Monday, August 3, 2009

TAARIFA YA IKULU KUHUSU SUALA LA KAMPUNI YA RICHMOND

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na maneno na vijembe ati kuwa kuna mkono wa Rais Jakaya Kikwete katika kutoa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura iliyopata Kampuni ya Richmond.
Kiini cha maneno hayo ni kauli za baadhi ya wanasiasa zilizopazwa sauti na baadhi ya vyombo vya habari.

Tunapenda kusema, tena kwa msisitizo, kuwa maneno hayo si ya kweli na hayana msingi wowote.
Rais hajahusika na uamuzi wa tenda hiyo kupewa kampuni ya Richmond kama vile ambavyo hakuhusika na kupewa tenda kwa kampuni za Aggreko na Alstom.

Kama mtakavyokumbuka wakati ule kampuni hizo tatu ndizo zilizopewa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura. Kampuni ya Aggreko ilipewa tenda ya kuzalisha umeme wa megawati 40 na Richmond kuzalisha megawati 105.6 pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Kampuni ya Alstom ilipewa tenda ya kuzalisha megawati 40 za umeme pale Mwanza kwa kutumia mafuta ya dizeli.

Katika uamuzi wa kupewa tenda kampuni hizo, Rais hakujihusisha, hakuhusishwa na wala hapakuwepo na sababu ya kuhusishwa au kujihusisha . Hiyo siyo kazi ya Rais. Hiyo ilikuwa ni kazi ya TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini na ndiyo walioifanya. Hayo ndiyo matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma na ndivyo ilivyofanyika.

Katika shughuli nzima ya uteuzi kulikuwa na Kamati mbili za kushughulikia upatikanaji wa makampuni ya kutoa huduma ya mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme wa dharura. Ya kwanza ilikuwa Kamati ya Watalaamu kutoka TANESCO, Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini iliyokuwa na jukumu la kutathmini wazabuni wote waliojitokeza kuomba na kupendekeza wanaofaa kufikiriwa kupewa kazi hiyo.
Kamati ya Pili ilikuwa ni ile ya Serikali ya Majadiliano (Government Negotiating Team) iliyokuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO, Benki Kuu na Shirikisho la wenye Viwanda kuwakilisha sekta binafsi. Kamati hii ilikuwa na jukumu la kufanya majadiliano na wale waliopendekezwa na Timu ya Wataalamu na hatimaye kupendekeza anayefaa kupewa.

Kamati ya Majadiliano ilipomaliza kazi yake ilikabidhi taarifa yake Wizarani kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Arthur Mwakapugi ambaye naye akaikabidhi kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Ibrahim Msabaha kwa uamuzi. Kama tulivyokwishasema mamlaka ya uamuzi yalikuwa chini yao. Hakuna wakati wowote katika mchakato wa kuamua kampuni ipi ipewe tenda alipofikishiwa Rais kwa uamuzi wake wala kutakiwa kutoa maoni.

Mambo aliyofanya Rais

Katika suala zima la kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme, Rais alihusika katika mambo manne. Kwanza, katika kuamua TANESCO itumie mitambo ya kukodi kuzalisha umeme na Serikali igharamie ukodishaji huo.

Suala hilo lilikuwa lazima liamuliwe na yeye kwa sababu lilikuwa linahitaji Serikali kugharamia ukodishaji. Kama si hivyo lisingefikishwa kwake kwani ni jambo ambalo lingekuwa juu ya TANESCO kuamua kukodisha na kulipia. Gharama hizo hazikuwa zimepangwa katika bajeti ya serikali hivyo ilikuwa ni lazima kupata idhini ya Rais ya kutafuta hizo pesa na kuzitumia kwa ajili hiyo.

Pili, Rais alihusika katika kuzungumza na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuwaomba wakubali sehemu ya pesa waliyopanga kuipa Tanzania kama msaada kutokana na mpango wa msamaha wa madeni itumike kugharamia ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme. Walikubali, na USD 225 milioni zilitumika kukodisha mitambo ya Kampuni za Aggreko, Alstom na Richmond (ambayo baadae ikawa Dowans) na matumizi mengine ya dharura za umeme. Matumizi hayo mengine yalijumuisha pia ununuzi wa mitambo ya aina ya Watsilla ya kuzalisha megawati 100 za umeme pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Mitambo hiyo imeshanunuliwa, kufungwa na tayari inazalisha umeme.

Tatu, Rais alihusika katika vikao vya Baraza la Mawaziri vilivyojadili matatizo ya upungufu mkubwa wa umeme nchini na kuamua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo. Moja ya hatua zilizoamuliwa kuchukuliwa, ni hii ya kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Katika vikao hivyo vya Baraza la Mawaziri alitoa maelekezo ya mambo ya kuzingatiwa katika zoezi zima la kupata makampuni au watu watakaotoa huduma hiyo. Hususan, Rais alisisitiza kuwa pamoja na udharura uliokuwepo Kanuni na Sheria ya Ununuzi wa Umma zizingatiwe.

Nne, Rais alikataa Kampuni ya Richmond isipewe malipo ya awali (down payment) ya USD 10 milioni na kutaka ukweli kuhusu uaminifu na ukamilifu (integrity) wa kampuni hiyo ujulikane. Rais alikataa maombi yaliyopelekwa kwake na Wizara ya Nishati na Madini ya kumuomba aagize Wizara ya Fedha, iilipe kampuni hiyo fedha hizo. Rais aliagiza Wizara ya Fedha ibaki na msimamo wake na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wafanye mambo mawili. Kwanza, wafanye utafiti zaidi kujua undani wa Kampuni ya Richmond. Isije kuwa ni kampuni bandia wakapewa fedha wakatokomea nazo na mitambo isipatikane na hukuna namna ya kuipata kampuni wala wahusika wake. Pili aliagiza wawatake viongozi wa Kampuni ya Richmond kwanza walete mitambo, ikishafika, ndipo walipwe. Maagizo hayo ya Rais yalizingatiwa na Kampuni ya Richmond ikapewa sharti hilo. Lakini, ikashindwa kulitekeleza na kuishia kuingia mkataba na Kampuni ya Dowans iliyokuja kuleta hiyo mitambo badala yake.

Hivyo ndivyo alivyohusika Rais katika suala zima la ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwa makampuni ya Aggreko, Alstom na Richmond. Kama kweli kungekuwa na mkono wake wa upendeleo kwa Kampuni ya Richmond kupata tenda, iweje tena yeye ndiye akatae kampuni hiyo isilipwe fedha za kianzio mpaka kuifanya ishindwe kazi? Ndiyo maana tunasema maneno hayo hayana msingi, yanasemwa na watu ambao ama hawaujui ukweli au wameamua kutokusema kweli kwa makusudi kwa sababu
wanazozijua wao. Tunatoa ufafanuzi huu kuwafanya Watanzania waelewe ukweli wa mambo.

Watumishi wa Umma

Kuhusu watumishi wa Umma waliohusika na uchambuzi wa zabuni, majadiliano na uamuzi, napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali imelishughulikia jambo hili na sasa linafikia ukingoni.

Mamlaka za nidhamu zimeangalia mambo mawili: tuhuma za rushwa na uzembe. Tuhuma za rushwa hazijathibitika mpaka sasa na tuko tayari kuchunguza zaidi. Lakini tuhuma ya uzembe imethibitika kwa ukweli kwamba Kampuni ya Richmond haikufanyiwa uchunguzi wa kina kuijua kampuni hiyo kwa undani kabla ya kuipa tenda. Due diligence haikufanywa. Kwa sababu ya makosa hayo mamlaka za nidhamu husika kwa watumishi hao zitawachukulia hatua zipasazo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi.

Wenzetu hawa waliridhika tu na maelezo ya mwakilishi wa Kampuni ya Richmond aliyetosheleza masuala ya kuwa na mitambo ya kuweza kuzalisha megawati 105.6, mitambo ambayo itafaa kwa mfumo wetu wa umeme, itapatikana kwa wakati na umeme kuuzwa kwa bei nafuu. Ni kweli kwamba kampuni hiyo iliwashinda wazabuni wote kuhusu masharti hayo lakini walisahau msemo wa wahenga kuwa “si kila king’aacho ni dhahabu.” Naamini wangefanya uchunguzi wa kina kuhusu kampuni ya Richmond wangegundua kuwa ni ya bandia na haikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza zabuni ile. Kwa sababu ya upungufu huo hatua zipasazo za kinidhamu zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa kiwango chake cha kuhusika.Yaani kwa uzito wa kosa lake. Kazi hiyo imeanza na inaendelea kufanyika.

Imetolewa 01 Agosti, 2009

PHILLEMON LUHANJO
IKULU,
KATIBU MKUU KIONGOZI
DAR ES SALAAM.

No comments: