Thursday, October 8, 2009

Raza: Mafisadi wanafanya nini Kamati Kuu?

MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, Mohamed Raza amesema ni vyema wale wanaotuhumiwa na ufisadi waliomo katika Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) wakajiengua.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kwenye Hoteli ya Star Light mjini Dar es Salaam, Raza alisema cha kushangaza zaidi ni kwamba miongoni mwa wanaotuhumiwa wako kwenye kamati ya maadili ya chama hicho.

Alisema watu hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi walioko kwenye Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na bungeni, wangejiondoa ili kulinda heshima zao na chama chao.

“Mtu mzima akipewa tuhuma yakhe, hukaa pembeni, huo ndiyo ustaarabu,” alisema Raza ambaye hakuwa tayari kutaja majina yao lakini akasisitiza kwamba wanajulikana.

Alisema kujiondoa kwa watuhumiwa hao kutamsaidia Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho aliyeko msitari wa mbele katika kupiga vita ufisadi.

Raza alimsifu Spika wa Bunge, Samwel Sitta kwa msimamo wake uliolifanya Bunge kuwa la aina yake katika kusimamia maslahi ya wananchi, hasa katika vita dhidi ya ufisadi.

‘Kama siyo Bunge, Tanzania leo tungekuwa watumwa. Tanzania ingekuwa ya matajiri wachache,” alisema.

Aliongeza: “Spika ambaye ni kada wa CCM ameweka heshima kubwa katika nchi yetu (katika kupiga vita ufisadi).”

Alisema tuhuma za ufisadi walizonazo baadhi ya viongozi ni nzito. “Kuendelea kwao kuwa bungeni tunasononeka sana,” alisema.

Alisema wimbo unaoimbwa wa maisha bora kwa kila Mtanzania utabaki tu kuwa wimbo usiokuwa na vitendo kwa sababu ya matatizo mengi yakiwemo ya ufisadi. “Tujiulize je, nia ipo?” aliuliza.

Alisema kwa vile mpaka sasa wanachokabiliwa nacho ni tuhuma, waendelee kulipwa mishahara lakini wajiondoe bungeni na nyadhifa nyingine nyeti wanazoshikilia.

Alishangaa ni kwanini viongozi wa sasa hawataki kufuata mfano wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) alipojiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa matatizo yaliyojitokeza ndani ya wizara yake.

Raza alisema haelewi kamati iliyoundwa hivi karibuni na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mzee Ruksa kufuatilia mambo yaliyofanyika bungeni ni ya nini hasa.

“Tunaunda kamati ya Mzee Ruksa. Mzee Ruksa afanye nini sasa hivi. Huyu mzee tusimtumie vibaya. Hakuna bwana kwenye CCM wala hakuna kundi linaloongoza CCM. JK (Jakaya Kikwete) kachaguliwa na wananchi wote,” alisema.

Alisema ili CCM iendelee kushinda ni lazima uadilifu uwepo hivyo waliojitokeza kuwa msitari wa mbele kupiga vita ufisadi ni budi kuwapongeza. “Iko wapi CCM ya mwaka 1977, vijana tunalia,” alisema.

Alisema ipo haja ya CCM kuwa na chuo cha maadili. “Katika masuala ya uongozi lazima tuwe wa kweli,” alisema.

Alisema CCM ingekuwa vizuri ingewapongeza yenyewe makada wake wanaopiga vita ufisadi badala ya kazi hiyo kufanywa na watu wa nje kama ilivyotokea kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambaye alipewa tuzo na Marekani .

Mbali ya kuzungumzia kashfa ya ununuzi wa rada, Raza pia alizungumzia kwa uchungu tuhuma za ufisadi katika mfuko wa kuwezesha uagizaji bidhaa nje ya nchi (CIS).

“Tumefika wakati wa kuzungumza hali halisi. Fedha hizi (za kashfa ya CIS) ni nyingi sana. Fedha zilizochotwa zinaweza zikajenga skuli na vituo vingi vya afya,” alisema.

Alisema maadili ya uongozi katika Tanzania yameporomoka kwa sababu ya kutozingatia yaliyokuwa yanasemwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. “Leo hatuna maadili hata kwenye sera zetu,” alisema.

Alisema kuna umuhimu wa wafanya biashara kuzirejesha fedha walizozipata za CIS zisaidie wenye matatizo luluki vijijini.

Raza alisema kwamba huwa anaachwa hoi anapomwona mkurugenzi wa wizara anapokwenda na gari la Sh milioni 100 kwa wanavijiji wanaohangaika kwa jumbe la mkono la Sh 2,000.

Kuhusu uandikishaji wa vitambulisho vya wakazi Zanzibar, Raza alisema ya kuwa ana imani kuwa kila Mzanzibari mwenye haki ya kupata kitambulisho hicho atakipata.

Alisema tatizo aliloliona ni baadhi ya watu kutokuwa wa kweli katika zoezi hilo la kujiandikisha.

Alisema ni kawaida mtu anazaliwa sehemu nyingine, akakulia kwingine na kuwa mkazi wa eneo jingine.

Alisema tatizo linalojitokeza ni baadhi ya watu kulazimisha kujiandikisha sehemu ambazo wanaona zina maslahi kwa chama chao. Wanafanya hivyo waaktik wanafahamu kwamba sheria inamtaka kila mmoja kujiandikisha kwenye makazi yake ya sasa.

Alisema badala ya kuandikisha kwenye makazi yao halisi huenda sehemu walikozaliwa baada ya kuona sehemu hiyo ina wafuasi wengi wa chama chao au sehemu waliokulia kwa sababu hizo hizo hivyo kuleta mtafaruku.

Aliwataka watu kuwa wa kweli wanapojiandikisha ili zoezi hilo liondokane na ghasia nyingi zinazojitokeza.

No comments: