WANASIASA wakiwemo viongozi wastaafu pamoja na wazee, jana waliungana na Watanzania wengine kuelezea kukerwa na tabia ya baadhi ya wabunge kutokuwa na uadilifu na kukidharua kiti cha Spika wa Bunge.
Wengi wamesema, Bunge sasa ni la vichekesho, la mzaha, vurugu, kupiga zeze, la shuleni na la watu wanaokesha katika baa; baadhi wakiwataka waasisi wa taifa kunusuru hali hiyo huku wengine wakisema hakuna imani kwa Cha Cha Mapinduzi (CCM) wala upinzani.
Baadhi ya wanasiasa hao wameelezea hofu yao ya kubadilika kwa dhamira za wanaogombea ubunge; badala ya uwakilishi, wanafuata ajira na kuonya hali ikiendelea hivyo, hata wagombea urais wajao, watafuata maslahi binafsi Ikulu.
Aliyekuwa Mbunge wa Kwela mkoani Rukwa, Dk. Chrisant Mzindakaya alisema Bunge la sasa limekuwa linaendeshwa kama ‘kupiga zeze’ na wabunge wanajua Kanuni moja tu ya 68 ya kuomba Mwongozo wa Spika.
Aliwaasa wabunge wa CCM kutotumbukia katika malumbano hayo na badala yake wajibu hoja za upinzani kistaarabu.
Akilichambua Bunge hilo la 10, Mzindakaya aliyekaa bungeni kwa zaidi ya miaka 35, alisema ni tofauti na Bunge lililohusisha wapinzani kati ya mwaka 1995 na 2005 ambapo kulikuwa na umoja wa kitaifa, uadilifu na kuheshimu Kanuni, lakini hili la sasa limekuwa linaendeshwa kama ‘kupiga zeze’.
“Kutoa mawazo ni jambo zuri ingawa si lazima kukubaliana… wabunge sasa hawana utaifa wameweka mbele itikadi za kisiasa, hii si nzuri.
“Mfano katika Bunge la zamani tuliwahi kwenda Uingereza na tukaulizwa jinsi tutakavyotatua tofauti za kisiasa Zanzibar wakati huo mwafaka haukuwepo, lakini Mbunge wa CUF (hakumtaja jina) alijibu kizalendo kwamba lengo la vyama vyote ni kuijenga Zanzibar.
“Ukiangalia televisheni leo unaona Bunge limekuwa la vichekesho, lina wasomi wengi na vijana wasio na uadilifu, hawaheshimu Kanuni wala kiti cha Spika na kila anayesimama anajua Kanuni ya 68 tu; ya kuomba Mwongozo wa Spika,” alisema Dk. Mzindakaya na kuongeza:
“Haitakiwi kanuni kumuachia Spika peke yake, wote wanapaswa wazisome… wabunge wabadilike wajue ukishakuwa kiongozi unaacha kwenda baa kukaa kwenye kiti kirefu na mambo yasiyo na maadili na raha unaachana nazo.”
Alisema Mbunge mwadilifu hawezi kula rushwa, lakini wabunge wa sasa wameanza kupoteza uadilifu na sababu kuu ni kubadilika kwa malengo ya kuingia bungeni ambapo wapo wanaotaka uwaziri na wanakuwa wabunge bila wito, bali ajira.
Alieleza hofu yake katika miaka ijayo pia watakaogombea urais watakuwa wanatafuta ajira na maslahi yao na si wito wa kuwatumikia wananchi. Aliwataka wabunge wa CCM waisaidie Serikali yao kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kujibu hoja.
“Upinzani wanafanya makusudi kuharibu system (mfumo)…nao CCM wasipoangalia miaka mitano itaisha kwa malumbano ya kisiasa na hawatarudi bungeni maana hawatakuwa na kitu walichofanya cha kuwasaidia wananchi,” alieleza mwanasiasa huyo mkongwe.
Pia alizungumzia tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaojisifu kuwa na urafiki na Rais Jakaya Kikwete, alisema; “Rais akikupa uongozi, urafiki unakufa, unatakiwa ufanye kazi zaidi tena kwa uadilifu ili usimfedheheshe na ukimsikia mtu anajisifu Rais rafiki yake ujue hana akili.”
Chama Cha Kijamii (CCK), pamoja na kutokuwa na mwakilishi bungeni, jana kililaani tabia hizo za baadhi ya wabunge kuwa zinalifanya Bunge liwe eneo la mzaha na vurugu.
Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muhabi aliwataka waasisi wa Taifa waliobaki au viongozi wengine wenye utashi na ushawishi wa kubadili mwenendo huo potofu wa Bunge la sasa kutumia busara zao kulinusuru.
Muhabi alisema hali hiyo ikiachwa, inaashiria hatari ya kulifanya Bunge lipoteze umuhimu wake kwa kuwa kinachoendelea ndani ya mhimili huo muhimu ni matokeo ya kuwepo na viongozi wabinafsi na wenye kujali maslahi yao.
“Wabunge hawaheshimu kanuni …wala kufanya kazi waliyotumwa na waliowachagua, wenye kulala haya, wenye kuonyesha hasira zao… wanajiropokea na wenye kuonyesha umahiri wa kuvunja kanuni na kutomheshimu Spika nao wanajipa nafasi bila aibu.
“Endapo viongozi wengine waliobahatika kuasisi Taifa hili na Hayati Mwalimu Julius Nyerere au waliobahatika kuzishika busara na kuiga maadili yake wataendelea kujifungia kwenye mageti nyumbani mwao… hali itakuwa ya hatari,” alisema Muhabi.
Alisifu uongozi wa Bunge hilo kwa kuwachukulia hatua wanaovunja kanuni kwa kuwatoa nje ya ukumbi na kupendekeza kuandaliwe utaratibu maalumu wa viongozi wenye busara akiwemo Rais Kikwete kuwahutubia wabunge kuhusu maadili na nidhamu binafsi mara kwa mara. *Mbatia alia ni Bunge la kishule-shule
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia alisema malumbano hayo yanatokana na mfumo wa elimu uliopo na kukosekana kwa Chuo cha Uongozi uliosababisha bunge liwe la kishule.
Mbatia alisema kutokuwepo kwa chuo hicho kumesababisha wabunge wengi wachaguliwe bila kujua maana ya uongozi na hivyo kujikuta wanafanya mambo yasiyo ya kawaida na kutumia vipaza sauti kwa jazba bila mpangilio.
“Zamani watu wote wanaoongoza walipita Kivukoni na kujifunza maadili ya uongozi lakini leo hii vijana wanatoka shuleni moja kwa moja wanaingia bungeni na kufanya mambo yao ya kishule- shule.
“Tuachane na siasa nyepesi, maana tukitaka kuonyeshana mbabe kuliko mwingine, tutaliangamiza Taifa na tutaharibu kizazi chetu, tunatakiwa sote tukae kwenye meza moja ya mazungumzo na tuangalie matatizo yanayoikabili nchi kwa sasa,” alisema Mbatia.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Idd Simba alisema Bunge sasa halina maadili wala uzalendo, bali mvurugano.
Samba alisema anachokiona ni kundi la watu wachache waliodhamiria kugawa na kumaliza nguvu ya CCM kwa uchu wa kutaka kuingia Ikulu kwa lazima na kuonya wazee wa chama hicho wamejipanga nchi nzima kupambana nalo.
Simba akizungumza jana, Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na baadhi ya magazeti, alidai hali ni mbaya na tete, haivumiliki kwa kuwa inahatarisha amani iliyodumu kwa zaidi ya miaka hamsini.
“Hali ya siasa ni mbaya, watu wachache wanafanya mambo kwa maslahi yao huku wakidai wanamuenzi Mwalimu Nyerere, Mwalimu hakuwa hivyo.
“Angalia Bunge vyama vinagombana si kutoa huduma kama elimu, maji na afya, bali vyeo, wananchi hawana imani na chama tawala, wala upinzani wala mfumo wenyewe wa vyama vingi,” alisema Simba. Simba aliyewahi kuwa Mbunge wa Ilala na Waziri wa Viwanda na Biashara, alisema wazee wanajipanga kuwashikisha adabu wanasiasa wasio na nidhamu na kuhakikisha kuwa, CCM inarejesha imani, heshima na kuondoa udhaifu uliopo katika chama na siasa za nchi.
No comments:
Post a Comment