Friday, July 29, 2011

Lissu, Lema wafukuzwa bungeni

SARAKASI za wabunge bado zinaendelea bungeni mjini Dodoma, jana ilikuwa zamu ya wabunge watatu wa Chadema kutolewa nje ya kikao.

Wabunge hao Godbless Lema wa Arusha Mjini, Tundu Lissu wa Singida Mashariki na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini, walitolewa nje ya ukumbi na Naibu Spika, Job Ndugai, muda mfupi baada ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kumaliza kusoma hotuba yake.

Lema alikuwa akichangia Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, aliyoitoa jana kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2011/12, akiomba Bunge limwidhinishie matumizi ya Sh bilioni 482.3.

Baada ya Lema kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama akiomba kutoa taarifa na pia kuomba Mwongozo wa Naibu Spika kutokana na hotuba ya Lema.

Lukuvi alisema Watanzania wamekuwa wavumilivu, hivyo kutokana na hotuba ya Lema aliyoeleza ilijaa uchochezi, wapime wenyewe na kwamba hotuba hiyo ina matatizo na inashangaza mbunge aliyechaguliwa na wananchi kutoa maneno ya uchochezi na yasiyo ya kistaarabu.

“Mbunge unaweza kusema Tanzania si nchi ya haki… watawala wanatesa wananchi, uchaguzi wa meya Arusha ni batili … polisi wasitii maagizo ya makamanda wao, hotuba hii kwa kweli imejaa uchochezi mkubwa kwa nchi,” alisema Waziri Lukuvi na kushangiliwa na wabunge.

Hata hivyo, wakati Lukuvi akiendelea kuzungumza, Lema, Lissu na Msigwa kwa nyakati tofauti walitaka nao kuzungumza ili kumkatisha Lukuvi, lakini Naibu Spika aliwaambia wakae chini amalizie na wavumilie.

Naibu Spika alitamka mara kadhaa kuwataka Lissu, Lema na Msigwa wazime vipaza sauti, lakini hilo halikuwezekana, hali iliyomlazimu kuchukua hatua ya kuwatoa nje kwa kukiuka kanuni ya Bunge ya kuzungumza bila ruhusa.

Tofauti na ilivyokuwa juzi wakati Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema) alipotolewa nje na Mwenyekiti wa Bunge pia kwa kuvunja kanuni kama wenzake wa jana, lakini hali ilikuwa tofauti kwani Lissu na wenzake walitolewa na askari nje kabisa ya lango la Bunge na kupanda gari wakaondoka eneo hilo.

Kwa mujibu wa Naibu Spika, taratibu ndivyo zinavyotaka, si kwamba Mbunge anatolewa kwenye jengo la Bunge na kukaa maeneo mengine bali anatolewa nje kabisa hadi siku inayofuata atakaporuhusiwa kuingia tena bungeni.

Akifafanua baadaye, Ndugai alisema wananchi hawapendi ubabe na kuwaonya wabunge kwamba miaka mitano si mingi bungeni. Alisema alitumia kanuni ya 60(2) kuwatoa nje wabunge hao, ambapo kanuni hiyo inaeleza kwamba mbunge hataruhusiwa kuzungumza hadi aitwe kwa jina au wadhifa.

Kuhusu hotuba ya Lema, alisema Serikali ilionesha uvumilivu mkubwa kwa kumsubiri mpaka amalize, licha ya kuwapo maneno ambayo hayakuwa ya kiungwana, lakini wapinzani wao walishindwa kumsubiri Waziri Lukuvi amalize kuzungumza.

Pia alisema sera za matumizi ya hoja ya nguvu Afrika hairuhusiwi na Katiba na kwamba masuala mengine ambayo pia yalizungumzwa kwenye hotuba hiyo kama jambo halina uthibitisho, ni vema pia wahusika wakaliacha.

Alimshangaa Msigwa kwamba wakati Lema akizungumza, yeye alikuwa akishangilia kwa nguvu wakati hakupaswa kufanya hivyo kwa vile ni mtumishi wa Mungu.

Aliwaomba wabunge wajitahidi kutumia ishara ya kuhamasisha amani na kueleza kuwa kwa kawaida, hotuba inamfikia Spika siku moja kabla, lakini kanuni hazimpi nafasi ya kuzuia kutolewa, isipokuwa kwa baadhi ya vifungu na si hotuba yote.

“Ndiyo maana leo nilimzuia kusoma aya hii katika hotuba yake, ambayo inasema: ‘Serikali inayohubiri amani kila kukicha kwa kutumia vyombo vyake vya mabavu, imekuwa inakamata wananchi wasio na hatia na kuwabambikizia kesi za uongo pale wanaposhindwa kutoa rushwa katika vituo vya Polisi na mahakamani,” alisema Naibu Spika na kueleza kuwa jambo hilo halina uthibitisho, hasa kwa kuhusisha mhimili mwingine wa Dola kwa maana ya Mahakama.

Pamoja na mambo mengine katika hotuba yake, Lema alieleza kuwa pengine wapinzani walikuwa dhaifu kudhibiti hujuma na dhuluma walizofanyiwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini sasa hawatakuwa tayari kuhujumiwa uchaguzi wowote ujao ukiwamo wa Igunga.

“Mifano hiyo michache inaonesha nchi hii haina amani ya kweli, kilichopo si amani bali utulivu unaojengwa na nidhamu ya uoga. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahadharisha kuwa utulivu wa nchi hii upo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu kuu mbili.

“Kwanza ni kuongezeka kwa matabaka ya Watanzania wengi walio masikini na Watanzania wachache matajiri na wawekezaji wanaopata zaidi haki kwa sababu ya uwezo wao wa kifedha.

“Iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa, basi dalili zipo wazi kuwa uvumilivu wa Watanzania wengi masikini sasa umefika mwisho na lolote linaweza kutokea.

“Amani ya nchi hii ipo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu ya mtazamo potofu wa serikali yetu, kuamini kuwa njia sahihi ya kudumisha amani ni kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwafyatulia risasi, mabomu ya machozi na kuwapiga virungu.

“Hata hivyo sasa wananchi wameanza kuzoea hali hiyo na ni dalili mbaya kwa utawala, ni lazima Serikali ikaelewa kuwa umma wa Watanzania milioni 40 kamwe hauwezi kusambaratishwa na risasi za Jeshi la Polisi ambao idadi yao ni takribani 50,000.

“Kambi Rasmi ya Upinzani kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania, inaionya Serikali inayoongozwa na CCM, kwamba amani ya nchi hii kamwe haiwezi kulindwa na FFU wala majeshi,” alisema Lema na kuwataka polisi nchini wasitii maagizo yoyote katili ya makamanda wao.

Awali katiba hotuba yake, Waziri Vuai alisema hali ya nchi inaendelea kuwa ya amani na utulivu, lakini baada ya uchaguzi uliopita, zimeanza kuonekana dalili za uvunjifu wa amani zikichangiwa na viongozi wa kisiasa.

Alisema baadhi ya viongozi hao wanaandaa maandamano na mikutano ya mara kwa mara, hali inayowanyima wananchi fursa ya kushiriki shughuli za maendeleo na miradi ya kuwapunguzia umasikini.

Alisema muda unaotumika kuandaa maandamano kama ungetumika kwa shughuli za maendeleo bila shaka Tanzania ingepunguza umasikini kwa kiasi kikubwa. Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abadallah (CCM) akichangia hotuba hiyo, alisema kilichozungumzwa na wapinzani si sahihi, kwani haki bila wajibu ni fujo na kwamba watu wanatakiwa kutii mamlaka.

Alisema kama Serikali ikiwa haiwachukulii watu hatua, itaonekana legelege na kwamba lazima polisi waendelee kufanya kazi zao vizuri na kueleza kuwa anashangaa mbunge anaweza kutoa maneno makali na wananchi wakaunga mkono.

“Nauliza kuna kiongozi gani amewahi kuumia katika maandamano? Kuna kiongozi aliwahi kuwaambia wanawake miaka ya nyuma wavue nguo ili kuonesha malalamiko yao, nikawaambia mwambieni aanze mkewe.

“Kupinga kila kitu si ushujaa, uchaguzi umekwisha aliyeshinda kashinda, tusiwe kama Savimbi (Kiongozi wa zamani wa chama cha Unita cha Angola ambaye ni marehemu), yeye akishindwa anasema kaibiwa kura,” alisema Mbunge huyo.

Mahakama Yamwachia Huru Mtuhumiwa Wa Richmond

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, imemwachia huru Naeem Gire aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kughushi na kuwadanganya serikali kuwa mitambo ya Richmond ina uwezo wa kufua megawati 100 za umeme.

Gire ametoka kizimbani akichekelea baada ya hakimu wa mahakama hiyo, Waliarwande Lema , kutamka kuwa anamuona hata kesi ya kujibu kutokana na ushahidi uliofikishwa mahakamani na serikali kushindwa kumridhisha ili amuone kuwa na kesi ya kujibu.

"....Baada ya kupitia ushahidi katika vipengele vyote nimeona kuwa hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa kuridhisha kumuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu...kesi hii ni miongoni mwa kesi kadhaa ambazo huletwa mahakamani na kisha kuitwisha lawama mahakama", alisema Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Waliarwande Lema.

Thursday, July 28, 2011

Si kweli kwamba hatuwezi kuchimba wenyewe madini

-Asema juhudi za kumchafua Mwalimu hazitafanikiwa
-Ashangaa viongozi kusaliti juhudi zake
-Atamba CHADEMA imebadilisha mambo Musoma Mjini

JULAI 3, mwaka huu, Mwandishi, Godfrey Dilunga wa Raia Mwema, alifanya mahojiano na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ni mbunge wa kwanza jimbo hilo kutoka Upinzani tangu Uhuru wa Tanganyika.

Raia Mwema: Jina la Nyerere linaashiria unatoka katika familia kubwa katika siasa za Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla; yaani familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tueleze uhusiano uliopo kati yako na Mwalimu Nyerere.

Nyerere: Kwanza nikueleze jambo ambalo wengi hawalifahamu. Jina langu mimi haswa si Vincent. Jina langu ni Nyerere tangu kuzaliwa, hili la Vincent ni jina la ubatizo. Ni sawa hata kwa Mwalimu Nyerere, jina lake la kuzaliwa ni Kambarage. Hili jina la Julius ni jina la ubatizo.

Kwa hiyo, Mwalimu Nyerere jina la Julius na Kambarage yote ni ya kwake. Hakuna jina la mzazi wake hapo. Julius jina la kubatizwa na Kambarage jina la kienyeji kabla kubatizwa.

Sasa kama ulivyoniuliza, mimi ni mtoto wa Josephat Nyerere ambaye yeye na Mwalimu Nyerere ni mtu na mdogo wake. Huo ndiyo uhusiano uliopo ndani ya familia yetu hiyo.

Raia Mwema: Familia ya Nyerere imejikita zaidi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ingawa wakati fulani Makongoro Nyerere aliwahi kuwa mbunge wa NCCR-Mageuzi Arusha. Wewe imekuwaje ujiunge na Upinzani, hususan CHADEMA?

Nyerere: Kwanza ni suala la kuelewa zaidi. Unajua hii ni nchi yetu sote, masuala ya vyama ni utaratibu tu lakini msingi mkuu ni uongozi utakaowaletea wananchi maendeleo kwa kadiri ya matarajio yao.

Mimi ni mkazi wa Musoma, nafanya shughuli zangu pale muda mrefu. Katika uongozi uliokuwapo (ubunge) nilikuwa naona mambo mengi hayaendi sawa; hasa masuala ya maendeleo na uhusiano wa kisiasa kati ya mbunge na sehemu kubwa ya wananchi.

Hali hiyo ilinishawishi kutaka kugombea ubunge na niliamini kwamba nitaweza kugombea na kwa kusaidiana na wakazi wenzangu wa Musoma Mjini ningeshinda na tungeshirikiana ili kushinda kwa pamoja kujiletea maendeleo.

Raia Mwema: Nani alikuwa wa kwanza kumdokeza wazo lako hili la kutaka kugombea ubunge?

Nyerere: Mtu wa kwanza kabisa ni kaka yangu Makongoro Nyerere. Nilimweleza dhamiri yangu, lakini hakutaka kuniunga mkono. Alinishauri niache masuala hayo kwa wakati huo, nijipe muda wa kutafakari zaidi. Lakini ushauri wake niliuheshimu japo sikuutekeleza kama alivyotaka.

Baadaye niliwaeleza pia baadhi ya wakazi wenzangu wa Musoma Mjini kuhusu suala hilo, wakiwamo pia rafiki zangu. Walishangaa na kuniuliza unazo fedha? Umezipata wapi?

Raia Mwema: Kwa nini walikuuliza suala la fedha?

Nyerere: Waliniuliza hivyo kwa sababu ilikuwa ni utamaduni, ukitaka kugombea ubunge na hasa Musoma Mjini lakini pia hata mbunge aliyekuwapo alikuwa na fedha nyingi. Kwa hiyo waliamini ili kushindana naye ni lazima nawe uwe na fedha za kutosha.

Kwa hiyo, fikra zilizokuwapo ni uchaguzi unaoongozwa na nguvu ya fedha na si masuala ya uadilifu au uwezo wa kuunganisha wananchi katika maendeleo.

Raia Mwema: Uliichukuliaje hali hiyo, uliogopa na kufirikia upya kukimbia uamuzi wako wa kutaka ubunge?

Nyerere: Haikunikatisha tamaa na kimsingi niliichukulia kama changamoto ya kufanikisha nia yangu, nikizingatia kuwa sehemu kubwa ya wananchi ambao ni wapiga kura hawana fedha kama ilivyo kwangu na pengine wengine hawana fedha zaidi....ni masikini.

Niliamini watu namna hiyo ndiyo mtaji wangu, nitawaelewesha na bila shaka watanielewa na kwa kweli walinielewa kila hatua niliyofanya waliniunga mkono hadi nikawa mbunge na kampeni zangu zilikwenda vizuri sana.

Raia Mwema: Mwanzo ulieleza mshauri wako wa kwanza alikuwa Makongoro Nyerere, kuna masuala fulani awali mliwahi kushirikiana hasa katika siasa? Nini kilishawishi hasa uanze kumfuata yeye ili umueleze wazo lako?

Nyerere: Ni kweli kwamba Makongoro amewahi kuwa mbunge wa NCCR-Mageuzi na anajua masuala haya, lakini pia mimi niliwahi kuwa kampeni meneja wake wakati anagombea uenyekiti wa CCM - Mkoa wa Mara.

Niliendesha kampeni zake vizuri na akashinda. Kwa hiyo, katika masuala ya siasa tuko karibu zaidi na hata masuala mengine.

Raia Mwema: Kumekuwapo na madai kwamba; ingawa yeye ni CCM lakini alikuwa akikusaidia kampeni zako za ubunge hadi ukashinda. Unazungumziaje hili?

Nyerere: Ukiliweka hivyo, unakuwa umekosea. Leo niseme wazi kwamba walionisaidia ni wana-CCM karibu wote wa Musoma Mjini, na walifanya hivyo kwa sababu maalumu, ukiwamo udhaifu wa mbunge aliyekuwapo na ambaye ndiye aliyepitishwa na chama chake kugombea ubunge.

Kwa hiyo, si Makongoro aliyenisaidia na kwa kweli yeye mwenyewe alikwishawahi kufanya kampeni dhidi yangu, akimnadi mgombea wa CCM. Ndiyo, alikuwa akifanya mikutano mbalimbali ya kampeni ya chama chake lakini mimi nilikuwa na wana-CCM wa kawaida, walinisaidia kwa hali na mali. Amewahi kufanya mkutano Shule ya Msingi Mkendo, akamnadi mgombea wa CCM sio mimi. Kwa hiyo, si kweli kwamba alinisaidia.

Na kwa kweli, hiyo imekuwa changamoto kubwa sana kwangu; kwa sababu hawa watu wote walionichagua wamekuwa na matarajio makubwa kwangu lakini nashukuru kazi yangu inakwenda vizuri na kumeanza kutokea mabadiliko makubwa ya maendeleo jimboni. Ni changamoto na nitahakikisha wana-CCM hao na wananchi wengine kwa ujumla hawajutii uamuzi wao huo hata siku moja.

Raia Mwema: Umezungumzia udhaifu wa mbunge aliyepita ndiyo sehemu ya nguvu zilizochangia ushindi wako. Ni udhaifu gani huo?

Nyerere: Hilo liko wazi, sio la kuficha ni suala linalojulikana Musoma Mjini. Huyo mbunge alihodhi biashara karibu zote kubwa Musoma Mjini, madiwani karibu wote wakati huo walikuwa wakandarasi. Kwa hiyo, miradi mingi ya Halmashauri ilikuwa ikizunguka katika ‘himaya’ yao. Wachache pale Musoma Mjini walionekana kuwa na maisha mazuri zaidi, kwa hiyo alijenga mtandao wake kwa kuhakikisha wenye maamuzi ndiyo wanaonufaika, akasahau wananchi wa kawaida.

Lakini pia hakuwa ametekeleza ahadi zake nyingi za maendeleo kwa wananchi wa jimbo la Musoma Mjini.

Raia Mwema: Katika akili ya kawaida, kuna mantiki mtu akisema jina kubwa la Mwalimu Nyerere limekusaidia pia kushinda. Unakubaliana na mantiki hii hasa ukizingatia siku hizi watoto wa wakubwa wamekuwa vinara wa mikakati ya kisiasa?

Nyerere: Unachosema wengi ndiyo wanachokizungumza ambacho si kweli kwangu na hata katika familia yetu kwa ujumla. Hili suala la kufanya siasa kwa kutumia surname (jina la ukoo) hazipo kwangu wala kwa yeyote kwetu na kimsingi sio siasa pekee, hata masuala mengine.

Mimi nimekuwa mfanyabiashara lakini sijawahi kufanya mambo yangu kwa kutumia nguvu za surname, na hivyo ndiyo malezi yetu yalivyokuwa.

Sisi tumekuwa tukiishi maisha ya kawaida, tumesoma shule za kawaida na mimi mwanangu anasoma shule hizo hizo. Kwa hiyo, hatufanyi siasa za surname.

Kwanza, mimi na wanafamilia wenzangu tunajivunia kuwa katika ukoo huo lakini hakuna anayetumia jina hilo kwa manufaa fulani binafsi. Hata wazazi wetu hawakuwa hivyo, kumbuka walikuwa watoto wa chifu, lakini hakuna aliyejigamba na cheo hicho. Hata maisha yetu, hatukutumia umaarufu wa Mwalimu Nyerere akiwa Rais na hata alipostaafu kwa manufaa yetu.

Hatukuwa tukiishi maisha ya ki-Ikulu-ikulu, wakati Mwalimu akiwa Rais. Tuliishi maisha ya kawaida na kusoma shule za kawaida ambazo zilikuwa bora zaidi.

Raia Mwema: Inaelezwa kwamba Mwalimu aliwekeza muda wake zaidi kutumikia nchi kuliko familia na watoto wake hakuwapa elimu nzuri nje ya nchi au popote na hakuiachia mtaji au raslimali nyingi kama ilivyo kwa marais wengi Afrika. Ukweli ukoje hapa?

Nyerere: Ni kweli Mwalimu Nyerere alitumia muda wake mwingi kutumikia nchi pengine ukilinganisha na masuala ya familia, na kwa kweli hilo ni jambo la kujivunia kwa sababu ni kigezo cha kiongozi bora katika uongozi wa juu wa nchi.

Ukitazama viongozi wengi waliotumia nafasi zao za uongozi kutumikia familia zao badala ya Taifa hawakufika mbali. Walijenga uadui mkubwa na wananchi wao na matokeo yake hata usalama wa familia zao unakuwa shakani. Wewe unajua kinachoendelea katika baadhi ya nchi Afrika, kama Misri na kwingine. Viongozi wamechuma mali nyingi, wamesahau wananchi wameondoka madarakani hawana heshima yoyote, lakini angalia Mwalimu Nyerere, katumikia wananchi na bado heshima yake ipo hadi leo.

Kuhusu hili suala la kutosomesha watoto wake, hebu niambie mtoto gani wa Mwalimu Nyerere hakusoma vizuri? Wote wamesoma vizuri. Pengine suala ni kwamba wamesoma katika shule za kawaida kama ilivyo kwa watoto wengine wa masikini hapa nchini. Mwalimu alisomesha watoto wake lakini katika shule za kawaida, si za kifahari.

Raia Mwema: Tueleze, uliingia CHADEMA ili kugombea ubunge...ulikuwa mwanachama wa muda gani kabla ya uchaguzi mkuu, na kabla ya hapo ulikuwa katika chama gani?

Nyerere: Kwanza sikuwa mwanachama wa chama chochote isipokuwa nilikuwa shabiki wa CCM. Hata nilipokuwa meneja wa kampeni za Makongoro nilikuwa shabiki mkubwa wa CCM.

Baadaye nilijiunga na CHADEMA Oktoba 20, mwaka 2008, miaka takriban miwili kabla ya uchaguzi.

Raia Mwema: Kwa nini hukujiunga rasmi na CCM na badala yake ukaenda CHADEMA?

Nyerere: Kwanza si kosa kujiunga na CHADEMA, na kwa kweli ni kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye Watanzania karibu asilimia 80 walitaka chama kimoja; yeye akashauri mfumo wa vyama vingi uanzishwe kwa sababu maalumu.

Kwa hiyo, nilifuatilia sera na misimamo ya CHADEMA ikaniridhisha kuwa naweza kuwa mwanachama wa chama hicho.

Lakini pia wengi walishangaa wakaanza kusema kuwa nakwenda CHADEMA kuharibu, kufanya kazi ya CCM. Kwamba eti mimi ni mamluki lakini kwa kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele walithibitisha si kweli.

Raia Mwema: Turejee jimboni, hali ikoje jimboni kwako. Kuna vikwazo vyovyote katika kufanya kazi yako, hasa ikizingatiwa ni mbunge wa Upinzani?

Nyerere: Kwanza nikueleze, Musoma Mjini kuna kata 13, CHADEMA tumeshinda kata nane kwa hiyo tunaongoza Halmashauri ya Manispaa.

Mimi mwenyewe mbali na ubunge ni diwani wa kata ya Mkendo; maana wananchi walitaka pia nigombee udiwani. Hii kata ndiyo yenye Ikulu ndogo, ofisi za serikali kama Mkuu wa Mkoa, magereza, polisi na mahakama.

Sasa katika utekelezaji, mwanzo tulipoingia madarakani watendaji wengi wa Halmashauri walituona kama maadui. Na kwa kweli tuligundua matatizo mengi. Kwa mfano, Halmashauri ilikuwa ikidai wafanyabiashara wengi ambao baadhi ni viongozi wakubwa CCM, yumo hadi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM-Taifa (NEC), Gachuma. Tunamdai fedha nyingi kwa muda mrefu na tuko imara kudai fedha hizi kwa wote wanaodaiwa na Halmashauri.

Tumekuwa tukipata hisia kwamba wengine wamekuwa wakifanya siasa ili wapate miradi ndani ya Halmashauri na kufanya mizengwe mingine ya kuikosesha Halmashauri mapato kwa wakati.

Lakini kwa sasa watendaji wengi wa Halmashauri wamegundua kuwa sisi ni wenzao katika kupigania maendeleo ya jimbo na wanatuunga mkono; japo wapo wachache wenye wasiwasi na inawezekana ndiyo waliokuwa wakinufaika na uongozi mbovu uliopita.

Hali ya miundombinu tumeanza kurekebisha, mifereji inazibuliwa na kujengwa, barabara zinafanyiwa kazi na tumeagiza makandarasi wawe wanatoa taarifa kwa mwananchi yeyote atakayewauliza.

Raia Mwema: Wapo wanaosema Mwalimu Nyerere alikuwa mdini, ukiwa ndani ya familia, hili umewahi kulibaini?

Nyerere: Hapana, Mwalimu hakuwahi kuwa mdini na alikuwa mpinzani nambari moja wa udini. Aliamini udini unaweza kuangamiza taifa na ushahidi uko wazi. Leo hii sheria za nchi zinazuia viongozi kuchaguliwa na kuongoza kuzingatia matakwa ya dini zao.

Na sijui alikuwa mdini kwa dini ipi. Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kwenda Libya kwa Gaddafi na akaulizwa apewe msaada gani kwa wanakijiji wenzake Butiama, akitambua kuwa hapakuwa na msikiti bora na mzuri, aliomba fedha za ujenzi wa msikiti na ulijengwa na sasa ndiyo msikiti bora zaidi mkoani Mara.

Kama angekuwa mdini, na hasa kama anapendelea dini yake angeomba fedha za upanuzi wa kanisa au hata ujenzi wa shule kijijini, lakini alijua kijiji si cha Wakristo pekee; bali hata pia Waislamu. Na hata katika elimu, leo kuna maprofesa wamesoma wakati wa Mwalimu Nyerere, tena wakiwa dini tofauti na Mwalimu. Haya ni maneno ya kumchafua, ambayo hata hivyo, wananchi wanaujua ukweli.

Raia Mwema: Nilikuuliza utendaji wako kama mbunge una vikwazo gani jimboni na hata mkoani kwa ujumla na una shauri nini?

Nyerere: Kuna mambo hayapaswi kuendelea na kwa kweli ni lazima tuhakikishe tunatenga shughuli za kiserikali na shughuli za chama. Tuondoe utaratibu wa Mkuu wa Mkoa kuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa au Mkuu wa Wilaya kuwa Mjumbe wa Kamati ya siasa ya CCM. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka ya kiserikali. Chama kifanye shughuli zake na serikali ifanye shughuli zake.

Raia Mwema: Binafsi ndoto yako ni ipi katika mustakabali wa Tanzania?

Nyerere: Kwa kweli ndoto yangu ni siku moja kuona Tanzania yenye uongozi bora zaidi. Naitamani Tanzania ya namna hiyo, yenye uongozi unaoaminika na wananchi wote, usio na mianya ya ufisadi, nchi isiyo na ukatili kati ya raia kwa raia kama mauaji ya albino.

Raia Mwema: Kwa maelezo yako, huridhiki na mwenendo wa uongozi uliopo. Nini tatizo?

Nyerere: Kuna matatizo mengi, sehemu ya uongozi imeanza kumeguka na kusaliti juhudi za Mwalimu Nyerere. Wameingia katika harakati za udini, lakini pia masuala ya msingi kama kilimo bado hayana mpango mahsusi wa kuridhisha. Kilimo kimechukuliwa kama tukio na si mchakato wa kuikomboa nchi. Kilimo ni kama tukio kama kuwa na sikukuu ya Krismasi na ikiishi basi.

Leo kuna kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, lakini tangu utekelezaji uanze bado unasikia maeneo mengi ya nchi yanakumbwa na njaa, wabunge wengi wameomba msaada wa chakula kiende kwenye majimbo yao. Sasa tukiendelea kuchukulia kilimo kama tukio na si mchakato, tunaweza kumaliza Kilimo Kwanza tukawa na Kilimo Mbili, Kilimo Tatu hadi 100, lakini nchi itaendelea kukumbwa na njaa.

Lakini pia kuna suala la uvunaji wa raslimali za nchi kama madini. Uvunaji umekuwa wa ovyo, nchi hainufaiki vya kutosha na vurugu zimekuwa zikitokea maeneo ya migodi.

Raia Mwema: Huoni kwamba wawekezaji wa nje wanasaidia uvunaji ambao tumeshindwa kwa kukosa teknolojia na fedha za kutosha, kama wanavyoeleza viongozi watetezi wa wawekezaji?

Nyerere: Naamini kwanza si kweli hatuna fedha za kununua mitambo ya uchimbaji madini kama ambavyo wawekezaji wa kigeni wamefanya. Kama nchi inaweza kununua ndege za kivita kwa mabilioni au kufanya mambo mengine, ingeweza kufanya uamuzi mgumu kununua mitambo ya kuchimba madini, na kama hatuna raslimali watu wenye taaluma husika tungeweza kukodi menejimenti.

Kwa nini hatufanyi hivyo? Ndiyo maana nasema uongozi bado haujafanya kazi yake vizuri. Na kwa ujumla, hakuna nidhamu katika udhibiti wa raslimali za nchi.

Raia Mwema: Wabunge mnaweza kujadili suala la ‘chenji ya rada’, nini msimamo wako?

Nyerere: Katika suala hili, msimamo ni kwamba watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani kwanza. Hatuwezi kuendelea na mijadala kila kukicha wakati wahusika wakiendelea kubaki mtaani, wakiendelea kugombea nafasi za uongozi, wakiendelea kushika nafasi za uongozi katika vyama vyao na kwa ujumla wakiendelea na maisha ya kawaida kama vile hawakufanya uovu wowote dhidi ya nchi na wananchi. Jambo la muhimu hapa ni kuchukua hatua kwanza.

Raia Mwema: Suala la posho limeanza kuwagawa wabunge wa CHADEMA, John Shibuda, mbunge mwenzenu amepinga wazi wazi. Utata huu unauzungumziaje?

Nyerere: Niseme tu kwamba, kabla ya kujiunga na chama chochote kila mtu anakuwa na malezi yake kisiasa. Hata mimi kabla ya hapo nilikuwa na mambo yangu mengine, lakini unapoamua kujiunga na chama fulani maana yake unakubaliana na msimamo ya kisera na kikatiba na unaposhindwa ni bora kutoka.

Sasa, mimi si msemaji wa chama, na kwa kweli si adui wa Shibuda; bali ni mwenzangu, ni kiongozi mwenzangu, na tunaheshimiana sana, lakini pia mimi ni mtiifu kwa misimamo ya kisera na kikatiba katika chama chetu.

Raia Mwema: Mwanzo umesema ulikuwa shabiki wa CCM, unakizungumziaje chama hicho?

Nyerere: Nadhani wanawajibika kujiweka sawa na kwa kweli inashangaza chama kama hicho kinakuwa na kurugenzi ya propaganda. Kwa wananchi wengi, propaganda ni uongo na kwa hiyo chama kama hicho kinapokuwa na kurugenzi ya propaganda; maana yake ni chama chenye idara maalumu ya kusema uongo kwa jamii. Hili nadhani sio jambo zuri.

Raia Mwema: Umepanga kuendelea na siasa katika maisha yako yote?

Nyerere: Suala la kuendelea katika siasa ni wananchi wenyewe wataamua, hao ndiyo wapiga kura. Wakiamua miaka mitano waliyonipa inayosha basi nitawaheshimu. Na kwa kweli hakuna haja ya kupigania huu ni uamuzi wa wananchi, wapo wenzangu wanasema mimi kijana siwezi kuondoka katika siasa wakati huu, mimi nadhani kuondoka katika siasa si suala la uzee au ujana; bali ni uwezo wa kutumikia wananchi.

Wednesday, July 27, 2011

Mbunge - Wanaosema sisi mzigo wanatudhalilisha

MBUNGE wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (CHADEMA) amelalamikia wabunge wanawake kudhalilishwa bungeni kwa kuitwa kuwa ni mzigo.

Bila kutaja chanzo cha kauli hiyo, Gekul katika swali la nyongeza, amesema, udhalilishaji wa wanawake haufanyiki katika maeneo ya stendi na sokoni, bali hata bungeni ambako alisema walisikika viongozi (bila kutaja majina) wakisema wabunge wanawake ni mzigo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani amesema leo bungeni mjini Dodoma kuwa, katika makosa ya namna hiyo, lazima awepo mlalamikaji.

Ameshauri kwamba, kama wanawake wameona wamedhalilishwa, waungane waende kwenye vyombo vya Dola kushitaki.

“Kama tumeona tumedhalilishwa ni vyema tukaenda kwenye vyombo vya Dola tukashitaki. Siwezi kuamuru kwamba wakamatwe. Kama tunaona tunadhalilishwa tuungane kwa pamoja tupeleke suala hili mahakamani,” amesema Kombani.

Awali, katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Mallac (Chadema), lililoulizwa na Gekul kwa niaba yake, alihoji sababu za sheria zinazodhibiti matusi kushindwa kuchukua mkondo wake kwa watu wanaotoa matusi hadharani.

Amesema, ingawa kutoa matusi hadharani ni kosa, imekuwa ni jambo la kawaida katika maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi hususani wapiga debe, vijiwe vya vijana kuwadhalilisha akinamama na watoto wa kike.

Akijibu swali hilo, Waziri Kombani alisema kutoa matusi hadharani ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi.

Amesema, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za nchi, imeweka makosa ya aina tatu yanayohusu utoaji wa matusi.

Katika kifungu cha 89 cha sheria hiyo inatamkwa kwamba mtu yeyote anayetumia lugha ya kudhalilisha aidha kwa kutamka au kwa ishara dhidi ya mtu yeyote katika hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani, atakuwa ametenda kosa la jinai na anapotiwa hatiani, atatumikia adhabu ya kifungu cha miezi sita jela.

Waziri amesema, katika kifungu cha 135 cha sheria hiyo, inatamka kwamba mtu yeyote atakayemdhalilisha mwenzake kwa kumbughudhi aidha kwa kutumia maneno, sauti au ishara au kitu kitakachoashiria matusi, akipatikana na hatia, atapewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano au kulipa faini ya Sh 300,000 au adhabu zote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Waziri, katika kifungu cha 138D ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kufanya udhalilishaji wa kijinsia kwa mtu mwingine. Akitiwa hatiani, atapewa adhabu ama kifungo miaka mitano au kulipa faini Sh 200,000 au kupewa adhabu zote.

Hata hivyo, amesema, pamoja na makosa yanayohusu lugha ya matusi kuwemo katika sheria za nchi na adhabu zilizopo, bado sheria haiwezi kufanya kazi bila ya mtu aliyetendewa kosa au makosa ya aina hiyo kutoa taarifa kwenye vyombo vya Dola vyenye mamlaka ya kushughulikia makosa hayo.

“Napenda kushauri kwamba ili vyombo vya Dola ziweze kufanya kazi zake ipasavyo, tuwaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye vyombo vya Dola vinavyoshughulikia makosa ya jinai ili waweze kupata haki yao kwa wahalifu kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Waziri Kombani.

Warioba: Umoja wa Watanzania unatetereka

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema hali ya kuvunjika kwa umoja wa Watanzania inayojionesha Tanzania Bara inamwogofya.

Ametoa mfano wa shughuli za kijamii kama maziko zinazofanyika kisiasa kuwa ingawa ni za jamii, lakini vyama vya siasa vinapoingilia, vinasababisha jamii yenye itikadi tofauti kushindwa kushiriki.

Warioba alisema hayo juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV kila Jumatatu na kutoa mfano wa maziko ya diwani wa Shinyanga bila kumtaja jina, ambayo yaliendeshwa kichama.

Maziko hayo ni ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Masekelo katika Manispaa ya Shinyanga, Philipo Shelembi (Chadema), Aprili ambapo Chadema walimzika kichama.

Mbali na Chadema, hata CCM wamekuwa na utaratibu wa kuzika makada wake wakiwamo viongozi waliochaguliwa na wananchi katika nafasi mbalimbali kwa heshima za chama, ikiwemo kufunika jeneza kwa bendera ya chama na watu waliovalia sare za chama kubeba mwili.

Warioba alisema mazishi ni shughuli za kijamii na zinapaswa ziendeshwe kijamii, lakini hali ya sasa ya vyama kuingilia shughuli hizo kisiasa, inasababisha jamii yenye itikadi tofauti ya kisiasa kuacha kushiriki.

“Lazima Watanzania tutafakari, hili ni jambo la hatari katika umoja wetu ni kama ilivyokuwa Zanzibar, watu walisusiana harusi na mazishi, sasa inaanza kuoneka Bara, inaniogopesha,” alisema Warioba.

Alizungumzia tuhuma za udini na kufafanua kuwa zinatolewa na wanasiasa hasa wakati wa uchaguzi, lakini wananchi katika hali yao ya kawaida, wanaishi bila tofauti hizo na kusisitiza umuhimu wa kuweka mambo ya umoja kutochezewa kisiasa.

Pia alitofautiana na mitazamo ya wanasiasa kuita Serikali ya chama; kama CCM wanavyosema kuwa Serikali iliyoko madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi na kuhoji iliko Serikali ya Tanzania.

Alifafanua kuwa, vyama vya siasa ni utaratibu tu wa kuwapa Watanzania viongozi, lakini kiongozi atakayeshinda katika uchaguzi, anaacha kuwa wa chama na badala yake anakuwa wa Watanzania.

Pia alipinga mamlaka ya vyama vya siasa kuadhibu viongozi waliochaguliwa na Watanzania: “Wakati wa mjadala wa Katiba mpya, itabidi Watanzania wajadili madaraka yako wapi? Kwenye vyama au kwa wananchi?” Alihoji.

Alitoa mfano wa uamuzi wa madiwani wa Chadema Arusha kufikia mwafaka na wenzao wa CCM lakini Chadema ikaagiza waachie madaraka; na kusema waliowachagua ni wananchi kwa nini chama kiwanyang’anye madaraka ambayo si ya chama?

Kuhusu kero za Muungano, Warioba alisema walioungana ni Watanzania, lakini itabidi wakati wa mjadala wa Katiba mpya, hilo lijadiliwe kama zilizoungana ni Serikali au Watanzania.

Alitoa mfano wa mambo ambayo viongozi wamekuwa wakisema yaliongezwa katika orodha ya Muungano na kuongeza kwamba ingawa ardhi si sehemu ya mambo ya Muungano, lakini Watanzania wa upande wowote wa Muungano wanaweza kudai ardhi kama haki yao na kuipata.

Alisema hata biashara si jambo la Muungano, lakini Watanzania kutoka upande wowote, wanaweza kudai haki yao ya kufanya biashara sehemu yoyote ya Muungano na kupewa.

Tuesday, July 26, 2011

Maandalizi ya Tamasha la Jinsia 2011

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII TGNP WATAWASILISHA:

MADA: MAANDALIZI YA TAMASHA LA JINSIA 2011

Lini: Jumatano Tarehe 27 Julai, 2011

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo


WOTE MNAKARIBISHWA

TGNP YAGEUKA MKOMBOZI KWA MADIWANI VITI MAALU NAMTUMBO

MADIWANI wanawake viti maalum wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wameanzisha kampeni maalum kupiga vita tabia ya wanaume wa wilaya hiyo ya ukandamizaji wanawake kiuchumi.

Wakazi wa wilaya hiyo ambao hujishughulisha na kilimo cha Tumbaku, wanawake wengi huolewa mitala na kutumikishwa katika kazi za mashambani kuzalisha mazao ya chakula na biashara husasani Tumbaku na kutekelezwa msimu wa mauzo ambapo wanaume hutumia fedha vibaya bila kujali familia na wengine kuongeza kuoa wanawake wasichana.

Madiwani hao ambao hivi karibuni waliainisha vikwazo vya maendeleo ya wanawake na watoto katika wilaya hiyo, walibaini ukandamizwaji kiuchumi unaofanywa na wanaume wa wilaya hiyo unaotokana na mfumo dume.

Kutokana na kubaini hilo umewekwa mpango mkakati wa mwaka mmoja wa kutoa elimu katika ngazi ya familia, kijiji na kuiweka ajenda ya usawa wa kijinsia kuwa ya kudumu katika mikutano yote watakayoshiriki madiwani hao ikiwa ni pamoja na kuyahusisha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutoa elimu hiyo.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hii mara baada ya kumaliza mafunzo yaliyoendeshwa na Mtandao wa Jinsia (TGNP) katika kampeni yao ya haki za uchumi kwa wanawake walio pembezoni, na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi yaliyofanyka mkoan Ruvuma, wamesema mwanamke wa Namtumbo lazima akombolewe.

Diwani Asteria Nchimbi alisema maendeleo ya wilaya hiyo yanakandamizwa na mfumo dume.

“Wanawake ndiyo wanaozalisha mali lakini mapato yote hutumiwa na wanaume,” alilalamika Diwani Nchimbi na kudai watashirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo, Saveri Maketa ambaye ameanza kutoa elimu ya umuhimu wa usawa wa kijinsia na kupanga bajeti kwa ushirikishwaji wa familia.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo Saveri Maketa alikiri kuwa licha ya mapato makubwa ya fedha wanazozipata wananamtumbo kutokana na uzalishaji wa Tumbaku hali ya maisha inabadilika kwa kasi ndogo hasa kutokana na mfumo dume wa maamuzi yote kufanywa na wanaume.

“ Wanawake wanashiriki kazi zote za uzalishaji lakini kunatatizo katika kupanga matumizi ya fedha,” alibainisha Maketa na kuongeza kuwa hivi sasa elimu anayoitoa inaanza kubadili sura za nyumba kuezekwa bati toka nyasi ingawa kwa kasi kidogo.

Imeandaliwa na Juma Nyamayo kutoka Namtumbo Ruvuma ,Nyumayo ni mwanachama wa mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) mikoa ya kusini mwa Tanzania na mwandishi wa gazeti la Habari leo mkoa wa Ruvuma

Rostam amuenzi mjane wa Mwakiteleko

MWENYEKITI wa Bodi ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Rostam Aziz ameahidi kumlipa mjane wa mwanahabari marehemu Danny Mwakiteleko, Winfrida, mshahara aliokuwa akipokea mumewe kwa muda wa miaka mitano.

Aidha, ameahidi kuwalipia ada za shule watoto wawili Carol (13) na Vanessa (11) mpaka
kiwango cha elimu ya juu pamoja na wategemezi wawili wa Mwakiteleko aliowaandika
katika faili lake kazini.

Mwakiteleko, (45), aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Rai na Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), alifariki dunia Jumamosi alfajiri na alisafirishwa jana kwenda kijijini kwao Ndala Mwakaleli wilayani Rungwe, mkoani Mbeya kwa maziko.

Taarifa hiyo ya Rostam ilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Hussein Bashe wakati wa kutoa salamu za rambirambi za kampuni hiyo katikashughuli za kutoa heshima za mwisho zilizofanyika nyumbani kwa marehemu Tabata Chang’ombe
jijini Dar es Salaam.

Alisema Rostam alimtuma kutoa rambirambi hiyo ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo kwa kutambua utendaji kazi wa Mwakiteleko.

Alisema kampuni hiyo itawasomesha hao; mmoja aliyeko kidato cha tatu na mdogo aliye darasa la sita mpaka elimu ya juu.

“Pia Kampuni itagharamia masomo ya wategemezi wawili wa Danny ambao mmoja ni mtoto wa kaka yake ambaye pia ni marehemu; mtoto huyo anasoma shule ya msingi na
mwingine mtoto wa dada wa mke wake anayesoma Stashahada katika Chuo cha Diplomasia,” alisema Bashe.

Alisema marehemu alikuwa na ndoto ya kutoa toleo maalumu la mika 50 ya Uhuru pamoja na miaka 12 ya Tanzania bila Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hivyo watatoa matoleo hayo kumuenzi marehemu aliyekuwa mchapakazi bila kuchoka wala kulazimishwa.

Kabla ya salamu za kampuni hiyo, ibada ilifanyika nyumbani kwa marehemu na kuongozwa na Mchungaji Philemon Kibwana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Tabata Kuu, aliyewataka wafiwa kulia kwa matumaini katika machungu waliyonayo
huku wakiangalia zaidi maisha yao.

Katika msiba huo, Serikali iliwakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi aliyepongeza Jukwaa la Wahariri kwa kuonesha umoja tangu marehemu alipopata ajali hadi katika msiba na kuwatakakuambukiza umoja huo kwa Taifa
zima.

Pia aliipongeza Kampuni ya New Habari (2006) kwa ahadi hiyo kwa familia ya marehemu kwa kuwa katika misiba mingi ni vigumu kusikia waajiri wakizungumzia waliobaki.

Alisema utaratibu huo unasaidia wafanyakazi kufanya kazi kwa juhudi kwani wanaona jinsi mwajiri wao anavyowathamini na kuongeza tija miongoni mwao.

Dk. Nchimbi pia alitoa salamu za pole kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alitamani kuhudhuria mazishi hayo, lakini jana alikuwa katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mkoani Mtwara.

“Rais alitamani sana kuwa pamoja nasi, lakini imeshindikana na Ikulu inafanya utaratibu kuwasilisha ubani kwa familia ya marehemu,” alisema Dk. Nchimbi.

Taasisi na kampuni mbalimbali walitoa salamu zao za rambirambi kwa familia ya marehemu zenye zaidi ya Sh milioni tisa.

Monday, July 25, 2011

Kikwete apunguza maofisa anaosafiri nao nje

RAIS Jakaya Kikwete ameridhia idadi ya maofisa katika ziara zake za nje ipunguzwe ikiwa ni hatua ya kupunguza gharama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliliambia Bunge mwishoni mwa wiki wakati akijibu hoja ya kambi ya upinzani iliyoendelea kutaka safari za nje kwa viongozi zipunguzwe.

Membe alisema katika safari ya hivi karibuni ya Rais Kikwete nchini Shelisheli, idadi ya maofisa alioongozana nao ilikuwa 34 na kwa safari ya Afrika Kusini ilikuwa 34.

Hata hivyo, Waziri Membe alisema wakati mwingine, wingi wa maofisa huzingatia na aina ya ziara na nchi anakokwenda.

Alitoa mfano kwamba, endapo anakwenda nchi ambayo ulinzi wake upo shakani, idadi inaweza kuongezeka.

Alisema, zipo ziara nyingine kama vile za kibiashara inawezekana akalazimika kuongozana na ujumbe wa wafanyabiashara.

Awali, katika kuchangia hotuba ya makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yaliyopitishwa, kambi hiyo ya Upinzani kupitia kwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekia Wenje ilisema safari za viongozi wa juu zinatakiwa ziendane na hali ya uchumi.

Wenje alisema katika dhana ya kupunguza matumizi, baadhi ya safari za nje ambazo siyo lazima mkuu wa nchi kwenda, awaachie viongozi wengine washiriki kwa kuwa msafara wa Rais nje ya nchi una gharama kubwa ikilinganishwa na mawaziri au maofisa wengine wa Serikali.

“Kambi ya Upinzani inaitaka wizara ikishirikiana na ofisi ya Rais kuweka utaratibu wa safari za viongozi nje ya nchi, ili kupunguza matumizi makubwa ya Serikali na hatimaye fedha hizo zielekezwe katika miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Wenje.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikisisitiza kwamba safari za Rais Kikwete nje ya nchi ni zenye manufaa na imekuwa ikitoa mafanikio ya ziara hizo katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa mfano, Marekani ambako Rais Kikwete amekuwa na ziara tangu wakati wa utawala wa Rais George W. Bush na sasa Rais Barack Obama, Tanzania imenufaika kwa kupatiwa fedha nyingi katika miradi ya barabara, umeme, afya na maji.

Friday, July 22, 2011

SHAIRI LA BAJETI

Na Bi. Subira Kibiga
TGNP

Karibuni karibuni, tuijadili Bajeti
Hotuba imewasili,bungeni kuisapoti
Tuisome kwa makini, hoja tuzijengeni
Bajeti imsbani, aliyekufa ni nani?

Bajeti imsibani, aliyekufa ni nani
Kila siku matangani marehemu hatoki ndani,
Vijana wako sandani,wazee makaburini
Bajeti imsibani,aliyekufa ni nani?

Bajeti inamlenga nani,umaskini ndio ilani
Takwimu ulipata wapi,hata usome bungeni
Sisi twakushangaeni,wananchi hali ya chini,
Bajeti imsibani, aliyekufa ni nani?

Ajira ndio msingi, bajetini hatuoni
Nimeongeza vitini,vya vikoba mitaani
Na mikopo ya mitaani,ufilisi majumbani
Bajeti imsibani aliyekufa ni nani?

Hamkuweza kuthamini,makundi ya pembezoni
Mkulima habadiliki, kila siku wa zamani
Jembe lake mkononi,trekta aweze nani
Bajeti imsibani aliye kufa ni nani?

Elimu ni mtihani, kwa asilimia Fulani
Watoto wa mashakani, mazingira hayafanani
Wajisomea njiani, usafiri awape nani
Bajeti imsibani, aliyekufa ni nani?

Hotuba tuisomeni, kisha tuichambueni
Inaleta tija gani, kwa makundi pembezoni
Kijana wa kijiweni,au mzee wa maskani
Bajeti imsibani aliyekufa ni nani?

Bajeti ni muhimili, kwetu sisi maishani
Mipango si matumizi,ndio iliyoko bungeni
Hotuba tuisomeni, pesa hazionekani
Bajeti imsibani aliyekufa ni nani?

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Nishati na Madini Inaaibisha Taifa na Watanzania

Sisi Muungano wa Asasi za Kiraia zinazotetea Usawa wa jinsia, haki za binadamu, demokrasia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) tumepokea kwa mshtuko, mshangao na masikitiko makubwa, tuhuma kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Madini na Nishati, ameandaa mpango mahususi wa kukusanya pesa kutoka idara na wakala walio chini ya wizara yake, kwa ajili ya kuhonga Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

Kwetu sisi wanaharakati, kitendo hiki ni ishara ya mambo makubwa zaidi yanayofanywa na baadhi ya viongozi wetu yanayosababisha kuendeleza ufukara na umaskini wa taifa letu na watu wake.

Kama tuhuma hizi ni za kweli, ni wazi kuwa mikakati mingine kama huu haikuanza mwaka huu, na hauwezi kuwa mkakati wa Wizara ya Madini na Nishati pekee. Na kama hivyo ndivyo, basi Serikali ya Tanzania yote inanuka rushwa, na haina uhalali wa kuendelea kuongoza nchi, Serikali na Watanzania.

Hali hii inatufanya tuzidi kuamini kuwa Serikali inayoghubikwa na kuendeshwa kwa mfumo wa kuhongana miongoni mwa viongozi na watendaji wenye mamlaka ya kufanya maamuzi katika mihimili mikuu ya dola, ni Serikali ya hatari na isiyostahili kuendelea kuwa madarakani. Serikali ya namna hii haiwezi kuwa na utashi wa kutumikia matakwa ya wananchi, isipokuwa kununuliwa na mafisadi.

Uchambuzi yakinifu wa bajeti tunaofanya mara kwa mara sisi wanaharakati unatuonesha jinsi gani rasilimali za taifa hili zinavyoendelea kufaidisha wachache na kudumisha ufukara kwa wengi. Wanaharakati wa FemAct tunasema kwamba tatizo hili ni kubwa na lisiishie tu kwenye kuwaadhibu waliyohusika na rushwa ya kupitisha bajeti. Tatizo ni pana zaidi na linahitaji tafakari pana ya kimfumo.

Tatizo la Umeme


Tatizo la umeme sio la leo, ni suala ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu, Serikali imekosa mbinu na mikakati sahihi hadi kufikia hatua ya kutaka kubinafsisha Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco). Mikataba mingi michafu imeingiwa na Serikali kwa kutumia makampuni makubwa ya nje kama IPTL, Agreco, Songas, Richmond, Dowans na NetGroup Solutions. Hakika mbinu chafu zisingezaa matunda mema; tatizo la kukosa umeme limeongezeka mara dufu na wakati wote huu mwananchi masikini anaendelea kuteseka licha ya kulipia gharama zote anazobebeshwa na viongozi waongo na wanaokubali kuhongwa.

Lakini katika mazingira haya ya rushwa, utapeli na ufisadi, Serikali imekosa utashi wa kushughulikia tatizo la umeme kwa kuzingatia mipango ya muda mrefu kama Miradi ya Makaa ya Mawe, Mchuchuma , Ngaka na Kiwira, ambavyo kwa pamoja ina uwezo wa kuzalisha megawati 1500 za nishati ya umeme ambayo inatosha kumaliza tatizo lililopo kwa takribani miaka mingi ijayo.

Inashangaza kuona taifa lenye rasilimali nyingi na miaka 50 baada ya uhuru likizalisha megawati 1034, wakati vyanzo vitatu vilivyotajwa hapo juu vingezalisha megawati 1500.

Mbali na mradi wa Mchuchuma, maporomoko ya mto Rufiji ya Stgiler’s Gorge, yana uwezo wa kuzalisha megawati zaidi ya 2,000 za umeme wa gharama nafuu. Lakini kila mwaka tunasikia ahadi kuwa mradi huu utaanza bila mafanikio matokeo yake tumeendelea kung’ang’ania kukodisha majenereta kutoka Ulaya na Marekani ambayo baada ya muda mfupi hushindwa kufanya kazi wakati mwingine kutuingiza kwenye mikataba michafu ya kifisadi.

Umeme kwa ajili ya nani?

FemAct tunataka kuona umeme ukiwa ni nishati muhimu kwa kila raia wa taifa hili, masikini wa kijijini na wa mjini, unaopatikana na kwa bei ambayo inaruhusu kila mwananchi anaweza kumudu gharama zake.

Ingawaje Tanzania ina utajiri mkubwa wa vyanzo vya nishati kama vile gesimoto(geothermal) nishati ya jua na upepo, pamoja na mkaa wa mawe, takribani asili mia 39% ya wakazi wa mijini na asili mia 2% tu ya wakazi wa vijijini wenye kufikiwa na umeme. Asilimia 10 ya kaya zote ndizo zinapata umeme kwa kupitia gridi ya taifa, na 1% tu ya kaya zote za Tanzania zinauwezo wa kutumia umeme kwa ajili ya kupikia. Wakati tukidai kwamba taifa limekumbwa na dharura kuwa gizani takribani nusu mwaka sasa, asili mia kubwa ya watanzania wako kwenye hali hii ya hatari takribani miaka hamsini tangia tupate uhuru.

Iweje, miaka hamsini tangu tupate uhuru Taifa liko gizani? Iweje wazalishaji wakuu wa chakula, mazao ya biashara na walezi wa watoto wa taifa hili wawe kwenye giza kuu tangu bendera ya mkoloni kushushwa na kupandishwa kwa bendera ya Taifa huru? Iweje asili mia sabini hadi tisini ya Watanzania wamekuwa wakitegema aidha mkaa au kuni kwa ajili ya kupata nishati ya matumizi ya kaya? Matokeo yake yameendelea kuwa mzigo mkubwa wa wanawake wazee kutafuta na kubeba kuni, kupikia kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe huku wakikumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kutokana na macho yao kuwa mekundu.

Kwanini serikali itoe rushwa?
FemAct inaamini kuwa kuna sababu nyingine inayolazimisha Serikali kujaribu kutoa rushwa ili kupitisha bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati ni mfumo mzima wa mikataba, uwekezaji, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za madini na gesi asilia hapa nchini ambao hauna uwajibikaji; na uwazi wake una mashaka na hivyo kuhalalisha vitendo vya rushwa na ufisadi. Watanzania hawanufaiki na madini na gesi asilia kutoka nchini mwao. Kuna migogoro mingi katika maeneo yanakochimbwa madini na gesi asilia baada ya wananchi kugundua ulaghai unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali kwa kushirikiana na wawekezaji katika migodi ya madini na visima vya gesi asilia.
Kutokana na masuala yaliyoorodheshwa hapo juu, FemAct inataka Serikali ifanye marekebisho haraka kukidhi haja ya madai yafuatayo:-

1. Katibu Mkuu,Waziri ,Naibu wake kwa pamoja na watendaji wengine waliohusika kuchangisha fedha za kuwahonga wabunge waondolewe kazini na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria haraka. Matendo yao ni kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.


2. Tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awafute kazi watendaji hao mara moja na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe mfano kwa wahalifu wengine waliojificha katika ajira za Serikali.


3. Katika marekebisho ya bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati Serikali ilete mikakati sahihi ya kulimaliza tatizo la umeme nchini. Serikali itaje vyanzo mbadala vya kuaminika vya kuzalisha umeme na sio kukodisha majenereta na kujiingiza kwenye mikataba ya kifisadi.


4. Serikali ieleze hatua thabiti inazozichukua kuhakikisha vyanzo vya umeme wa upepo, nguvu ya jua,makaa ya mawe,maporomoko ya mto Rufiji, yanatumika ipasavyo kuzalisha umeme badala ya kuingia mikataba na makampuni ya kitapeli na kutegemea umeme wa mvua.


5. Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ieleze sababu za kushindwa kugundua mapungufu katika bajeti hiyo mapema na kuirudisha serikalini badala ya kupoteza muda wa umma.


6. Serikali ielekeze nguvu ya kufikisha umeme kwa wananchi wa vijijini na kwa bei rahisi ili kuongeza tija katika uzalishaji hasa kupitia kilimo na kuongeza ari ya kuanizishwa kwa viwanda vya kusindika mazao vijijini.


7. Serikali iwe wazi katika shughuli zake zote, hususan, mikataba ya madini, kufua umeme na kuzidua gesi asilia.


8. Serikali iunde tume huru kuchunguza mauaji ya hivi karibuni huko Nyamongo Mara na hii itamkwe ndani ya bajeti kwamba serikali itawalinda wananchi wake waishio jirani na migodi kwa mali zao na usalama wao. Vile vile serikali itoe tamko hatima ya mgodi wa Buhemba.


9. Serikali iweke wazi mikataba yote ya madini iliyopo ili kutoa fursa kwa umma kudadisi ikiwa ina maslahi kwa taifa. Zoezi la kuweka mikataba yote ya madini hadharani ni muhimu sana kuliko kuendelea kuvutia wawekezaji wapya katika sekta za nishati na madini ambazo zimeghubikwa na kashfa za ufisadi na uzembe.



Imetolewa Dar es salaam na:

Usu Mallya
Kny Sekretarieti ya Femact

Jairo apelekwa likizo, CAG kumchunguza

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, amepewa likizo kuanzia leo ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili na kupata ukweli kabla ya hatua zingine kuchukuliwa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, alisema jana mjini Dodoma kwamba, yeye ndiye mwenye mamlaka ya nidhamu na kwa kuwa tuhuma zinazomhusu Jairo ni za fedha, amemteua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kumpa siku 10 afanye uchunguzi wa awali.

Luhanjo alisema, ndani ya siku kati ya mbili na tatu, atakuwa amemteua mtu wa kukaimu nafasi hiyo, wakati Jairo akiwa katika likizo hiyo ambayo ni ya malipo. “Siku mbili, tatu mtasikia nani nimemteua,” alisema Luhanjo.

Katibu Mkuu Kiongozi alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na kusema tuhuma dhidi ya Jairo ni nzito hali ambayo imemlazimu kuamua aende likizo licha ya kwamba Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, inaruhusu mtuhumiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa.

Kwa mujibu wa Luhanjo, tuhuma zinazochunguzwa ni zilizotolewa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini.

Baadhi yao ni pamoja na kuzitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo, zichangie Sh milioni 50 kila moja, ili fedha hizo zitumike kulipa wabunge na kufanikisha mawasilisho ya makadirio hayo.

Tuhuma zingine ni za kulipa masurufu ya safari watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walishalipwa na wizara na taasisi hizo.

“Hataendelea na kazi kipindi cha uchunguzi. Hatua zaidi zitategemea uchunguzi huo wa awali… nimeamua niseme, msianze kubashiri, kwamba tunamsubiri Rais aliyemteua, mimi ndiye mwenye mamlaka … nikipata taarifa ya uchunguzi wa awali, nitampa notisi ya matokeo ya awali,” Luhanjo aliwaambia waandishi wa habari.

Uamuzi wa kusisitiza kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka, unatokana na vyombo vya habari jana kuchapisha taarifa zikimkariri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa uamuzi juu ya Jairo unamsubiri Rais Jakaya Kikwete.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari ambao Luhanjo alifuatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo na waandishi wa Waziri Mkuu, Luhanjo alitoa somo kwa waandishi wa habari juu ya utaratibu wa kushughulikia tuhuma dhidi ya mtumishi wa umma.

Luhanjo alisema kulingana na Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, mwenye mamlaka ya nidhamu kwa mtumishi yeyote wa umma anayetuliwa na Rais kasoro wanasiasa, mawaziri na wakuu wa mikoa, ni Katibu Mkuu Kiongozi.

Alisema katika kushughulikia tuhuma zinazomkabili mtumishi wa umma, lazima uchunguzi wa awali ufanyike kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, ili kubaini kama mtumishi husika ametenda kosa la kinidhamu.

“Katika kipindi cha uchunguzi, mtumishi anayetuhumiwa, anaweza kupewa likizo ya malipo ili kupisha shughuli za uchunguzi au akaruhusiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa,” alisema Luhanjo.

Alifafanua kwamba kama uchunguzi wa awali dhidi ya Jairo, utabaini makosa ya kinidhamu, Mamlaka ya Nidhamu itampa taarifa za tuhuma ambazo zitaambatana na hati ya nashitaka, itakayoelezea kwa ufupi kosa alilotenda na ni lini anapaswa awe amejibu tuhuma husika. Mtuhumiwa anapaswa asimamishwe kazi na kulipwa nusu mshahara.

“Mtuhumiwa atatoa maelezo yake kwa mujibu wa hati ya mashitaka aliyopewa. Anaweza kukataa au kukubali. Akikubali, Mamlaka ya Nidhamu itaendelea kutoa adhabu kulingana na uzito wa kosa. Adhabu inaweza kuwa kufukuzwa kazi, kupunguzwa cheo au kupunguzwa mshahara ama adhabu nyingine iliyoelekezwa na Sheria ya Utumishi wa Umma.

“Iwapo atakana mashitaka, Mamlaka ya Nidhamu itaunda Kamati ya Uchunguzi itakayopewa hadidu za rejea ambazo pamoja na mambo mengine, zitaeleza muda wa uchunguzi huo kukamilika. Taarifa ya kamati itawasilishwa kwa Mamlaka hiyo, ikiwa na mapendekezo.

Ikumbukwe kuwa Kamati hii haitoi adhabu kwa mtuhumiwa isipokuwa inatoa mapendekezo tu,” Luhanjo alisisitiza. Baada ya taarifa ya kamati ya uchunguzi, Luhanjo alisema Mamlaka itaendelea kutoa adhabu kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo. Kama adhabu itakuwa ni kuvuliwa madaraka, Mamlaka ya Nidhamu itawasiliana na Mamlaka ya Uteuzi kuhusu kutekeleza suala hilo.

Hata hivyo, Luhanjo alisema iwapo mtuhumiwa hajaridhika na uamuzi unaoishia kwa Mamlaka ya Nidhamu, sheria zinampa fursa ya kukata rufaa kwa Rais. “Rais ana mamlaka ya kuthibitisha au kukataa uamuzi wa Mamlaka ya Nidhamu,” alisema.

Tuhuma dhidi ya Jairo ziliibuliwa Julai 18 bungeni na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM). Jana katika maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF) alihoji sababu za uamuzi wa kumwajibisha Jairo kumsubiri Rais Kikwete wakati yupo Makamu wa Rais anayefanya kazi kwa niaba yake.

Mbunge huyo alisema kufanya hivyo ni kinyume na Katiba ambayo katika Kifungu cha 47 (1) (c) ana mamlaka ya kufanya kazi zote za Rais anapokuwa amesafiri nje ya nchi. “Ulitoa kauli bungeni kwamba huna mamlaka ya kumwajibisha Katibu Mkuu, unamsubiri Rais. Je huoni kwa kufanya hivyo umekiuka kanuni za Katiba?” alihoji Abdallah.

Akijibu, Pinda alisema kulingana na Katiba, si kila jambo wanaopewa dhamana wanapaswa kutoa uamuzi.

Alisema pamoja na kwamba Katiba inaelekeza pia Waziri Mkuu kupewa mamlaka iwapo Makamu wa Rais hayupo, wana kikomo cha madaraka. “Tusitafsiri kipengele hiki kwamba Rais akiondoka ndio sasa umepewa unga,” alisema Pinda.

Pinda aliwaambia wabunge kuwa suala hilo angeliwasilisha kwa Rais Kikwete aliyekuwa ziarani Afrika Kusini kwa kile alichosema ndiye mwenye uamuzi, kwa kuwa ndiye aliyemteua.

Juzi Waziri Mkuu akawaambia tena waandishi wa habari kuwa alipowasiliana na Rais, alimwambia asubiri arejee nchini ndipo uamuzi utolewe kuhusu sakata hilo.

Thursday, July 21, 2011

Wanafunzi 56 wazuiwa kurudi UDOM

WANAFUNZI wa Shahada za awali wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Kompyuta, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CIVE) katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliosimamishwa masomo kwa muda usiojulikana takribani miezi mitatu iliyopita, wameitwa chuoni.

Wanafunzi 56 kati ya waliosimamishwa wamezuiwa kurudi chuoni.

Taarifa iliyotolewa juzi katika tovuti ya chuo, imetaja majina ya wanafunzi 56 ambao wote ni wavulana wasiotakiwa kurudi chuoni na kusema kwamba, watapewa taarifa zao binafsi na mamlaka husika.

Kwa upande wa wanafunzi walioruhusiwa kurudi, uongozi wa chuo umewabana kwa kuwapa masharti kadhaa miongoni mwake ikiwa ni kwamba walitakiwa kurudi chuoni na kufanya usajili upya Julai 7 mwaka huu kabla ya masomo kuanza Agosti Mosi mwaka huu.

Masharti mengine waliyopewa wanafunzi hao ni kwamba wale wanaodaiwa ada, gharama za malazi, mitihani na gharama nyingine, ni lazima walipe madeni hayo kabla ya kurudi chuoni.

Pia kila mwanafunzi anatakiwa kulipa gharama za usajili Sh 10,000 na wameamriwa malipo yote yafanyike kabla ya Julai 23 kupitia akaunti za chuo zilizo mjini Dodoma.

Kila mwanafunzi anatakiwa aape kwa wakili kiapo cha utii wa Sheria Ndogondogo za wanafunzi wa UDOM na za nchi.

“Kiapo kibandikwe picha mbili; moja ya mzazi au mlezi wa mwanafunzi na moja ya mwanafunzi mhusika. Mwanafunzi atakayekiuka kiapo chake atafukuzwa chuo mara moja,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na ofisi ya Makamu wa Chuo.

Chuo hicho kilifungwa Aprili mwaka huu baada ya kukumbwa na mgogoro kati ya wanafunzi na Menejimenti.

Uongozi ulichukua hatua hiyo kutokana na hali ya usalama kuwa tete baada ya wanafunzi 27 kusimamishwa masomo hali iliyowafanya wanafunzi wengine kuandamana wakidai wenzao warudishwe.

Chanzo halisi cha ilikuwa ni maandamano yaliyofanywa na wanafunzi hao kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, mjini Dodoma wakidai wapewe fedha za mafunzo ya vitendo na vitendea kazi zikiwemo kompyuta walizodai kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika ziara yake ya Januari mwaka huu, alishauri wapewe.

Madaktari bingwa kufanya upasuaji bure

JOPO la madaktari bingwa tisa kutoka Shirika la Interplast la Ujerumani linatarajiwa kuendesha huduma za upasuaji wa kurekebisha sura na maumbile kwa wakazi wa mkoa wa Tanga wenye matatizo hayo.

Huduma hiyo itatolewa bure kwa siku 15 mfululizo kuanzia Julai 31 hadi Agosti 14 mwaka huu kwa kuhusisha madaktari hao watakaoshirikiana na madaktari wengine wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Tanga jana, mratibu wa upasuaji huo, Dk. Wallace Karata alisema utahusisha midomo iliyopasuka, kaa kaa lililopasuka, makovu sugu yanayozuia muonekano na utendaji kazi wa viungo mbalimbali pamoja na uvimbe mwilini.

Dk. Karata alisema, matibabu hayo yatatolewa bure kwa kuwa shirika hilo limegharamia vitu vyote muhimu kwa ajili ya kufanikisha matibabu hayo isipokuwa gharama za usajili wa mgonjwa pamoja na kulazwa.

“Kwa mara ya nne sasa shirika hilo litaleta jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha viungo mbalimbali hapa mkoani kwetu Tanga, tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi tena mwaka huu kwa kuwa matibabu yatatolewa bure.

“Kila mgonjwa atachangia Sh 1,000 ya kusajili kadi pale hospitali ya Bombo,” alisema na kuongeza kuwa kwa wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji mkubwa, watalazimika kuendelea kupata matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.

Tangu kuanza kutolewa kwa matibabu hayo kwenye Mkoa wa Tanga, mwaka 2008 hadi mwaka jana tayari wagonjwa 119 wamefanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbile yao huku wengi wao wakiwa ni watu wazima.

Wednesday, July 20, 2011

Posho elimu ya juu yapanda kwa Sh 2,500/-

SERIKALI itaongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutoka Sh. 5,000 ya sasa hadi Sh. 7,500 katika mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka huu.

Alisema, kiasi cha Sh. bilioni 77.8 kitatumika kwa suala hilo na wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo na kwa wanaosoma shahada za uzamili na uzamivu, wanatarajiwa kupewa mikopo kwa mwaka 2011/12.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) itaimarisha utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa kuainisha taarifa za wakopeshwaji na zile za Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Mitihani na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

Alisema pia Bodi hiyo itasogeza huduma za utoaji mikopo karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi ya kanda Zanzibar.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu wizara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta , alisema ili kuimarisha uwezo wa Serikali kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi, Kamati yake ilishauri Serikali itafute mbinu mbadala za kupata fedha ili kuinua uwezo wa kutoa mikopo mwaka hadi mwaka.

Alisema, ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2006, kiundwe chombo mahususi chini ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ili kufuatilia ukusanywaji wa marejesho ya mikopo iliyokwishatolewa.

Alisema, taarifa za mikopo husika zitambulike kwa walengwa ili kurahisisha ukusanyaji wa fedha hizo kwa ushirikiano wa mwajiri na Bodi ya Mikopo na kuwa fedha za marejesho ya mikopo hiyo zitambulike bayana, kwa kuonekana katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu kila mwaka.

Pia Kamati ilishauri utoaji vitambulisho vya Taifa ukamilike ili kutambua wanafunzi wanaokopa na waliokopa na uraia wao, ambapo pia Kamati ilishauri kuwapo udhibiti wa karo hasa katika vyuo visivyo vya Serikali.

Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM), alishauri kutokana na utata katika urejeshwaji wa mikopo, Serikali itoe fedha hizo bure kwa wanafunzi badala ya kuwakopesha.

Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo kwa Wizara ya hiyo Cristowaja Mtinda, alisema kutokana na muundo wa Bodi ya Mikopo na uendeshaji mbaya, kuna haja ikavunjwa kwani imeshindwa kuifanya elimu ya juu ipatikane kwa kila mwanafunzi anayestahili.

Alisema Bodi hiyo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 mwaka uliopita, lakini ilikusanya marejesho ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.9 kati ya Sh. bilioni 21 zilizotarajiwa kukusanywa.

“Kutokana na sababu hizo, Serikali iazimie kuivunja Bodi hii, pamoja na kufanya uchunguzi huru wa fedha zilizotumika chini yake hadi sasa na kujiridhisha kama waliopewa dhamana hii hawakutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi,” alisema.

Alisema baada ya Bodi hiyo kuvunjwa, Serikali iunde chombo kipya kitakachojulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (TAHEFA), ambacho kitachukua majukumu yote ya Bodi.

Mahakama yaamuru IPTL ifilisiwe

MAHAKAMA Kuu Tanzania imetoa amri ya kuifilisi Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Mahakama imeagiza kuwa, kazi hiyo ya kuifilisi IPTL ifanywe na mfilisi wa kampuni hiyo ambaye ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Uamuzi huo ulitolewa rasmi wiki iliyopita na Jaji wa mahakama hiyo, Semistocles Kaijage katika kesi ya madai namba 254 ya mwaka 2003 iliyofunguliwa na kampuni ya Vip Engineering and Marketing Ltd dhidi ya IPTL, Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad na Mfilisi.

Jaji Kaijage alisema, kutokana na ombi lililowasilishwa na Kampuni ya Vip Engineering and Marketing Ltd ambaye ni mmoja wa mshirika wa IPTL Februari 25, mwaka 2002 na baada ya kuwasikia mawakili wake kwa njia ya maandishi na ombi hilo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Oktoba 10, mwaka 2003, aliamuru kampuni hiyo ifilisiwe.

Mawakili wa Vip Engineering and Marketing Ltd ni pamoja na Michael Ngalo wa Kampuni ya Mawakili ya Ngalo and Company, Respicius Didace wa Kampuni ya Mawakili ya Didace and Company na Dosca Baregu kutoka Kampuni ya Mawakili ya Mutabuzi & Company.

“Mahakama hii inaamuru ifilisiwe kwa mujibu wa kanuni na kazi hiyo ifanywe na mfilisi anayeshughulika na masuala ya IPTL,” alisema Jaji Kaijage.

Aidha, aliamuru mfilisi huyo ambaye ni Rita kwa kushirikiana na wadau wa IPTL kutumia kampuni inayotambulika katika shughuli za ukaguzi wa umma kuchunguza mali za IPTL, madeni yake na kama kuna tuhuma za rushwa na kisha kutoa ripoti hiyo kwa Mahakama Kuu.

Akizungumza na blog hii jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Philip Saliboko alikiri kuwa Mahakama imewaagiza kuifilisi Rita, lakini bado wakala hao hawajapokea barua ya maagizo hayo rasmi kutoka Mahakama Kuu na kwamba, wanasubiri.

“Ni kweli sisi kama wafilisi wa IPTL tumetakiwa tufanye kazi hiyo ya kuifililisi lakini kwa sasa hatujaanza hatua yeyote kwa kuwa bado hatujapata taarifa rasmi za maagizo kutoka Mahakama Kuu,” alisema.

Alisema, iwapo watapatiwa barua na maagizo hayo rasmi, wataanza kwanza na kujitangaza kwenye vyombo vya habari ili wale wote wanaoidai au kudaiwa na IPTL wajitokeze wakiwa na ushahidi wao kwa Rita ambapo pia watatangaza zabuni kwa kampuni itakayochunguza kila kitu kuanzia gharama, madeni na madai ya IPTL.

Ngeleja, Malima watakiwa kujiuzulu

MBUNGE wa Arusha, Godbless Lema (CHADEMA) jana aliomba Mwongozo wa Spika akitaka Waziri na Naibu Waziri wa Nishati na Madini wawajibike katika sakata la wizara hiyo kuchangisha Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa Bajeti.

Lema aliomba Mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 68(7) kwa kusema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, asingeweza kuwa na ujasiri wa kuchangisha fedha hizo bila mawaziri husika kuwa na taarifa.

Mbunge huyo ambaye alitaja moja kwa moja bungeni kwamba Katibu Mkuu huyo alijihusisha katika vitendo vya rushwa kutokana na fedha hizo, alihoji kama kweli ndiye anapaswa kuwajibika pekee na si pamoja na Waziri mwenye dhamana, William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima.

Spika Anne Makinda hakukubaliana na hoja ya Lema kutokana na kile alichosema kwamba mjadala wa suala hilo umewekwa pembeni kutokana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuliomba Bunge juzi kwamba anakwenda kulifanyia kazi. “Naomba waendelee kufanya inavyostahili kiutawala,” alisema Makinda.

Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), ndiye aliyeibua hilo sakata wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kabla haijaondolewa bungeni juzi.

Shelukindo aliwasilisha barua bungeni iliyoandikwa na Katibu Mkuu Jairo ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo kila moja ichangie Sh milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.

Mbunge huyo wa Kilindi pamoja na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.

Pinda katika hoja yake bungeni alikiri kwamba Jairo kawaudhi na kuwatibua wabunge na akaahidi kuwasilisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete aliyemteua ili achukuliwe hatua.

“Lazima nikiri hata mimi nilishtuka kweli sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi hakuna namna ya kutetea,” alisema Pinda.

Wakati huo huo, baadhi ya wadau wa umeme nchini wamewatupia lawama watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa ndiyo chanzo cha matatizo ya umeme kutokana na kutotekeleza kivitendo, mipango ambayo ingesaidia kuondokana na tatizo hilo.

Watendaji hao pia wameshutumiwa kuwa mabingwa wa kupiga maneno na kufanya ujanjaujanja katika kushughulikia tatizo la umeme.

Pia wameshutumiwa kuwa wanapuuzia mchango wa sekta binafsi wakati ndio watumiaji wakubwa wa umeme.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema kinachokosekana kwa watendaji hao ni akili na ubunifu, badala yake alisema wanatanguliza ujanjaujanja na ni werevu wa kupiga maneno.

“Tatizo letu tunakwepa kuwatumia wataalamu katika masuala haya; badala yake tunawatanguliza wachekeshaji na wapiga porojo … katika hali ya namna hii, kamwe hatuwezi kuondokana na tatizo la umeme,” alisema Dk Semboja. Alisema kwa sasa suala si fedha bali ni akili ya kubuni mikakati ya kuondokana na tatizo hilo kama walivyofanya Kenya na Ethiopia.

“Kama suala ni fedha, Tanesco wanahitaji bajeti ya miaka 20 ijayo, kumaliza tatizo la umeme, lakini sasa tunahitaji ubunifu na akili.” Alitoa mfano kuwa ndani ya Tanesco na Serikali kuna wataalamu ambao wameshirikishwa katika mipango inayohusisha ushiriki wa jumuiya za kanda kama ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) na ile ya Bonde la Mto Nile, lakini utekelezaji wake kwa Tanzania hautiliwi maanani.

“Mimi nimekuwa nashiriki miradi yote hiyo, lakini ushiriki wa Serikali yetu ni mbovu, ndiyo maana nasema tuna watu wenye uwezo, watafutwe tuachane na hawa wachekeshaji na wapiga maneno,” alisema Dk Semboja. Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Felix Mosha, alisema Tanzania itaondokana na tatizo la umeme iwapo wataishirikisha sekta binafsi katika mipango yake.

Mosha alisema asilimia 85 ya watumiaji wakubwa wa umeme wa Tanesco ni wenye viwanda, hivyo alishauri Serikali kuwa inapaswa kuwahusisha katika mipango yote kuanzia ya muda mfupi, kati na mrefu ili nao watoe maoni yao ya namna ya kuondokana na tatizo hili. Alisema matatizo haya yanayoendelea ya mgawo wa umeme ni matokeo ya Serikali kuidharau sekta binafsi hasa kwenye suala la umeme.

“Hata pale jambo linalogusa sekta binafsi, Serikali haitaki majadiliano nasi na badala yake wamekuwa wanajadiliana wenyewe na kuamua mambo yao.” Mosha alisema: “Naamini kukwama kwa bajeti hii sasa itatoa fursa ya kutushirikisha, na sisi tuko tayari, kwani tuna mapendekezo yetu ambayo tutawapatia watu wa Serikali.”

Alisema, kama Serikali itaendelea kuwapuuza, ustawi wa viwanda nchini uko katika hatihati, kwani vingi vinategemea jenereta ambazo zilikuwa maalumu kutatua tatizo la muda mfupi na si ilivyo sasa kutokana na gharama zake kuwa juu kuliko umeme.

Mwenyekiti huyo pia alisema katika hali ya sasa, viwanda vya Tanzania havina ubavu wa kushindana na vya nchi zingine za nchi wanachama wa EAC kutokana na kutokuwa na nishati ya uhakika.

Alionya pia kuwa watu wengi watapoteza ajira, kwani viwanda vingi vinafanya kazi kwa siku mbili kwa wiki jambo ambalo linamwia vigumu mwajiri.

Tuesday, July 19, 2011

Makadirio ya Ngeleja yakwama, apewa wiki tatu

MAKADIRIO ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/12 imekwama na hivyo kuahirishwa baada ya wabunge kuigomea.

Imeahirishwa kwa wiki tatu kutokana na ombi lililowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Hii ni mara ya kwanza kwa Makadirio ya Serikali kukataliwa bungeni wakati wa mjadala, ingawa huko nyuma makadirio hayo yalikwama katika ngazi ya Kamati za Kudumu za Bunge.

Kwa mujibu wa Pinda, Serikali itahakikisha inashirikisha Kamati ili yatakaporudishwa bungeni, makadirio hayo yajibu matakwa ya wabunge na yawe yanayotekelezeka hususan katika kukabili tatizo la umeme linaloonekana kukera zaidi wawakilishi hao wa wananchi kwa jumla.

Baada ya Pinda kutamka hoja hiyo iahirishwe, ukumbi wa Bunge uliokuwa umesheheni tofauti na siku zingine, ulilipuka kwa makofi na vigelegele, bila kujali itikadi za vyama ingawa zilisikika baadhi ya sauti kupitia vipaza sauti zikisema, ‘CCM, CCM na wengine wakisema ‘Peoples Power (Nguvu ya umma)’ ambayo ni salamu ya Chadema.

Kuhusu suala la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Pinda alisema, “ni kweli kawaudhi, kawatibua kweli. Lazima nikiri hata mimi nilishituka kweli sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi, hakuna namna ya kutetea.”

Aliendelea kusema: “kikwazo pekee ni kwamba Rais hajatua Afrika Kusini na ndiye mwenye mamlaka ya kuteua makatibu wakuu. Nikisema mimi nichukue uamuzi nitakuwa naingilia maeneo yasiyo yangu. Mnipe Baraka, akifika leo nitawasilisha haya kwake.”

Spika wa Bunge, Anne Makinda akiunga mkono uamuzi wa kuahirisha makadirio hayo, alisema suala la umeme limevuta hisia za Watanzania wengi.

“Nakubali hoja ya wiki tatu wajipange vizuri Serikali ije na kitu kinachotekelezeka na kinacholeta matumaini kwa Watanzania. Kamati ya Uongozi itapanga tarehe,” alisema Spika Makinda na kutangaza kikao cha Kamati ya Uongozi kukutana jana kupanga tarehe mpya.

Akizungumza nje ya Bunge baada ya kuahirishwa kwa hoja yake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema anakubaliana na michango ya wabunge, na kwamba hali hii ya umeme, inatokana na fedha kidogo zilizotengewa Wizara hiyo.

Hali ilianza kuwa mbaya katika michango ya jana asubuhi, wakati ilipoelezwa kuwa Wizara imechangisha takribani Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake ili kufanikisha uwasilishaji wa makadirio ya matumizi yake bungeni.

Alikuwa Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), wakati akichangia mjadala huo, aliwasilisha barua bungeni inayodaiwa kuwa iliandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara, David Jairo, ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo zichangie Sh milioni 50 kila moja, kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa makadirio hayo.

Mbunge huyo pamoja na wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.

Sehemu ya barua hiyo yenye saini ya Jairo kwenda kwa idara na taasisi hizo, inasema, “ili kufanikisha mawasiliano ya hotuba hiyo ya bajeti, unaombwa kuchangia jumla ya Sh 50,000,000.

“Fedha hizo zitumwe Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye akaunti Namba 5051000068 NMB tawi la Dodoma. Baada ya kutuma fedha hizo, wizara ipewe taarifa kupitia ofisi ya DP kwa uratibu.”

Barua hiyo ambayo hata hivyo haikufafanua fedha hizo ni kwa ajili gani, sehemu nyingine ilisema kawaida wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti Dodoma, maofisa wa taasisi zilizo chini yake, huambatana na viongozi waandamizi kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

Hata hivyo, Sendeka alisema watendaji wanaohudhuria si wengi kiasi cha kutumia fedha hizo.

Sendeka alimwomba Waziri Mkuu amwelekeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa dharura kubaini kama fedha hizo zimo kwenye akaunti hiyo.

Wakati hilo likiibuliwa, wabunge wengi waliochangia, walijenga msimamo wa kutounga mkono hoja.

Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla (CCM) aliwashawishi wabunge wote wasikubali kuunga mkono hoja wakati nchi ikiwa imetanda giza kutokana na mgawo wa umeme.

“Naomba nitumie fursa hii kuwashawishi wabunge wenzangu, msiunge hoja. Waliotufikisha hapa wanajulikana na hawachukuliwi hatua,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema ,waliokubali kuingia mikataba kandamizi ya kuuza migodi, wanafikiri kwa matumbo badala ya vichwa. Alisema inashangaza kuona watu hao baadhi wako bungeni na wengine wanaendelea kuwa kwenye mfumo wa Serikali, bila kuchukuliwa hatua zozote.

Spika Anne Makinda aliingilia kati kwa kumtaka kutumia lugha ya kawaida badala ya kusema wanatumia matumbo, lakini mbunge huyo aliendelea kusisitiza kuwa wahusika wanafikiri kwa matumbo, kutokana na kuingia mikataba kwa maslahi binafsi na si kwa uzalendo.

“Wangetumia vichwa, wasingesaini. Unasaini mkataba unaoruhusu ardhi kuuzwa na wewe unajengewa nyumba Mbezi!” alisisitiza kwa mshangao.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, kwa niaba ya Mnadhimu wa Bunge, aliomba mwongozo wa Spika na kusema kauli ya kujengewa nyumba Mbezi Beach ni ya kuudhi.

Alimtaka Mbunge huyo kama ana ushahidi auwasilishe kwa Spika, kuliko kusema jambo hilo, ambalo linadhalilisha mawaziri wote.

Spika alimwunga mkono na akawataka wabunge wasiseme kwa hamasa, akisisitiza kwamba kauli kama hiyo inamvunjia heshima pia mtoa hoja.

Wakati huo huo, suala la kampuni ya Symbion kuchukua mitambo ya Dowans lilionekana kuguswa na baadhi ya wabunge; huku baadhi, akiwamo Sendeka, wakielezwa kushangazwa na ukimya uliogubika baada ya kampuni hiyo kuchukua mitambo hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rebeka Mngodo (Chadema), alitaka kufahamu walioridhia Symbion ichukue mitambo hiyo, huku akisema Katiba inaelekeza Bunge lijadili na kuridhia mikataba.

Akizungumzia tatizo la umeme, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alishauri iundwe kamati ndogo ya wabunge tisa ikimshirikisha Rais ambaye ni sehemu ya Bunge, kutafuta suluhisho la haraka.

Alisema Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ilipokwenda Malaysia, Balozi wa Tanzania nchini humo, aliwaambia kwamba aliiandikia Serikali kuhusu IPTL kwamba ina hali mbaya na mradi pekee ambao kampuni hiyo inao, ni uliomo nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walisema lengo si kumsulubu Waziri Ngeleja isipokuwa walimhadharisha kuwa watendaji na viongozi wake ndiyo wanaomsulubu.

Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Amar (CCM), pamoja na kusisitiza kuwa haungi mkono hoja hadi kieleweke, alimwambia waziri, kwamba wanaomsulubu ni watendaji wake ambao wamekuwa wakiingia mikataba isiyo na maslahi kwa Taifa.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvester Koka, akizungumzia tatizo hilo ambalo lilionekana kumsulubu zaidi Waziri Ngeleja, alisema, “hili si suala la Ngeleja. Serikali haikuwekeza vya kutosha katika nishati.”

Mbunge wa Bahi, Omary Badwel (CCM) pamoja na kuikosoa wizara kwa kusema wananchi hawataki maneno bali vitendo, pia alimtetea Ngeleja kwa kusema, “tutamlaumu Ngeleja, lakini hana jinsi, fedha anazopewa ni kidogo. Serikali haipeleki fedha za kutosha kama zinavyopitishwa na Bunge”.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), ambaye pia hakuunga mkono hoja ya wizara kwa kile alichosema wananchi wamechoshwa na orodha ya miradi, alisema bajeti haioneshi kama umeme ni kipaumbele.

Alisema kati ya Sh bilioni 58 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka jana, Sh bilioni 13 pekee ndizo zilipatikana.

Baada ya kubainika kuwa wabunge wengi waliochangia wamekataa kuunga mkono hoja, Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CCM), aliomba Mwongozo ili Bunge liamue kuondoa hoja ya wizara kabla ya muda wa kamati ya matumizi kukaa.

Aliomba hilo lifanyike kwa kile alichosema wizara ipewe muda irekebishe matatizo yaliyo katika bajeti yake, ili kuepuka aibu ya kukataliwa na wabunge.

Hata hivyo, Spika alisema kwenye kanuni hakuna utaratibu wa namna hiyo. Makinda alisema kuanzia muda huo wa mchana hadi saa 11 jioni, marekebisho yatakuwa yamekamilika.

Shelukindo aliwataka wabunge bila kujali itikadi zao, warudishe imani kwa wananchi kwa kukataa kupitisha hoja hiyo.

Alilitaarifu Bunge kuwa angewasilisha hoja baadaye ya kutaka hoja hiyo ya waziri irudishwe ifanyiwe kwanza marekebisho kwa takribani wiki mbili, ndipo iletwe bungeni kwa mara nyingine.

Uchambuzi wa Bajeti ya Afya



SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO


UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII BATT WATAWASILISHA:


MADA: UCHAMBUZI WA BAJETI YA AFYA


Lini: Jumatano Tarehe 20 Julai, 2011


Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni


MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo


WOTE MNAKARIBISHWA!!

Monday, July 18, 2011

Resolute yatoa 320m/- halmashauri ya Nzega

WILAYA ya Nzega mkoani Tabora imekabidhiwa Sh milioni 320 na Mgodi wa Dhahabu wa Resolute zikiwa ni malipo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2011/12.

Akikabidhi hundi hiyo ya Dola za Marekani 200,000 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisa Uhusiano wa Resolute, Mariamu Mavura alisema fedha hizo zimetolewa na kampuni hiyo kama kodi.

Mavura alisema fedha hizo zitumike katika miradi inayoonekana kwa wananchi ili kila mkazi wa Nzega aone na kufahamu fedha hizo kutoka Resolute zimefanya nini katika nyanja za maendeleo.

Akitoa mifano ya ujenzi wa maabara za shule pamoja na shule za sekondari za kidato cha tano na sita kwa kila Tarafa nne za wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Florence Horombe, akipokea hundi hiyo kwa niaba ya Serikali, alisema Serikali inatambua umuhimu wa mgodi huo katika kuchangia mapato ya kodi kwa Halmashauri hiyo.

Horombe alisema mawazo ya mgodi katika matumizi ya fedha hizo yamepokelewa kwa umakini na yatafanyiwa kazi katika matumizi hayo.

DC aliikabidhi hundi hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Kyuza Kitundu, aliyesema fedha hizo zitatumika katika miradi ya ujenzi wa maabara na madarasa ya shule za elimu ya juu kwa kila tarafa.

Kitundu aliupongeza mgodi huo kwa kuwa walipakodi wazuri ambao hawana usumbufu kama baadhi ya wawekezaji wengine.

Friday, July 15, 2011

Rostam amshitua Lowassa

SIKU moja baada ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kutangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mmoja wa watu wake wa karibu, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, amesema hakutegemea kama rafiki yake huyo angejiuzulu ubunge.

Lowassa alizungumza jana mchana mjini Dodoma na kuongeza kuwa alishtushwa zaidi alipoona katika Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) namna wananchi walivyokuwa wakimlilia Rostam.

Alipoulizwa lini atazungumzia kauli zinazotolewa katika vyombo vya habari zikimtaka ajivue gamba, Mbunge huyo wa Monduli mkoani Arusha, alisema atazungumza muda utakapofika.

Rostam na Lowassa wamekuwa marafiki kwa muda mrefu na wote walikuwemo katika Mtandao, kundi maarufu lililoendesha kampeni za kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, Rostam amehusishwa na kashfa mbalimbali nchini zikiwemo za ufisadi, yeye na mawaziri wawili wa zamani, Waziri Mkuu Lowassa na Andrew Chenge.

Watatu hao wamekuwa wakitajwa katika kashfa za Richmond, EPA na rada na majina yao yalitajwa na akina Nape na Chiligati, kuwa wanapaswa kujivua gamba.

Hatua ya Rostam kujiuzulu juzi, sasa inafanya macho na masikio ya wengi kuelekezwa kwa watuhumiwa wenzake hao, Lowassa na Chenge, ambao nao kama Rostam walipewa na CCM muda wa kupima.

Jana, kulikuwa na taarifa kwamba mmoja wa watuhumiwa hao wawili, waliobaki alikuwa akipanga kuchukua hatua kama hiyo ya Rostam, na vikao vilikuwa vikiendelea kupanga jinsi ya kutangaza hatua hiyo. Hata hivyo, gazeti hili lilishindwa kumpata mwenyewe kuthibitisha hilo.

Katika taarifa yake wakati akitangaza kujiuzulu, Rostam aliwatuhumu Nape pamoja na Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Chiligati kuwa wamekuwa wakipindisha dhana nzima ya ‘kujivua gamba'.

Rostam alisema, wawili hao wamekwenda mbali kwa kulitaja jina lake kwa kulihusisha na ufisadi, wakati ukweli wa kimazingira na ushahidi wa wazi umeshathibitisha kuwa ni porojo za kisiasa zinazotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule wa 2015.

Rostam ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu nchini, alikuwa Mbunge wa Igunga mkoani Tabora kwa miaka 18, tangu alipomrithi marehemu Charles Kabeho katika uchaguzi mdogo wa mwaka 1994.

Mbali ya kuutema ubunge, Rostam amejiuzulu wadhifa mwingine mkubwa wa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwakilisha Mkoa wa Tabora tangu mwaka 1997.

Alikuwa mwenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM, akitajwa kuwa mstari wa mbele katika kampeni za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 1995 na 2000, na baadaye katika ‘Mtandao’ kundi linaloaminika kumsaidia Rais Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005.

Alitangaza kujiuzulu nafasi zote ndani ya chama tawala juzi alipozungumza na wazee wa Igunga, akisema si kwa sababu ya kujivua gamba, kwa maana ya kuwataka wote wenye tuhuma za ufisadi kujiondoa CCM, bali kutokana na kuchoshwa na siasa uchwara.

“Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu,” Rostam aliwaeleza wazee wa Igunga.

Katika Sekretarieti ya Kwanza ya CCM baada ya Uchaguzi Mkuu akiwa Mweka Hazina, kabla ya mabadiliko yaliyomtupa nje na kumbakiza na wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu na kujiuzulu Aprili mwaka huu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa chama hicho hakijapata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa mwanasiasa huyo.

Alisema kiutaratibu, mbunge huyo anatakiwa awasilishe kwa njia ya maandishi uamuzi wake huo ndipo chama kinapoanza kushughulikia uamuzi wa aina hiyo.

“Sisi bado hatujapata taarifa yoyote rasmi kutoka kwa Mheshimiwa Rostam. Taarifa zake za kujiuzulu kweli tuzimesikia kwenye vyombo vya habari, kwa hiyo siwezi kutoa maelezo yoyote ya hatua ambazo chama kitachukua kufuatia uamuzi huo,” alisema Mukama.

Hata hivyo akiongea na mwandishi wa gazeti hili mjini Nzega, Rostam alisema, baada ya kutangaza mbele ya wazee waliomshawishi kwa miaka 18 iliyopita kuwa mwakilishi wao kujiuzulu nyadhifa zake kinachofuata sasa ni kufuata utaratibu.

“ Kuna utaratibu, ninapashwa kukiandikia chama changu barua na wao ndiyo watakaopeleka bungeni na Bunge nao kuwaandikia Tume ya Uchaguzi” alisema Rostam na kuongeza kwamba ni mchakato ingawa hakusema lini barua hiyo ataiwasilisha.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kwa sasa hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa ni mapema mno.

“Sina maoni. Kwa sasa ni mapema mno nitakapokuwa tayari kuzungumza nitawataarifu,” alisema Nape.

Alisema, anachofahamu ni kwamba ameshazungumza sana, kutuhumiwa sana na kuzushiwa mambo mengi hivyo kwa sasa ni bora anyamaze na kuwapa nafasi watu wengine nao wazungumze.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kupeleka taarifa za kujiuzulu kwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili Chadema kijiandae kwenda kuchukua jimbo hilo.

Zitto alisema hayo jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika na kuhoji kama Spika ana taarifa ya kujiuzulu kwa Mbunge huyo, ili aipeleke haraka NEC.

Akijibu hoja hiyo, Spika Makinda alisema, hana taarifa rasmi kwa kuwa hakupelekewa barua ila amesoma katika mitandao kama watu wengine.

Makinda alisema taarifa rasmi ikimfikia, utaratibu utafuatwa kushughulikia jimbo lililo wazi.

Thursday, July 14, 2011

Rostam Aziz ajivua gamba

HUENDA katika siku 90 zijazo, wananchi wa jimbo la Igunga mkoani Tabora , wakaingia kwenye uchaguzi mdogo, baada ya Mbunge wao mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM ukiwamo ubunge.

Mbali na ubunge wa Igunga mkoani Tabora alioushikilia kwa miaka 18, Rostam pia ameachia ngazi nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM akiwakilisha mkoa huo.

Hatua yake imekuja siku moja baada ya kukamilika kwa siku 90 ambazo baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya CCM walidai zimetolewa kwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kupima mwenyewe uamuzi wa kujivua gamba.

Hata hivyo, wakati akizungumza na wazee wa Igunga jana, Rostam aliyewahi pia kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema kujiuzulu kwake hakuna uhusiano wowote na kujivua gamba.

“Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa, kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu,” Rostam aliwaeleza wazee wa Igunga.

Alisema CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, iliamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.

Hata hivyo, anasema mabadiliko hayo ambayo Rais Kikwete aliyafananisha na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘kujivua gamba,’ licha ya kuungwa mkono na wajumbe wa iliyokuwa Kamati Kuu akiwemo yeye, yalipotoshwa na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti mpya ya CCM.

“Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye,” alieleza Rostam na kuongeza:

“Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku 90 wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.

“Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.

“Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu, kuwa ndio ambao walikuwa wakilengwa na uamuzi huo.

“Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.”

Rostam alisema mshangao na mshituko wake haukusababishwa na kutajwa kwa jina lake, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ “ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.

“Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa, kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC, uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.

“Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti, wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi, umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.”

“Wazee wangu, ninyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa,” alisema Rostam mbele ya wazee hao.

“Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

“Sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara.

“Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi, kwa sababu tofauti na wengine wengi nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa,” alieleza.

Hivyo, alisema amefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wake ambao anaamini baada ya kujitoa, watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizonazo za kuiongoza CCM na nchi kupitia Serikali yake.

“Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.

“Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alifafanua Rostam aliyechaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1994, akiziba nafasi ya marehemu Charles Kabeho.

Kwa upande mwingine, alisema uamuzi wake anaona ni fursa kwa viongozi wa CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama hicho, ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.

Alisema pia ana imani thabiti kwamba, uamuzi wake wa kubaki kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM, utakuwa chachu kwa chama hicho na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.

Hata hivyo, alisema anaondoka Igunga akiacha mafanikio makubwa katika jimbo hilo na mkoa wa Tabora kwa jumla.

“Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani hapa, lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya,” alisema Rostam.

Lakini pia alimpongeza Rais Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanyia nchi. “Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania.

“Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa jumla; tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndizo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo,” aliomba.

Rostam amekuwa miongoni mwa wanasiasa maarufu wa Tanzania tangu aliposhinda ubunge mwaka 1994 na mwenye nguvu ndani ya chama hicho, kiasi cha kuweza kushinda ujumbe wa NEC mwaka 2007 na kuwamo katika timu ya kampeni ya Rais Kikwete mwaka 2005.

Hata hivyo, pamoja na mchango wake mkubwa katika kampeni hizo, hajapata kupewa nafasi yoyote ya uwaziri naye mara zote ameridhika akielekeza zaidi nguvu katika biashara zake kama alivyobainisha hayo jana katika hotuba yake.

Katika Sekretarieti ya Kwanza ya CCM baada ya Uchaguzi Mkuu alikuwa Mweka Hazina wa Chama, kabla ya mabadiliko yaliyomtupa nje na kumbakiza na wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu hadi kujiuzulu Aprili.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, amehusishwa na kashfa mbalimbali nchini zikiwamo za ufisadi, yeye na mawaziri wawili wa zamani, Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa na Andrew Chenge ambaye pia alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Watatu hao wamekuwa wakitajwa katika kashfa za Richmond, EPA na rada na majina yao yalitajwa na akina Nape na Chiligati, kuwa wanapaswa kujivua gamba.

Hatua ya kujiuzulu jana, sasa inafanya macho na masikio ya wengi kuelekezwa kwa watuhumiwa wenzake hao, Lowassa na Chenge, ambao nao kama Rostam walipewa na CCM muda wa kupima.

Akizungumzia kujiuzulu kwa Rostam, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi, alisema kuachia ubunge kwa Rostam hakutoathiri chama hicho na kwamba ni haki yake na demokrasia inayotekelezwa nchini.
“Jimbo la Igunga halitoathirika na kujiuzulu kwake, CCM tunaamini jimbo hili likitangazwa kuwa liko wazi, tunao watu wengi wenye sifa ambao wanaweza kulirejesha kwa chama chetu,” alisema.

Alisema hata Rostam mwenyewe alipojiuzulu aliweka bayana kuwa atasaidia kuhakikisha kuwa jimbo hilo linabaki CCM, hivyo chama hicho kitajipanga wakati ukifika, kuhakikisha kuwa hilo linawezekana.

Naye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alisema demokrasia ya Tanzania inatoa uhuru kwa mtu au kiongozi kutoa uamuzi kama wa Rostam pale atakapoona inafaa, hivyo uamuzi wa kujiuzulu kwa mbunge huyo ni haki yake.
Alisema kinachofuata sasa ni kwa mbunge huyo kufuata taratibu ambazo ni kuandika barua ya kujiuzulu kwa Ofisi ya Bunge ili jimbo hilo lijulikane liko wazi na kwa mujibu wa sheria, uchaguzi mdogo unatakiwa kufanyika siku 90 baada ya kutangazwa kuwa wazi.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, alisema Rostam amejiuzulu nafasi zake zote za ubunge na chama kwa nia safi na ni habari njema kwa chama.
“Unajua kama kiongozi umekuwa ukisemwa kwa muda mrefu kwa mabaya ni vyema ukajiuzulu ukapisha wengine nao waongoze na kuonesha uwezo wao,” alisema Kimiti.
Hata hivyo, alionya haitakuwa busara iwapo mbunge huyo atakuwa amejiuzulu kwa nia mbaya na kuanzisha makundi ndani ya chama, lakini alipongeza uamuzi wa kiongozi huo na kuuita wa hekima.

Hussein Bashe, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema falsafa ya kujivua gamba inatumika vibaya na kusema nchi ina mambo mengi lakini siasa za chuki zinapewa kipaumbele na ndiyo sababu hata bungeni zimeingia na watu wanasema ovyo ovyo.