Thursday, August 27, 2009

Waraka ni Neno la Mungu-Pengo

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema ujumbe na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na makanisa kupitia kwa viongozi wake, wakiwamo maaskofu na mapadri kwa waumini na wananchi, si lazima zipate baraka za Serikali.

Pengo alisema hayo jana kwenye Kanisa la Kawekamo wakati akiendesha misa maalumu ya maziko ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Anthony Mayala (69) ambaye alifariki dunia wiki iliyopita kwa ugonjwa wa moyo.

Mbali ya kutoa wasifu wa Askofu Mayala kwa maelfu ya waumini na wananchi waliofurika kanisani hapo, ambaye alimwelezea kuwa kiongozi wa kiroho mwadilifu asiyekuwa na makuu, alikiri Kanisa kupoteza mtu hodari.

"Anthony ingawa amekufa akiwa kijana, amestarehe, Mungu amemstarehesha tu, alikuwa mtu mwema, sina shaka na hilo, maana nilimfahamu siku nyingi tuliishi naye," alisema.

Pengo alisema hivi sasa kuna hali ambayo inawabana viongozi wa madhehebu ya dini ambayo hailengi kuwapa uhuru wa kutekeleza wajibu wao kwa waumini na kuhoji Tanzania ya leo inaelekea wapi.

“Tunapoambiwa, maaskofu msiandike barua mpaka tuzione, tutafika wapi? Maaskofu wanapoandika barua na ujumbe kwenda kwa waumini, hutekeleza Neno la Mungu, msiwafundishe namna ya kuandika mambo ya kimungu,“ alisema Pengo.

Pengo alifananisha hali hiyo na mfumo wa kikomunisti uliokithiri katika Poland, na kwamba nchi hiyo ilifikia mahali ikaamua Ukomunisti uhubiriwe baada ya kushindwa kuizima imani ya Mungu.

“Poland waliposhindwa kuzima imani ya Mungu waliamuru Mungu ahubiriwe kutokana na imani ya ukomunisti, je Tanzania ya leo iko tofauti na hapo? Je, tunakoelekea ni wapi?” alihoji Kardinali Pengo ambaye hata hivyo alisisitiza kuwa alikuwa Mwanza kwa lengo la kufanya ibada ya maziko na hakuwa na nia ya kujiingiza kwenye ajenda za kisiasa.

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alionekana kukerwa na maneno yanayoendelea hivi sasa nchini, akiweka bayana kuwa umetokea mfumo unaokuja kwa kasi wa wananchi kulaani ufisadi na mauaji ya vikongwe na suala zima la rushwa bila kuja na njia mbadala wa utatuzi wake.

“Kila siku tunasikia mauaji ya albino, vikongwe na watu wasiokuwa na hatia, tunasikia juu ya watu wanaojihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa na malalamiko mengi katika Taifa letu hivi sasa, jambo la kusikitisha ni kuwa wote tunalalamika na kulaani matendo hayo, lakini tungekuwa tunayachukia kutoka kwenye nyoyo zetu, yasingetokea,” alifafanua.

Alisema ambacho kingefanyika ni jamii kuchukua njia mbadala za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo na si kulaumu na kulaani na akasema huenda jamii imechukua hatua hiyo kwa lengo la kujenga chuki, lakini na wao wakipata nafasi ni dhahiri watajihusisha na ufisadi na rushwa.

“Kila mtu ajiulize, hizi kelele zinapigwa kwa dhati? Maaskofu nasi tujiulize je tunapiga kelele hizo tukiwa na uhakika zinatoka nyoyoni? Ama ni kama kuwaonea wivu hao walio kwenye ufisadi kwa sababu tu hatujaipata nafasi hiyo na tukiipata tutaitumia kuwa mafisadi?,” alisema na kuitaka jamii iache mijadala ya ufisadi kwa vile inachochea hasira kwa jamii kwa kumwona kila mtu ni fisadi.

Awali kabla ya maziko, maaskofu wote 31 waliohudhuria, walifanya maandamano kuelekea kwenye uwanja wa misa ambako mwili wa marehemu uliwekwa na viongozi wakiwamo mapadri na watawa walitoa heshima za mwisho. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) lilimtangaza rasmi Padri Renatus Nkwande ambaye alikuwa msaidizi wa Mayala kuwa Msimamizi Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza hadi hapo Papa atakapofanya uteuzi rasmi.

Akimtangaza rasmi jana mbele ya baraza hilo la maaskofu, Askofu Nestor Timanywa wa Jimbo Kuu la Bukoba alisema kuwa uteuzi huo ulianza rasmi jana na maaskofu walimtakia kila la heri kwa majukumu yake mapya.

Naye Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwasili kanisani hapo mchana, akifuatana na mkewe Mama Salma, akitoa salamu za Serikali na Taifa kwa jumla, alisema huo ni msiba mkubwa wa kitaifa kwani aliyepotea si tu kiongozi wa kiroho, bali mtu makini na mahiri wa kuliletea Taifa maendeleo, hususani katika sekta ya elimu.

Rais pia alitoa salamu maalumu kwa Kardinali Pengo akimwelezea Mayala kuwa mtu mwenye hekima, busara na ambaye hakuwa na makuu wala makeke.

Baadaye msafara wa Rais uliondoka kwenda Kanisa Kuu la Bugando na kufuatiwa msafara wa viongozi wa dini na ibada ya maziko ilifanywa kanisani hapo na Rais wa TEC, Askofu Jude Ruwa'Ichi na marehemu alizikwa ndani ya Kanisa hilo.

Viongozi mbalimbali akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri na viongozi wengine wa Serikali na wananchi walifurika kanisani hapo kumsindikiza marehemu Mayala.

No comments: