MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema inakabiliwa na changamoto ya kutotabirika kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuyumba kwa Shilingi ya Tanzania, hali inayosababisha pia kuyumba kwa bei za mafuta nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Mawasiliano na Uhusiano, kutokana na hali hiyo mabadiliko hayo ya bei na kuyumba kwa Shilingi, Ewura na Serikali hawana uwezo wa kuyazuia.
Ilisema mamlaka hiyo itakuwa inatoa taarifa za mara kwa mara ili kuufahamisha umma juu ya takwimu sahihi kuhusu biashara ya mafuta kwa lengo la kuwapa wadau uelewa sahihi wa yanayojiri katika sekta hiyo.
Ilisema mabadiliko ya kwanza kuhusu marekebisho ya kodi katika mafuta aina ya dizeli na mafuta ya taa yalianza tangu Julai mosi ambapo awali bei ya mafuta ya taa ilikuwa Sh 1,675 na dizeli ilikuwa Sh 2,155.
Alisema baada ya ukokotoaji kutokana na agizo la Bunge la kupunguza baadhi ya tozo za mafuta, bei mpya kwa upande wa mafuta ya dizeli ilipungua kwa asilimia 4.86 ambapo bei elekezi ni Sh 1,939 na bei ya kikomo ni Sh 2,84 kwa lita.
Kwa upande wa mafuta ya taa, iliongezeka kwa asilimia 21.88 ambapo bei elekezi ni Sh 1,940 na kwa bei kikomo ni Sh 2,086 kwa lita.
“Kurekebisha tozo na gharama zingine zinazotozwa kwenye mafuta Ewura imeanza mchakato utakaosababisha kushuka zaidi kwa bei ya mafuta ifikapo Agosti mosi, mwaka huu.”
Taarifa ilisema, Ewura itamaliza mchakato wa kupitia kanuni za kukokotoa bei ya mafuta utakaohitimishwa kwa taftishi itakayofanyika Julai 22, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment