JAJI Mkuu mstaafu Barnabas Samatta amesema majaji nchini wamekuwa ‘wakilazimishwa’ kutoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa mbalimbali na kushauri Serikali na Bunge kuipa Mahakama Kuu mamlaka itoe adhabu mbadala.
Wakati Jaji Samatta akitoa rai hiyo kuna taarifa kuwa Rais Jakaya Kikwete amebadilisha hukumu 400 za kifo kuwa za kifungo cha maisha.
Jaji huyo mstaafu alisema wakati mwingine jaji aliyetoa adhabu ya kifo kwa mshitakiwa na kamati maalumu inayomshauri Rais juu ya utekelezwaji wa adhabu za kifo zilizotolewa mahakamani, hupendekeza kwa Rais kuwa adhabu hiyo isitekelezwe na badala yake mshitakiwa apewe adhabu nyingine na mara nyingi ikiwa ni kifungo kirefu.
Samatta alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wanaharakati wa haki za binadamu katika maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika Dar es Salaam katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Kwa nini sheria imbebeshe jaji mzigo wa kutoa adhabu ya kifo wakati anaamini, na kila mpenda haki angeamini kuwa siyo haki kwa mshitakiwa, siyo haki kwa ndugu wa marehemu na siyo haki kwa jamii na kuwa nyufa iliyopo kati ya adhabu hiyo na uovu wa mshtakiwa haizibiki hata utaalamu wa juu ukitumika?” Alihoji Samatta.
Alisema pia washtakiwa wa kifo wamekuwa wakiteseka kisaikolojia wakati wakisubiri hatima yao katika kipindi cha kati siku ambayo jaji anatoa hukumu ya kifo na siku ambayo Rais anapunguza adhabu hiyo ya kifo.
Kwa mujibu wa Samtta dunia imekwishaanza safari ya kufuta adhabu ya kifo na kuisisitizia Serikali na Bunge, kama wanaona ugumu kushiriki katika safari hiyo katika kipindi kifupi kijacho, kwa nini wasianze kuipa Mahakama Kuu mamlaka hayo?
Akifafanua hoja yake hiyo, Samatta alitumia hoja za wanaotetea kufutwa kwa adhabu hiyo kwamba, kwa kuwa haki ya binadamu ya kuishi na kuzaliwa haitolewi na katiba, wafalme au watawala basi hakuna mwanadamu mwingine mwenye mamlaka ya kusitisha haki hiyo katika mazingira yoyote yale.
Alisema pia kuna hatari ya adhabu hiyo kutolewa kwa makusudi au kwa makosa kwa mtu ambaye hana kosa na kwamba ikitumika hivyo hakuna njia yoyote ya kumrudishia marehemu huyo maisha yake.
Katika kutetea hoja hiyo, alinukuu maneno ya mwandishi wa Kifaransa, Nicolas Chamfort aliyepata kusema katika hadithi, “asubuhi leo tumewahukumu watu watatu kunyongwa.
Wawili kati yao kwa kweli walistahili kupewa adhabu hiyo.” Samatta pia alitoa mfano wa tukio aliloliita kuwa la kusikitisha lililotokea wiki iliyopita huko Uingereza ambapo mfungwa mmoja aliachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la mauaji ya kukusudia baada ya kugundulika kuwa hakuhusika kwa namna yoyote ile na mauaji hayo kwa kuwa marehemu aliuawa na mtu mwingine.
“Mtu huyo ana bahati sana kuwa adhabu ya kifo haitumiki huko Uingrereza kwa kosa la mauaji. Isingekuwa hivyo, huenda angekuwa marehemu zaidi ya miaka ishirini iliyopita,” alisema Samatta.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRINGON), Dk Emmanuel Kandusi alisema adhabu ya kifo ni ya kulipa kisasi na kwamba si suluhisho la tatizo la mauaji duniani na kupendekeza elimu iongezwe zaidi kukomesha mauaji mbalimbali.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Tanzania inakadiriwa kuwa na wafungwa 2,246 ambao wanasubiria utekelezaji wa hukumu ya kifo katika magereza mbalimbali nchini huku watu 232 tu wakiwa ndio walitekelezewa hukumu hiyo tangu 1961.
No comments:
Post a Comment