Mwenyekitiwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Manento, amesema Mahakama Kuu ya Tanzania imetekeleza wajibu wake katika kutoa hukumu ya aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na wenzake wanane, na kwamba anayesema kinyume cha hukumu hiyo anakiuka Katiba ya nchi.
Aidha, alisema kwa mujibu wa Katiba, haki za binadamu zimezingatiwa, maana mahakama ndicho chombo cha juu cha kutekeleza haki hiyo na hukumu hiyo haiwezi kutenguliwa kwa namna yoyote sasa, mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo na Mahakama ya Rufaa, hatua hiyo ikichukuliwa.
“Mahakama imeshatoa uamuzi, hakuna anayeweza kuongeza hapo wala kupunguza, hakuna mwingine anayeweza kusema tofauti ya hukumu hiyo na ikatekelezeka na kama atatokea, atakuwa anakiuka Katiba,” alisema Jaji Manento ambaye alikuwa akifafanua Kifungu cha 107 (A) (1) cha Katiba.
Jaji Manento alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, waliomtaka afafanue mara baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Haki za Binadamu na Biashara, kwa viongozi wa kampuni na asasi mbalimbali nchini.
Akifafanua kifungu hicho, pamoja na mambo mengine, alisema kinaeleza kuwa mahakama ndiyo mamlaka ya juu inayohakikisha haki za binadamu zinapatikana na inatekeleza hilo kwa misingi ya Katiba ambayo ni sheria mama.
Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho, mahakama ikishatoa uamuzi, hakuna wa kuongeza wala kupunguza na akitokea mtu mwingine kutoa hukumu kinyume na iliyotolewa mahakamani si sahihi, kwa kuwa mahakama imetekeleza wajibu wake na haijafanya kitu nje ya sheria zilizopo.
Kuhusu malalamiko ya wananchi hasa ndugu wa wafanyabiashara waliouawa Januari 14, 2006, Jaji Manento alisema amesoma kwenye magazeti kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ameonesha nia ya kukata rufaa, ambayo alisema ndiyo njia sahihi ya kuendeleza haki za binadamu na si vinginevyo.
Alisema katika Mahakama ya Rufaa, kesi itasikilizwa na majaji watatu na si mmoja kama ilivyokuwa katika Mahakama Kuu na kuongeza, kuwa kinachofanyika si kumpinga Jaji aliyetoa hukumu, bali ni kupitia kesi kwa mara nyingine.
Hata hivyo, alisema wananchi wanaolalamika, wana haki ya kufanya hivyo, kwa kuwa wanatekeleza moja ya haki za msingi za mwanadamu za kujieleza na kusikilizwa, ili mradi havunji sheria za nchi, lakini akawataka wananchi waheshimu uamuzi wa mahakama.
Aidha alisema kwa misingi ya maadili ya ujaji, haruhusiwi kudadavua hukumu iliyotolewa na Jaji mwenzake, hata kama ingekuwa na upungufu na kuwaonya baadhi ya watu wenye nafasi kama hiyo, kuwa macho wasije kukiuka maadili ya kazi.
Zombe na wenzake waliachiwa huru na Mahakama Kuu, Dar es Salaam Jumatatu wiki hii baada ya Jaji Salum Massati kueleza kuwa watuhumiwa hao wameonekana hawana hatia huku akiwataka waendesha mashtaka kuwatafuta watuhumiwa wawili (Saad na James) ambao walitajwa kuhusika moja kwa moja kuwapiga risasi wafanyabiashara hao.
Wafanyabiashara waliouawa katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, Kinondoni, Dar es Salaam Januari 14,2006 ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi, Mathias Lung’ombe na dereva teksi wa Manzese, Dar es Salaam, Juma Ndugu.
Kutoka Ulanga, John Nditi anaripoti kuwa wanakijiji cha Ipango, wanakusudia kufanya maandamano ya amani hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kutoa kilio chao juu ya kuachiwa huru kwa washtakiwa hao. Kutokana na uzito wa jambo hilo, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ulanga ilitarajia kukutana jana katika kikao cha kawaida na kuingiza ajenda ya hali ya kisiasa kuhusu hukumu hiyo kwa kuwaita viongozi wa matawi wa Ipango na wa kata ya Mahenge ili kujadiliana.
Pamoja na msimamo wa wanakijiji hao wa kufanya maandamano, ndugu wawili wa kiume wa familia ya Chigumbi, Selestin na Franco, kwa nyakati tofauti walisema familia yao haijaridhika na hukumu.
Hata hivyo walisema familia iko tayari kuungana na Serikali kukata rufaa ya kupinga hukumu hiyo licha ya familia kukosa uwezo wa kifedha na kuwaomba wananchi kuwaunga mkono.
Naye Mzee Lunkombe, ambaye ni mzazi wa marehemu Mathias alisema ni mapema kuzungumzia hatua familia inayotaka kuchukua baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo. Ofisa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Ipango, Festo Uyalo, alisema moyo wa kujitolea kwa wananchi wa kijiji hicho baada ya hukumu hiyo umekufa.
Pamoja na kukusudia kufanya maandamano hayo, wanachama wa CCM wamesusa fomu za uongozi wa serikali za vitongoji na vijiji unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2010 kwa madai kuwa serikali imewanyima haki.
Katibu wa tawi la CCM Ipango, Pacienci Lyahera, alithibitisha baadhi ya wanaCCM wa kijiji hicho kurudisha fomu walizochukua kuomba uongozi kupitia chama hicho ingawa hakutaja idadi yao, lakini hali haiko hivyo katika sehemu zote kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ulanga, Leticia Mtimba.
Hata hivyo alikiri kwamba eneo la kijiji cha Ipango, ambako ndiko kwao marehemu, upo ushawishi wa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa wananchi kuugomea uchaguzi huo wa Serikali za mitaa hasa kwa upande wa CCM.
No comments:
Post a Comment