Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane waliokuwa wanashitakiwa kwa mauaji, wameachiwa huru na mahakama kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kupeleka ushahidi usio na mashaka kuthibitisha kushiriki kwao katika kufanya mauaji hayo.
Walioachiwa huru na Zombe ni Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi (ASP) Ahmed Makele, Konstebo Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula. Wengine ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Jaji Salum Massati katika hukumu yake aliyoitoa jana, alisema mahakama imeridhika kuwa wafanyabiashara watatu na dereva teksi waliuawa kwa risasi huko kwenye msitu wa Pande, Mbezi Dar es Salaam; lakini waliofanya mauaji hayo hawapo mahakamani.
Alisema upande wa mashitaka unapaswa kuendelea kuwatafuta na kuwakamata wale waliowaua; kwani walioko mahakamani hakuna ushahidi unaoonesha kuwa ndio waliofyatua risasi na kuwaua watu hao wanne.
“Wapo walioua ila hawapo mahakamani, polisi watafuteni waletwe mahakamani,” alisema Jaji Massati katika hukumu ambayo iliduwaza umati uliofurika mahakamani hapo. Jaji Massati alisema kitendo cha upande wa mashitaka kuegemea kwenye maelezo ya washitakiwa Rashid Lema na Koplo Rajabu Bakari hauwezi kuishawishi mahakama hiyo iwatie hatiani washitakiwa hao.
Lema alikufa wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa. Alisema pamoja na kuwepo ripoti ya daktari inayoonesha marehemu kuuawa kwa kupigwa risasi, mahakama haiwezi kujiridhisha kuwa ni washitakiwa ndio waliofyatua risasi na kuwaua marehemu hao wakati ushahidi wa kuhusika kwao haupo.
Hukumu hiyo iliyosomwa kwa zaidi ya saa tano kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:25 alasiri, Jaji alikubaliana na hoja ya upande wa utetezi kuwa upande wa mashitaka walifanya upelelezi wa kesi hiyo haraka na kuwaacha wauaji wakiwa nje.
Akimchambua mshitakiwa wa kwanza Zombe, Jaji alisema mshitakiwa huyo wakati wa mauaji yanafanyika alikuwa ndiye Kamanda wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi; hivyo alikuwa na jukumu la kujua wahalifu hao walikohifadhiwa baada ya kukamatwa.
Alisema hata baada ya kusikia mauaji yametokea, Zombe hakuonesha nia ya kwenda kuona ambako ilidaiwa kulikuwa na mapambano kati ya polisi na majambazi badala yake alienda Kituo cha Polisi kuulizia fedha. “Hapa ni wazi kuwa ni kweli alijua kilichokuwa kinaendelea, lakini hata hivyo upande wa mashitaka umeshindwa kuonesha namna mshitakiwa huyu alivyoshiriki kwenye mauaji hayo,” alisema Jaji Massati.
Alikataa baadhi ya ushahidi uliotolewa kuwa Zombe aliwafundisha wenzake cha kujitetea kwenye Tume ya Jaji Kipenka Mussa. Lakini pia alisema madai kuwa Zombe siku ya tukio alikuwa anawasiliana na Bageni hazikuwa za kweli.
Kwa upande wa Bageni, Jaji Massati alisema licha ya kuwepo ushahidi wa kuongoza msafara hadi kwenye msitu wa Pande, na kutajwa na washitakiwa wawili kuwa ndiye aliyeamuru Koplo Saad afyatue risasi, ushahidi huo haukuungwa mkono na shahidi mwingine hivyo hauwezi kukubaliwa na mahakama.
“Kwa hali hiyo ushahidi wa namna hii hauwezi kukubalika kisheria, ni lazima uungwe mkono na mashahidi wengine jambo ambalo upande wa mashitaka walishindwa kulitimiza; hivyo nasema hana hatia juu ya kesi ya mauaji,” alisema.
Akimwelezea Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makelle, Jaji Massati alisema ushahidi uliopo mahakamani unathibitisha kuwa alikuwepo wakati washitakiwa wanakamatwa na alishiriki kuchukua mfuko uliokuwa na fedha.
Alisema kwa Ofisa Mwandamizi wa Polisi kama Makelle, alikuwa na wajibu wa kuchukua kielelezo hicho na kukihifadhi, lakini akasema kuwepo kwake pale hakuwezi kumtia hatiani kuwa alishiriki kwenye mauaji.
“Kinachomuunganisha mshitakiwa na marehemu ni hili begi la fedha, zaidi ya hapo hakuna mahali upande wa mashitaka umetoa ushahidi wa kuhusika kwake kuwaua marehemu, hivyo na yeye hana hatia,” alisema.
Pia akimwelezea Jane na Saro ambao walikuwa na Makelle siku ya tukio, Jaji Massati alisema pamoja na kuwepo eneo la tukio, lakini upande wa mashitaka haukupeleka ushahidi kama walihusika kuua.
Kwa upande wa Bakari ambaye alikuwa mshitakiwa pekee aliyekiri kuwepo eneo la tukio wakati mauaji yanafanyika, Jaji alisema mshitakiwa huyo licha ya kuungama kuwepo siku ya tukio; lakini kuna ushahidi kuwa hakushuka kwenye gari wakati mauaji yanafanyika.
Alisema alishuhudia Koplo Saadi anafyatua risasi, lakini alikataa maelezo yake aliyodai kuwa muuaji aliamriwa na Bageni. “Madai haya hayana msingi kwa namna yalivyo na yeye alisikia na hakushuhudia wakati Bageni anatoa amri hiyo,” alisema Jaji Massati.
“Huyu Saad anayetajwa hapa mahakamani hayupo, huyu ndiye anayedaiwa kuua,” alisema akimwelezea Mabula na Shonza, alisema ushahidi uliopo ni kwamba walikuwa kwenye doria siku ya tukio, lakini upande wa mashitaka haukupeleka ushahidi unaoonesha kuwa walikuwepo Pande ambako mauaji yalifanyika na kwamba walihusika kuwaua marehemu.
Akimwelezea Koplo Gwabisabi, Jaji Massati alisema hakuwepo Pande kwani siku ya tukio aliamriwa kuendesha gari la marehemu ambao walikamatwa na kushikiliwa na polisi. “Katika hali hii nashawishika kusema kuwa naye hakuhusika kwenye mauaji na wala Pande hakwenda,” alisema Jaji Massati.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Juni mwaka jana na imemalizika jana. Upande wa mashitaka uliita mashahidi 37 kuthibitisha mashitaka yao, lakini kati ya wote hao Jaji Massati alisema hakuna aliyethibitisha washitakiwa kuua.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Mugaya Mutaki alisema watawasiliana na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) wajue kama watakata rufaa ama la.
No comments:
Post a Comment