Thursday, August 20, 2009

Kikwete amtega Spika Sitta

-Amweka kwenye kipindi cha majaribio
-Mengi naye aguswa ndani ya NEC
-Ya Mkapa yawatisha wajumbe

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amemtega Spika Samuel Sitta ambaye ana muda hadi Novemba mwaka huu kujirekebisha, Raia Mwema imeambiwa.

Mtego huo ambao kwa upande mmoja unapalilia zaidi mpasuko wa ndani baina ya kundi la Sitta na jingine ambalo yeye amekuwa akidai linamtafuta, ulihitimishwa juzi pale Sitta alipotakiwa kujitetea ili asinyang’anywe kadi ya uanachama hatua ambayo dhahiri ingeshusha kila aina ya ndoto aliyonayo.

Baadhi ya wana CCM waliozungumza na Raia Mwema wakirejea Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ulioanza mwishoni mwa wiki iliyopita wanasema mbali na kumpatiliza Sitta, Kikwete pia aliruhusu kutikiswa kwa mtu wa karibu na Sitta, mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi, ambaye kama Sitta, amekuwa akisema kwamba yumo katika vita dhidi ya ufisadi ili kumsaidia Rais Kikwete anayeiongoza.

Habari za ndani ya CCM kutoka katika vikao rasmi na visivyo rasmi, zinaeleza kwamba Rais Kikwete ameamua, kutumia mtindo wa “kuuma na kupuliza” kwa marafiki zake, Sitta na Mengi kwa kuruhusu mjadala kwenda katika mpangilio ulioandaliwa mahususi kwa ajili ya ‘kuwashughulikia’ Sitta na Mengi, na kwa maana hiyo kundi la wabunge ambalo limekuwa likijitambulisha na Sitta.

Taarifa za ndani zinasema, katika kikao hicho, mbali ya Sitta kujadiliwa, mmoja wa wabunge alibanwa kwa kumshirikisha Mengi katika shughuli za CCM ikidaiwa kwamba mfanyabisahara huyo si mwana CCM.

Hata hivyo, habari zinasema kwamba pamoja na Mengi kuwa mwana CCM na mtu anayekisaidia chama hicho kwa muda mrefu, mfanyabiashara huyo amekuwa karibu na Rais Kikwete na amekuwa akimtaja na kumsifia Rais hadharani.

“Karibu wajumbe 40 walizungumza dhidi ya Sitta. Walikuwa wakitoa wito afukuzwe kwa jinsi anavyoliendesha Bunge ambalo katika siku za karibuni limekuwa likiibana sana Serikali.

“Aliomba sana msamaha, lakini dhahiri hakuna hata mmoja aliyekuwa akimsikiliza, hata wachache waliojaribu kumuunga mkono walizomewa wasiweze kuendelea kusema lolote.

“Kwa hiyo kwa sasa ni kama Sitta yupo katika kipindi cha majaribio. Hatima yake itategemeana na jinsi anavyoliendesha Bunge kati ya sasa na Novemba. Hiyo kamati iliyoundwa imepewa mwanya wa kuitisha kikao cha dharura kama itaona kuwa anakwenda ndivyo sivyo,” anasema mmoja wa wajumbe wa NEC aliyezungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kuwa hatajwi kama chanzo cha habari hii.

Mjumbe mwingine aliiambia Raia Mwema kwamba pengine msumari wa mwisho katika jeneza la Sitta utakuwa umepigiliwa na mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alimsema Sitta kwamba japo amekuwa akidai kwamba anaendesha Bunge kwa mtindo wa Uingereza (Jumuiya ya Madola), uendeshaji wake haukuwa sawa na huo wa Uingereza.

“Kwanza Ngombale alichanachana Waraka wa Wakatoliki akidai ni ilani ya kisiasa na kwamba haiwezekani nchi ikawa na ilani zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kisha akamrukia Sitta.

Yalizungumzwa mengi, pamoja na kumtetea Mkapa (Benjamin) na wapo walioonya kwamba kwa kuruhusu Mkapa kukwaruzwa, Kikwete alikuwa anaandaa kaburi lake mwenyewe,” anasema mjumbe huyo.

Lakini mjumbe mwingine, mfuasi wa kundi moja kati ya makubwa yanayopingana kwa sasa ndani ya CCM ameiambia Raia Mwema hata hivyo kwamba msimamo wa Kikwete katika suala la Sitta unaweza usiwe na maslahi makubwa kwa chama siku za usoni.

“Kikwete anaonekana hataki kuwaudhi marafiki zake wote wakiwamo hata wale ambao alionekana kuwatosa kutokana na kuhusishwa kwao na kashfa mbalimbali ambazo Sitta na kundi lake wamekuwa wakizisemea. Nadhani alipaswa kuwa na msimamo wa wazi katika hili maana linahusu mustakabali wake kisiasa na wa chama chetu.

“Sasa wananchi wana uelewa kuliko wakati mwingine wowote na kwamba mwaka mmoja si mbali kuelekea kwenye uchaguzi mwingine na hii ni hatari sana kama hakutatokea jambo lolote zito,” alisema mwanasiasa huyo katika mazungumzo ya simu kutoka Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao hivyo.

Soma zaidi

No comments: