CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitasita kuwavua uongozi na hata kuwafukuza wanachama wake watakaovunja maadili, imeelezwa. Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema NEC imekemea tabia iliyoanza kujitokeza katika Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa wabunge na wajumbe wa CCM.
Alisema siku za karibuni kuliibuka tabia ya baadhi ya wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wa CCM kutoa matamshi hadharani yenye mwelekeo wa kuchafuliana majina na yanayoashiria kuvunjika kwa umoja na mshikamano ndani ya CCM na serikali zote.
Alisema hivi sasa Bunge la Tanzania na Baraza la Wawakilishi hali imekuwa mbaya kati ya wabunge na mawaziri kujibizana na kutoleana lugha kali na kutishana mpaka wengine kufikia hatua ya kuomba kuongezwa ulinzi.
“Viongozi watakaovunja maadili haya watakuwa wamejibainisha kwamba hawana nia njema na CCM na watahesabiwa ni wasaliti wa chama na hivyo chama hakitasita kuwapa adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa uongozi na hata kufukuzwa katika chama,” alisisitiza.
Alisema hali hiyo inatokana na kutambua matatizo ya matamshi na vitendo visivyoridhisha katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, hivyo kuwapo haja ya kutafuta undani wa matatizo hayo na kupendekeza kwa Kamati Kuu njia za kuyatatua.
Chiligati alisema kamati hiyo itaongozwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi na kuwataja wajumbe wengine kuwa ni pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana ambaye aliwahi pia kuwa waziri.
Kamati hiyo pia itaangalia utendaji kazi wa kamati za chama bungeni na katika Baraza la Wawakilishi, kwa nia ya kubaini upungufu uliopo ili kupendekeza kwa njia za kurekebisha upungufu huo. Chiligati alisema pia itaangalia uendeshaji wa shughuli za Bunge na Baraza na kushauri namna ya kuimarisha panapostahili.
Alilifananisha Bunge na kikundi cha Orijino Komedi, ambapo ukifika muda wake, watu wanawahi televisheni kuangalia nani atamnyooshea mwenziwe vidole. Aliongeza: “Matamshi haya yana mwelekeo wa kudhoofisha Muungano wetu, Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na kukemea tabia hii pia imetoa maagizo”.
Aliyataja maagizo hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa CCM kurejea katika nidhamu ya chama na kuzungumzia masuala ya chama katika vikao rasmi na si vinginevyo, kamati za wabunge wa CCM na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM kutumika kujadili masuala yahusuyo chama ndani ya vyombo hivyo.
Alisema pia NEC imeziagiza Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutumia taratibu zilizopo kushughulikia kero za Muungano badala ya kufanya suala la mafuta kuwa la upande wa Zanzibar.
Alisema NEC pia ilionya kuhusu dhana inayojengeka kwamba vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini, inahusu kundi dogo la wanachama wa CCM na kwamba usahihi juu ya suala hilo, ni kuwa vita hiyo ni ya wana CCM wote, kwa mujibu wa Katiba ya chama na ni lazima iendelee kuhusisha wanachama wote wenye mapenzi mema na nchi.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Chiligati alisema hali ni shwari isipokuwa malumbano yanayosababishwa na viongozi wachache wa ngazi za juu ndiyo yamekuwa yakitishia amani. “Inashangaza viongozi hawa wa kisiasa wa ngazi za juu badala ya kuwa mfano katika uongozi wao, ndio wanakuwa wa kwanza kuanzisha malumbano,” alisema Chiligati.
Wakati huo huo, NEC ilisikitishwa na hali iliyojitokeza bungeni ya kutoa maneno ya kejeli dhidi ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Chiligati alisema Mkapa katika kipindi chake, aliliongoza Taifa kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa aliinua hali ya uchumi, aliendeleza miundombinu, huduma za kijamii hususan elimu, afya, maji na kulijengea heshima Taifa.
Alisema Mkapa anastahili pongezi si kejeli, anastahili heshima na si dharau na anastahili kuenziwa na si matusi na aliongeza kuwa kwa kuzingatia hayo, NEC iliwataka watanzania wote wenye nia njema na nchi, waache kumchafua na kumkejeli Mkapa na badala yake wampe heshima anayostahili na aachwe apumzike. Jana Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliripotiwa kunusurika kunyang’anywa kadi yake ya uanachama na NEC, baada ya baadhi ya wajumbe kudai kuwa anakigawa chama hicho.
No comments:
Post a Comment