Friday, August 28, 2009

Kikwete ana kwa ana na Maaskofu Katoliki

-Atarajiwa kupoza mtafaruku wa Waraka
-Kanisa lasita kumwalika kuwa mgeni rasmi wa hafla

WAKATI mjadala kuhusu waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki ukipamba moto, Rais Jakaya Kikwete, leo Jumatano, anatarajiwa kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Anthony Petro Mayala (69) atakapokutana uso kwa uso na Maaskofu wote wa Kanisa hilo ambao ndio waliobariki waraka huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, mbali ya Rais Kikwete, viongozi wastaafu akiwamo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wanatarajiwa kushiriki mazishi hayo.

Askofu Anthony Petro Mayala ambaye alifariki dunia ghafla Jumatano wiki iliyopita atazikwa leo ndani ya Kanisa Kuu la Epifania-Bugando jijini Mwanza.

Taarifa zilizopatikana wiki hii, Rais Kikwete anatarajiwa kuwasili Mwanza leo asubuhi na anatarajiwa pia kutumia fursa hiyo ambayo inaelezwa amekuwa akiitafuta “kuweka mambo sawa”, baada ya kuwapo sintofahamu kati ya Serikali yake na Chama cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza upande mmoja na Kanisa hilo lenye nguvu kubwa duniani upande mwingine.

Habari za ndani ya Kanisa Katoliki zinasema tangu baada ya Waraka wao kutoka, limekuwa halifurahishwi na mashambulizi yaliyotoka serikalini na katika CCM na kwamba kwa sababu hiyo kumekuwako na hali ya kutaka kumgomea ama kumsusa Rais Kikwete.

Dalili za mwanzo za hali hiyo ni kwamba Kanisa hilo, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, limesita kumwita Rais Kikwete kuwa mgeni rasmi katika shughuli za uchangiaji wa shule moja ya jimboni humo.

Habari za ndani zinaeleza kwamba Rais Kikwete alikuwa awe mgeni rasmi katika shughuli ya uchangiaji wa shule moja inayomilikiwa na Kanisa Katoliki lakini kutokana na kile kilichoelezwa ya kuwa ni “uzito mkubwa” ratiba ikabadilishwa na badala yake akaombwa kiongozi mmoja, mstaafu ndiye awe mgeni rasmi.

“Awali walimwalika kiongozi wa juu serikalini lakini wenzake wakasema si vyema kumtumia kiongozi huyo ambaye ni Mkatoliki na badala yake aende Rais Kikwete ambaye ni Mwislamu. Lakini kukatokea uzito mkubwa kutoka ndani ya uongozi wa Kanisa Katoliki na sasa inaelezwa bado haijaamuliwa ni nani awe mgeni rasmi japokuwa anatajwa sasa Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi,” anaeleza ofisa mmoja wa Kanisa ambaye yuko karibu na Kanisa Katoliki Dar es Salaam.

Uzito huo wa kumwalika Kikwete kuwa mgeni rasmi unaelezwa ndani ya Kanisa Katoliki kuwa unatokana na tamko la CCM kupinga matamko ya Kanisa hilo, tamko lililotanguliwa na kauli tata zilizotolewa na mwanasiasa mkongwe anayetajwa kuwa karibu na Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru.

Pamoja na ukweli kwamba CCM haijaukemea rasmi Waraka huo wa Wakatoliki, matamshi ya baadhi ya vigogo kama Mzee Kingunge yamekuwa hayapokelewi vizuri ndani ya Kanisa Katoliki nchini.

Kikikariri maamuzi ya wiki iliyopita ya Halmashauri Kuu yake, CCM, katika taarifa yake, kilionyesha wazi kutoridhishwa na Waraka huo lakini kikakwepa kuukemea, na badala yake kikaelekeza viongozi wakuu wa nchi kukutana na viongozi wa dini kurekebisha hali hiyo, huku viongozi wa Kanisa Katoliki wakionyesha wazi kutotaka kurudi nyuma.

Tamko la NEC lililotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, John Chiligati lilisema: “Baada ya NEC kuzingatia Waraka wa Maaskofu, na hasa malumbano na hisia tofauti zilizojitokeza kuhusu Waraka huo, imeelekeza kwamba viongozi wakuu wa nchi wafanye mazungumzo na viongozi wa dini zote ili kutafuta njia tulivu ya kusafisha hali ya hewa na kujenga umoja na utengamano katika jamii yetu.”

Habari zinasema kwamba huenda zikatolewa kauli za kujaribu kujibu mapigo kutoka kwa wanasiasa wakati wa mazishi ya leo.

Kanisa Katoliki ni moja ya makanisa yenye mtandao mkubwa wa kisayansi duniani kote na nchini Tanzania limejikita kwa kiwango kikubwa kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.

Pamoja na kutotaja chama, Waraka wa Kanisa Katoliki ambao sasa umekuwa ukienea kwa kasi nchi nzima umekosoa kwa kiasi kikubwa utendaji wa Serikali iliyoko chini ya Chama cha Mapinduzi na kutoa ushauri mbadala unaoelezwa kukera wakubwa.

Mbali ya kuandaa Waraka huo, Kanisa hilo tayari limeanza utekelezaji wa programu yake tokea Januari mwaka huu inayoishia mwaka 2011, ikiwa na lengo la kuwaandaa waumini wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na baadaye tathmini yake baada ya uchaguzi huo.

Sehemu ya programu ya Kanisa hilo inasema: “Watu wengi wanadhani kwamba mambo ya umma si sehemu ya majukumu yetu ya kidini na kiimani, na hivyo Kanisa halipaswi kujishughulisha na mambo hayo.

“Kinyume chake Kristo anatualika kuleta mafundisho ya Mungu, maadili ya asili yetu ya kibinadamu kama tulivyoumbwa na Mungu. Tunaalikwa kuyafanya hayo yawe ndio msingi na mwanga unaoongoza maamuzi na sera zetu.”

Katika programu hiyo ya kichungaji kumeandaliwa hatua madhubuti za ufuatiliaji ambao utaanzia kwa kufanyika mikutano ya makleri na viongozi wa halmashuri walei kujadiliwa katika ngazi ya Jimbo na kupewa umuhimu unaostahili.

“Katika kazi ya kuongoza mkutano wajumbe wa CPT (Wanataaluma Wakristo) na wawakilishi wa Serikali waalikwe kutoa maelezo juu ya hali halisi pale watu wanamoishi. Inapendekezwa paundwe timu ya Jimbo kwa ajili ya ufuatiliaji wa programu hii. Katika ngazi ya Parokia programu ilenge kufundisha wanavijiji/watu mitaani na katika jumuiya ndogo ndogo ili waweze kujadili masuala yaliyomo katika programu,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa kichungaji.

Pamoja na uongozi wa juu wa Kanisa kueleza kwamba hii si mara ya kwanza kwa Kanisa Katoliki kuandaa waraka wa kuongoza waumini wake na wananchi kuhusiana na mambo muhimu, hatua ya mwaka huu imeelezwa si ya kawaida na inaashiria kuwapo kwa ombwe kubwa katika mfumo wa kiuongozi na kijamii.

Tangu Waraka huo kutolewa na kuibua mjadala mkubwa, hiyo itakuwa mara ya kwanza Rais Kikwete kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki akiwemo Polycarp Kardinali Pengo. Watakutana ana kwa ana mjini Mwanza mjini Mwanza wakati wa mazishi ya Askofu Mayala.

No comments: