana na tatizo hilo kama walivyofanya Kenya na Ethiopia.

“Kama suala ni fedha, Tanesco wanahitaji bajeti ya miaka 20 ijayo, kumaliza tatizo la umeme, lakini sasa tunahitaji ubunifu na akili.” Alitoa mfano kuwa ndani ya Tanesco na Serikali kuna wataalamu ambao wameshirikishwa katika mipango inayohusisha ushiriki wa jumuiya za kanda kama ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) na ile ya Bonde la Mto Nile, lakini utekelezaji wake kwa Tanzania hautiliwi maanani.

“Mimi nimekuwa nashiriki miradi yote hiyo, lakini ushiriki wa Serikali yetu ni mbovu, ndiyo maana nasema tuna watu wenye uwezo, watafutwe tuachane na hawa wachekeshaji na wapiga maneno,” alisema Dk Semboja. Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Felix Mosha, alisema Tanzania itaondokana na tatizo la umeme iwapo wataishirikisha sekta binafsi katika mipango yake.

Mosha alisema asilimia 85 ya watumiaji wakubwa wa umeme wa Tanesco ni wenye viwanda, hivyo alishauri Serikali kuwa inapaswa kuwahusisha katika mipango yote kuanzia ya muda mfupi, kati na mrefu ili nao watoe maoni yao ya namna ya kuondokana na tatizo hili. Alisema matatizo haya yanayoendelea ya mgawo wa umeme ni matokeo ya Serikali kuidharau sekta binafsi hasa kwenye suala la umeme.

“Hata pale jambo linalogusa sekta binafsi, Serikali haitaki majadiliano nasi na badala yake wamekuwa wanajadiliana wenyewe na kuamua mambo yao.” Mosha alisema: “Naamini kukwama kwa bajeti hii sasa itatoa fursa ya kutushirikisha, na sisi tuko tayari, kwani tuna mapendekezo yetu ambayo tutawapatia watu wa Serikali.”

Alisema, kama Serikali itaendelea kuwapuuza, ustawi wa viwanda nchini uko katika hatihati, kwani vingi vinategemea jenereta ambazo zilikuwa maalumu kutatua tatizo la muda mfupi na si ilivyo sasa kutokana na gharama zake kuwa juu kuliko umeme.

Mwenyekiti huyo pia alisema katika hali ya sasa, viwanda vya Tanzania havina ubavu wa kushindana na vya nchi zingine za nchi wanachama wa EAC kutokana na kutokuwa na nishati ya uhakika.

Alionya pia kuwa watu wengi watapoteza ajira, kwani viwanda vingi vinafanya kazi kwa siku mbili kwa wiki jambo ambalo linamwia vigumu mwajiri.

No comments: