Leo Oktoba 14 mwaka huu, Taifa linaomboleza mwaka wa 10 tokea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, afariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London, Uingereza.
Tokea afariki dunia, Taifa limefanya siku hiyo kuwa ‘Nyerere Day’ kumkumbuka kwa njia ya kufanya mikutano na makongamano.
Mwaka jana, kongamano kubwa la kimataifa likishirikisha watu maarufu kama mwanaharakati wa haki za binadamu na mwandishi wa vitabu, Wole Soyinka wa Nigeria lilifanyika kwenye Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka huu imetangazwa kwamba Mwalimu atakumbukwa kwa kongamano lililoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Umma ingawa litafanyika Oktoba 12, Dar es Salaam, siku mbili kabla ya siku yenyewe iliyozoeleka ya ‘Nyerere Day.’
Katika kongamano la mwaka huu, miongoni mwa mada zitakazotolewa ni kuhusu ufisadi kwa mujibu wa mtazamo wa Mwalimu.
Nyingine itazungumzia mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika ujamaa, ubepari na ufisadi. Pia ipo itakayozungumzia mchango wa Mwalimu katika maendeleo ya jamii; hususan kilimo.
Aidha Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro Oktoba 22 mwaka huu kitakuwa na Warsha ambayo mada kuu itakuwa ‘Kilimo Kwanza na mawazo ya Mwalimu Julius Nyerere.’
Ni vyema kumkumbuka Mwalimu kwa mtazamo na mawazo aliyokuwa nayo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu yakiwamo yale ambayo hadi leo yanatuumiza vichwa.
Lakini vyema pia tukakumbushana kwamba kumkumbuka tu Mwalimu kwa msimamo aliokuwa nao na mchango wake kwa ustawi wa taifa hili hakutoshi.
Hatumtendei haki hata kidogo kwa kuwa hodari wa kumsifia kwa mtazamo na mawazo yake bila ya kutekeleza yale aliyokuwa akihubiri.
Kwa hakika, ufisadi wa kutisha tulioushuhudia nchini usingekuwapo kama watendaji wangezingatia yale yote yaliyokuwa yakizungumzwa na Mwalimu hata baada ya kuondoka madarakani.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba miongoni mwa viongozi wanaoendelea kuzisaliti fikra na miongozo ya Mwalimu, ni wale wale aliokuwa nao karibu mno wakiwamo hata baadhi ya wanafunzi wake.
Kwa mtazamo wetu (na tunapenda kusisitiza hili) ni unafiki kwa viongozi wetu hawa kujitia wanamlilia na kumkumbuka Mwalimu; huku wakiendelea kuyasambaratisha yale yote aliyoyasimamia wakati wa uhai wake. Ni vyema wakaacha unafiki huo.
No comments:
Post a Comment