Wednesday, August 5, 2009

Madini kwa Mzungu, mashimo kwa Mtanzania!

HATA kama isingekuwa udadisi wa vyombo vya habari, hatimaye ingejulikana tu jinsi tunavyoporwa utajiri wa madini yetu kupitia mikataba mibovu yenye kufukarisha nchi.

Ingawa Serikali imejitahidi mara nyingi kuficha, na hata kupotosha kwa makusudi, ukweli juu ya jambo hili, hila hizi zimegonga mwamba kwa sababu Mtanzania wa leo sio yule wa mwaka 1947.

Katika hali ya kufadhaika juu ya siri za ufisadi huu kuendelea kufichuliwa na vyombo vya habari, serikali ilikurupuka kuandaa muswada wa habari ambao, kama ungewasilishwa bungeni na kupita, ingekuwa ni kosa la jinai kwa mwanahabari kuandika juu ya mikataba ya kibiashara ya serikali na ufisadi ambapo adhabu yake ingekuwa ni kifungo cha muda mrefu.

Madhumuni ya muswada huo ilikuwa ni kuwalinda kwa kuwakingia kifua, wahujumu wa uchumi wa taifa letu ili waweze kuvuna na kutumbua bila ya hofu kile wasichopanda.

Lakini, wakati uporaji huu wa madini ukiendelea na serikali kuvisakama vyombo vya habari eti kwa "kununua hoja [kelele] ya Wapinzani" bungeni juu ya jambo hili, uongozi wa juu wa serikali ulijaribu kujikosha kila mara, lakini bila kuchukua hatua stahili.

Wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye, pengine kwa kuona joto la uelewa wa wananchi juu ya hujuma inayofanywa, aliona bora awe upande wa [wanaolalamika] walio wengi, pale mwezi Agosti 2006, alipotamka kwa kukiri ukweli kwamba, "nchi yetu hainufaiki na mikataba ya uwekezaji wa kigeni katika sekta ya madini kutokana na kwamba, kile kidogo tunachopata ni sawa na kodi ya pango la ardhi pekee, huku wawekezaji wakikomba thamani na faida yote ya madini". Chini ya Mikataba ya sasa, wawekezaji hao wanalipa mrahaba wa asilimia tatu tu ya faida halisi.

Baada ya kuona bosi wake amevunja ukimya kwa kutoboa ukweli, Waziri Mkuu wa wakati huo, Mheshimiwa Edward Lowassa, ambaye ndiye huyo huyo aliyekuwa akizima hoja za wabunge juu ya uporaji huo bungeni, aliona aibu kuachwa nyuma, naye akakusanya ujasiri bila kupenda, akatamka kwa kutahadharisha kuwa, "kama hali hii [ya mikataba mibovu] itaruhusiwa kuendelea, katika miaka michache ijayo, Tanzania itaachiwa mashimo ardhini na mazingira yaliyoharibika kutokana na uvunaji madini usiojali".

Lakini pengine kwa hofu ya kuwaudhi waporaji hao na kwa kuwakingia kifua akasema kuwa Serikali haikuwa na mpango wa kukatisha mikataba na wawekezaji hao, kwa sababu kufanya hivyo kungeigharimu serikali kiasi kikubwa cha fidia kwa kuvunja mikataba hiyo.

Alichokuwa akiuambia Lowassa umma wa Kitanzania ni kwamba, Watanzania wavumilie kuendelea kunyonywa hadi tone la mwisho la damu kwa sababu tu viongozi wao walikwishaingia mikataba ya kipumbavu na wawekezaji matapeli.

Wakati Rais Kikwete na Waziri Mkuu Lowassa wakitahadharisha juu ya athari ya mikataba mibovu kwa jamii ya Kitanzania, mkataba mwingine, mbovu zaidi wa mgodi wa Buzwagi ulikuwa mbioni kutiwa sahihi mjini London kwa masharti yale yale ya kiporaji.

Hapo, Watanzania walianza kujiuliza: Je, kukiri udhaifu wa mikataba ya madini kwa viongozi wetu kulikuwa na dhamira njema au ilikuwa ni kulia machozi ya mamba?. Na kama ilikuwa ni dhamira njema, kwa nini Mheshimiwa Lowassa alikaa hoteli moja na Waziri Nizar Karamagi mjini London, ambamo Mkataba wa Buzwagi ulitiwa sahihi, bila yeye kumkemea?

Vitendo na kauli za viongozi wetu vinatuaminisha kwamba, kumbe enzi za karne ya 19 za mikataba ya kilaghai ya kina Karl Peters, Cecil Rhodes, Sir George Goldie na watemi wa kale – kina Mangungo wa Msovelo [Tanzania], Lobengula wa kabila la Ndebele [Zimbabwe], Premph [Kwaku Dua] [Afrika Magharibi] na wengine, zingali nasi karne ya 21!

Tunaweza kuwasamehe wafalme hao wa kale, kwa kudanganywa wakauza nchi zao kwa "zawadi" [takrima] ndogo ndogo za shanga, vioo vya kujiangalia, tumbaku, shanga na pombe, kwa sababu ya ujinga wao [kukosa shule]; lakini si hawa viongozi wetu wa leo ambao wameungana na ubepari wa kimataifa kuangamiza nchi na watu wake. Kauli zao za kujifanya kutambua matatizo ya nchi lakini wasichukue hatua kuyakomesha, ni za kisaliti na kihaini.

Wanatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, kutupumbaza na kuuwa ujasiri wetu wa kimapinduzi kwa madai ya "kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji", wakati ukweli wanasafisha njia ya wakoloni na ukoloni kujirudia katika mazingira yetu.

Kilichowaleta wakoloni kwetu karne ya 19, ni hicho hicho kinachowaleta katika karne yetu, tena kwa kulakiwa na kutengenezewa mapito na watawala wetu, kama ilivyokuwa hapo mwanzo, wapate kuingia. Lakini ujinga wa kina Mangungo unazidiana kama tutakavyoeleza baadaye katika makala haya, Watanzania wakiongoza.

Ulaghai wa wawekezaji wa nchi za Magharibi unaweza kudhibitiwa tu na viongozi wenye maono, wasio na uchu wa utajiri na wenye kukerwa na shida na umasikini wa watu wao. Kiongozi mwenye maono hawezi kushindwa kuelewa kwamba sekta ya madini, kwa sasa, ndiyo yenye kuvutia kwa wawekezaji wa kigeni barani Afrika kuliko sekta zingine; na ndiyo ambayo, siyo tu itakayotuachia mashimo ardhini na mazingira yaliyoharibika, kama alivyobaini Mheshimiwa Lowassa miaka mitatu iliyopita [lakini bila kuchukua hatua tu], bali pia ndiyo itakayorejesha ukoloni mkongwe ili tuendelee kuporwa rasilimali zingine.

Kuthibitisha hilo tuangalie viashiria.

Afrika inakadiriwa kumiliki karibu asilimia 48 ya akiba ya madini yote duniani. Kimsingi, Afrika bado ni mzalishaji mkubwa wa mali ghafi [yakiwamo madini] kwa ajili ya viwanda vya nchi zilizoendelea.

Kwa mfano, kati ya mwaka 1970 – 1975, utafiti na uchimbaji wa mafuta barani Afrika ulichukua asilimia 54.5 ya sekta zote ambapo sekta ya madini ilichukua asilimia 20.3, na viwanda asilimia 9.6 tu. Lakini kati ya 1990 – 2002, uwekezaji katika madini ulipaa kufikia asilimia 54 wakati sekta ya mafuta iliporomoka hadi asilimia 26, na ile ya viwanda kushuka hadi asilimia 5.2 ya sekta zingine.

Kwa Tanzania, tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa, kati ya Kilometa 945,087 za mraba za nchi hii, Kilometa 886,037 za mraba zina utajiri wa madini mbalimbali, na eneo la Kilometa 59,050 lililosalia ni maji, lenye utajiri mwingine wa rasilimali.

Kwa hiyo, kama uvunaji wa madini na rasilimali zingine utaruhusiwa kwa kasi ya sasa, kwa kuwekwa mikononi mwa wawekezaji wa kigeni kwa kile kinachoitwa "kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji", muda si mrefu Tanzania itakuwa koloni la Wazungu kupitia makampuni ya kimataifa ya kuhodhi, yanayowakilisha matakwa ya nchi za Magharibi.

Licha ya utajiri mkubwa wa madini, Afrika bado ni moja ya mabara masikini sana duniani. Kwa mfano, hadi miaka ya karibuni, Angola, Botswana, Jamhuri ya Afrika ya Kati [CAR], Ghana, Liberia, Namibia, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tanzania na DRC, zilizalisha karibu asilimia 70 ya almasi yote duniani, lakini bado ni kati ya nchi masikini, zenye kutembeza "bakuli la omba omba".

Kwa madini ya dhahabu, shaba na vito vingine, Afrika inashikilia asilimia 51 ya soko la dunia, lakini haijaweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kwa nini?

Tofauti na mikataba ya kilaghai ya karne ya 19, mikataba ya sasa ya madini inahusisha ndoa kati ya siasa [wanasiasa] na rushwa kubwa za kimataifa ili kuwapora wananchi haki zao.

Ni kwa sababu hii sasa tunaambiwa na viongozi wetu kwamba mikataba hiyo ni siri ya serikali wakati ni haki ya kila mwananchi kuijua. Kwa nini mikataba mingine ya kimataifa inatangazwa kwa mbwembwe na tafrija ila ya madini tu? Tofauti yake ni nini?

Vivyo hivyo, taarifa za mapato ya sekta hiyo, zenye kukinzana, zinaashiria ufisadi au kuficha ukweli. Kwa mfano, tunaambiwa, kati ya 1992 na 2000, uvunaji wa dhahabu nchini uliongezeka kwa asilimia 266.7; yaani kutoka kilo 409 hadi 15,000 ambapo uzalishaji wa almasi uliongezeka kutoka karati 67,300 hadi 354,500.

Lakini, licha ya ongezeko hilo, chini ya wawekezaji wa kigeni, sekta ya madini ilichangia asilimia 2.5 tu ya pato ghafi la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 15 waliyochangia wachimbaji wadogo wadogo kabla ya kuenguliwa na Wazungu. Hii inaonyesha dhahiri kwamba kuna hujuma inayolindwa.

Serikali nayo, ama haina uhakika na kinachozalishwa au inaficha ukweli kwa hila. Kwa mfano, wakati Wizara ya Mipango ilisema kuwa mauzo ya madini yaliingiza dola milioni 396.1 mwaka 2002, Wizara ya Madini ilidai mauzo yalifikia dola milioni 432.3. Na wakati Wizara ya Mipango ilisema mauzo yalifikia dola milioni 491.1 mwaka 2003, Wizara ya Madini na Nishati ilidai yalikuwa dola milioni 560.2.

Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji dhahabu baada ya Afrika Kusini na Ghana, lakini inasaga meno kwa umasikini, licha ya utajiri mkubwa huo.

Kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya hujuma inayofanywa kwenye sekta ya madini, hatimaye Novemba 22, 2007, Serikali iliunda Tume ya Jaji [Mark] Bomani kuchunguza mikataba hiyo. Matokeo yake ni kuwa, "Ukishangaa la Mussa, la Firauni je?" Hapa ndipo "umangungo" [ujinga] wa Watanzania unapozidi ujinga wa watu wengine, kama inavyothibitishwa na ukweli ufuatao.

Mwaka 2008 uzalishaji dhahabu ulifikia wakia [ounces] 1,170,000. Kwa bei ya dola za Kimarekani 900 iliyotumika. Thamani ya dhahabu iliyouzwa ilikuwa dola bilioni 1,053 tu.

Na kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hulipa mrahaba [kodi] kidogo, kiwango cha asilimia tatu tu ya faida [net back value] kwa sasa, serikali ilipata [kama kweli imelipwa] dola 15,970,500 tu kutokana na uwekezaji huo!

Na kama serikali ingekubali na kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Bomani ya kuongeza kiwango cha mrahaba kufikia asilimia 50 ya faida ya mwekezaji, kama zifanyavyo nchi zingine za Kiafrika, serikali ingeweza kujipatia dola 52,650,000, sawa na Shs. 68,445,000,000.

Ujinga wetu unajidhihirisha pale tunapokubali kudanganywa na makampuni kwamba, gharama za uzalishaji ni kubwa kiwango cha dola 445 kwa wakia. Ujinga huu umetukosesha mapato ya dola 36,680,000, sawa na Shs. 47,680,000,000 kwa mwaka 2008 pekee; ambazo zingetumika kuleta maendeleo kwa wananchi wetu.

Ujinga wetu unakwenda mbali zaidi: Wakati tumekubali kudanganywa kuwa bei ya dhahabu katika soko la dunia ni dola 900 tu kwa wakia, wanunuzi kutoka India, Pakistani na wengineo wanalipa kati ya dola 1,200 na 1,300 kwa wakia huku tukijifanya kutolijua hilo. Kwa nini? Eti tunaweka "mazingira mazuri kwa wawekezaji".

Ilivyo sasa, nchi yetu hainufaiki hata kidogo na sekta ya madini; wanaonufaika ni hawa Wazungu wanaopora utajiri wetu, na sisi kuachiwa mashimo na mazingira yaliyoharibiwa kama urithi wetu.


Simu:
0713-526972

Barua-pepe:
jmihangwa@yahoo.com

No comments: