Monday, October 26, 2009

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KIZAAZAA!

Wakati zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji likielezewa kwa ujumla wake kuwa limefanyika jana kwa amani nchini kote, hali ilikuwa tofauti katika baadhi ya maeneo ambapo kumeripotiwa kuibuka kizaazaa cha aina yake kutokana na vurugu, visa na vibweka vya kila namna.

Taarifa ambazo Alasiri imezipata toka kwa waandishi walio maeneo mbalimbali, zimeeleza kuwa katika baadhi ya maeneo, watu kadhaa wametiwa mbaroni kutokana na vitendo vya kutimka na masanduku ya kura na wengine wamedaiwa kuchanachana karatasi hizo za kura.

Aidha, kwenye baadhi ya vituo, polisi walilazimika kuingilia kati na kuwatuliza watu kwa risasi za moto na mabomu ya machozi, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa hakuna anayediriki kuharibu amani na utulivu wakati wa ukamilishaji wa zoezi hilo la kusaka wenyeviti na wajumbe wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Kwa ufupi, baadhi ya matukio yaliyozua kizaazaa ni kama yafuatayo:

Mabomu, risasi

Katika eneo la Kawe Ukwamani Jijini Dar es Salaam, askari wa jeshi la polisi walilazimika kutumia risasi za moto na pia kumwaga mabomu kadhaa ya machozi kutokana na vurugu zilizodaiwa kuanzishwa na shabiki mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinadai kuwa vurugu hizo zilizotokea katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Ukwamani, zilitokana na balaa lililoanzishwa na kijana huyo aliyefahamika kwa jina moja la Azimio, ambaye baadaye aliwafanya wafuasi wa vyama vyote vitatu vya CCM, CUF na CHADEMA kuzua vurugu kituoni hapo huku wengine wakichapana makonde kavukavu.

Hali hiyo iliyojiri mishale ya saa 12:00 jioni, iliwafanya polisi kuingilia kati na hatimaye kutembeza risasi hewani na kisha kumwaga mabomu kadhaa ya machozi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amethibitisha tukio hilo na kueleza zaidi kuwa hadi sasa, wanamshikilia mtu mmoja kutokana na tukio hilo.

Aidha, tukio jingine la kutembezwa kwa risasi za moto limeripotiwa kutokea Jijini Mwanza, ambapo mtu mmoja amejeruhiwa vibaya na kukimbiziwa hospitalini.

Taarifa hizo zilizothibitishwa leo asubuhi redioni na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serrikali za Mitaa, Bi. Celina Kombani, zinaeleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya wananchi kuzua vurugu kituoni na kuwafanya polisi waingilie kati kwa kupiga risasi kadhaa hewani.

Hata baada ya risasi kupigwa hewani, baadhi ya wananchi hao walikaidi, hivyo polisi kujikuta wakimjeruhi mmoja wa wafanya fujo hao ambaye amekimbiziwa hospitalini.

Watu wasepa na masanduku

Kizaazaa kilichotokana na baadhi ya watu kukimbia na masanduku ya kura kimeripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini, ikiwa ni pamoja na kule Kilwa mkoani Lindi na Rufiji mkoani Pwani.

Taarifa za Kipolisi toka Lindi zinaeleza kuwa watu watatu wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kupora masanduku hayo ya kura na kutimka nayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Sifuel Shirima, amesema tukio hilo limetokea jana saa 7:30 mchana katika kitongoji cha Mnazi Mmoja, eneo la Kilwa Masoko.

Amewataja watu wanaoshikiliwa kutokana na tukio hilo kuwa ni Haji Mponda Yahaya,18, Shaibu Abdulrahman Kandililo,18 na Haruni Makangala ,18.

Aidha, akasema kule Lindi Vijijini, nako kuna watu kadhaa wanasakwa kwa tuhuma za kuvunja masanduku ya kupigia kura na kuchana chana karatasi zote za kura zilizokuwamo ndani yake.

Amesema watu hao walifanya tukio hilo usiku wa kuamkia leo na hadi sasa wanaendelea kusakwa.

Nako Rufiji, kumeripotiwa tukio la baadhi ya watu kutimka na masanduku ya kura.

Imedaiwa kuwa hali hiyo ilitokea baada ya baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi, mawakala wa vyama, polisi na wapiga kura wasiojua kusoma na kuandika kutofautiana juu ya utekelezaji wa zoezi hilo la upigaji kura.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Kassim Majaliwa, amethibitisha juu ya kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilijiri katika kituo kimoja cha Kata ya Mgomba.

Imedaiwa kuwa baadhi ya wapiga kura wasiojua kusoma na kuandika katika eneo hilo waliomba kusaidiwa, na ndipo mawakala wa vyama walipotaka kuifanya kazi hiyo ya kuwapigia kura watu walioamini kuwa ni wafuasi wao.

Ikadaiwa kuwa jambo hilo lilizua ubishani mkali baina ya wasimamizi, polisi na mawakala wa vyama, hali ambayo baadaye ilitoa mwanya kwa baadhi ya watu kutwaa masanduku na kutimka nayo.

"Baada ya kutokea kutoelewana, ndipo baadhi ya watu walipovamia na kuchukua kura zilizopigwa na wengine kukimbia na masanduku ya kura," amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Majaliwa.

No comments: