SIKU moja baada ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kutangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mmoja wa watu wake wa karibu, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, amesema hakutegemea kama rafiki yake huyo angejiuzulu ubunge.
Lowassa alizungumza jana mchana mjini Dodoma na kuongeza kuwa alishtushwa zaidi alipoona katika Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) namna wananchi walivyokuwa wakimlilia Rostam.
Alipoulizwa lini atazungumzia kauli zinazotolewa katika vyombo vya habari zikimtaka ajivue gamba, Mbunge huyo wa Monduli mkoani Arusha, alisema atazungumza muda utakapofika.
Rostam na Lowassa wamekuwa marafiki kwa muda mrefu na wote walikuwemo katika Mtandao, kundi maarufu lililoendesha kampeni za kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, Rostam amehusishwa na kashfa mbalimbali nchini zikiwemo za ufisadi, yeye na mawaziri wawili wa zamani, Waziri Mkuu Lowassa na Andrew Chenge.
Watatu hao wamekuwa wakitajwa katika kashfa za Richmond, EPA na rada na majina yao yalitajwa na akina Nape na Chiligati, kuwa wanapaswa kujivua gamba.
Hatua ya Rostam kujiuzulu juzi, sasa inafanya macho na masikio ya wengi kuelekezwa kwa watuhumiwa wenzake hao, Lowassa na Chenge, ambao nao kama Rostam walipewa na CCM muda wa kupima.
Jana, kulikuwa na taarifa kwamba mmoja wa watuhumiwa hao wawili, waliobaki alikuwa akipanga kuchukua hatua kama hiyo ya Rostam, na vikao vilikuwa vikiendelea kupanga jinsi ya kutangaza hatua hiyo. Hata hivyo, gazeti hili lilishindwa kumpata mwenyewe kuthibitisha hilo.
Katika taarifa yake wakati akitangaza kujiuzulu, Rostam aliwatuhumu Nape pamoja na Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Chiligati kuwa wamekuwa wakipindisha dhana nzima ya ‘kujivua gamba'.
Rostam alisema, wawili hao wamekwenda mbali kwa kulitaja jina lake kwa kulihusisha na ufisadi, wakati ukweli wa kimazingira na ushahidi wa wazi umeshathibitisha kuwa ni porojo za kisiasa zinazotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule wa 2015.
Rostam ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu nchini, alikuwa Mbunge wa Igunga mkoani Tabora kwa miaka 18, tangu alipomrithi marehemu Charles Kabeho katika uchaguzi mdogo wa mwaka 1994.
Mbali ya kuutema ubunge, Rostam amejiuzulu wadhifa mwingine mkubwa wa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwakilisha Mkoa wa Tabora tangu mwaka 1997.
Alikuwa mwenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM, akitajwa kuwa mstari wa mbele katika kampeni za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 1995 na 2000, na baadaye katika ‘Mtandao’ kundi linaloaminika kumsaidia Rais Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005.
Alitangaza kujiuzulu nafasi zote ndani ya chama tawala juzi alipozungumza na wazee wa Igunga, akisema si kwa sababu ya kujivua gamba, kwa maana ya kuwataka wote wenye tuhuma za ufisadi kujiondoa CCM, bali kutokana na kuchoshwa na siasa uchwara.
“Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu,” Rostam aliwaeleza wazee wa Igunga.
Katika Sekretarieti ya Kwanza ya CCM baada ya Uchaguzi Mkuu akiwa Mweka Hazina, kabla ya mabadiliko yaliyomtupa nje na kumbakiza na wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu na kujiuzulu Aprili mwaka huu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa chama hicho hakijapata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa mwanasiasa huyo.
Alisema kiutaratibu, mbunge huyo anatakiwa awasilishe kwa njia ya maandishi uamuzi wake huo ndipo chama kinapoanza kushughulikia uamuzi wa aina hiyo.
“Sisi bado hatujapata taarifa yoyote rasmi kutoka kwa Mheshimiwa Rostam. Taarifa zake za kujiuzulu kweli tuzimesikia kwenye vyombo vya habari, kwa hiyo siwezi kutoa maelezo yoyote ya hatua ambazo chama kitachukua kufuatia uamuzi huo,” alisema Mukama.
Hata hivyo akiongea na mwandishi wa gazeti hili mjini Nzega, Rostam alisema, baada ya kutangaza mbele ya wazee waliomshawishi kwa miaka 18 iliyopita kuwa mwakilishi wao kujiuzulu nyadhifa zake kinachofuata sasa ni kufuata utaratibu.
“ Kuna utaratibu, ninapashwa kukiandikia chama changu barua na wao ndiyo watakaopeleka bungeni na Bunge nao kuwaandikia Tume ya Uchaguzi” alisema Rostam na kuongeza kwamba ni mchakato ingawa hakusema lini barua hiyo ataiwasilisha.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kwa sasa hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa ni mapema mno.
“Sina maoni. Kwa sasa ni mapema mno nitakapokuwa tayari kuzungumza nitawataarifu,” alisema Nape.
Alisema, anachofahamu ni kwamba ameshazungumza sana, kutuhumiwa sana na kuzushiwa mambo mengi hivyo kwa sasa ni bora anyamaze na kuwapa nafasi watu wengine nao wazungumze.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kupeleka taarifa za kujiuzulu kwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili Chadema kijiandae kwenda kuchukua jimbo hilo.
Zitto alisema hayo jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika na kuhoji kama Spika ana taarifa ya kujiuzulu kwa Mbunge huyo, ili aipeleke haraka NEC.
Akijibu hoja hiyo, Spika Makinda alisema, hana taarifa rasmi kwa kuwa hakupelekewa barua ila amesoma katika mitandao kama watu wengine.
Makinda alisema taarifa rasmi ikimfikia, utaratibu utafuatwa kushughulikia jimbo lililo wazi.
No comments:
Post a Comment