KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini kuwa Msaidizi wa Spika wa Bunge, Christopher Ndallo, amechukua sh milioni 70 kwa safari zake za ndani na nje ya nchi bila nyaraka zozote.
Aidha, PAC imetoa miezi sita kwa Ofisi ya Bunge kutoa vielelezo vya msingi kuhusu mkataba wa ukarabati wa ofisi ndogo ya Bunge, Dar es Salaam, unaodaiwa kugharimu Sh bilioni 1.1, tofauti na makubaliano ya awali yaliyoanzia Sh milioni 425 na kwamba kinyume na hivyo, wahusika lazima warudishe fedha hizo.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam, katika kikao cha Kamati hiyo, wakati Ofisi ya Bunge ilipokuwa ikitoa maelezo ya hesabu zake za mwaka 2006/07 na 2007/ 08 zilizopata hati chafu.
Akielezea kuhusu Msaidizi wa Spika, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alimtaka Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, kutoa maelezo kuhusu msaidizi huyo anayedaiwa kuchukua kiwango hicho cha fedha ambazo nyaraka zake hazikuonekana.
Kwa mujibu wa Cheyo, alisema msaidizi huyo amekuwa akichukua fedha kwa ajili ya safari za ndani na nje ya nchi, lakini amekuwa harudishi nyaraka zozote zikionesha malipo halali, akamtaka Katibu wa Bunge kujibu kama huwa anapata usingizi kutokana na matukio hayo ambayo hayafurahishi.
“Kabla hatujafika mbali katika kuchambua taarifa yenu, hebu nianze kwa kuuliza, wewe Katibu, hivi huwa unalala usingizi kwa mahesabu yanayoipatia taasisi hati chafu? Jambo la kushangaza ni pale ambapo katika vitabu vyenu mmemwandikia kuwa atarudisha kwa kukatwa mshahara wake, lakini je jambo la kujiuliza analipwa shilingi ngapi hadi aweze kulipa kiwango hicho chote?,” alihoji Cheyo.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha fedha, taarifa inaonesha kuwa kuna wakati msaidizi huyo alichukua zaidi ya Sh milioni 30 kwa wakati mmoja, na Kamati inahitaji kujua kiwango hicho kitarudishwaje au Bunge litaendelea kukopeshana hadi lini.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Lucy Msafiri, alisema hilo ni jambo zito na inahitaji maelezo yenye uwazi kufahamu kama fedha hizo zilichukuliwa kwa matumizi binafsi au ya Spika.
Alisema taarifa inajichanganya, kwa kuwa pengine inasema ni kwa matumizi yake na sehemu nyingine ni kwa matumizi ya Spika, sasa iweje msaidizi akatwe kwenye mshahara.
“Suala la kujiuliza yeye anahusika vipi, kwani Oktoba mwaka huu, alitakiwa kukatwa Sh milioni nane nyingine milioni 2.4 nyingine milioni 4.5 na milioni 2.6 zilizochukuliwa kwa safari za ndani na nje ya nchi,” alihoji Lucy.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walishauri msaidizi huyo aondolewe kama hana sifa zinazostahili kwa maana ya kwamba, harudishi nyaraka jambo ambalo linaweza kumharibia Spika, akaonekana yeye ndiye aliyehusika kwa njia moja au nyingine.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa ofisi za Bunge, Cheyo alisema tangu kuanza kwa ujenzi huo, taarifa zimekuwa zikibadilika mara kwa mara tofauti na mkataba wa awali, jambo ambalo Kamati ilihitaji Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kulifanyia kazi tena.
Alisema ipo haja ya CAG kufanya hivyo kutokana na kwamba hawajaridhika na taarifa hiyo na kwamba ili kujiridhisha kwa taarifa hizo na kuona kama hakuna msukumo wowote ambao ulionekana wakati wa ujenzi huo, lazima urudiwe.
Cheyo alisema ujenzi wa mradi huo umeishtua kamati, kutokana na kuonekana na kupata hati chafu katika kipindi cha mwaka 2006/07 na pia 2007/08 hati ambazo zimekuwa zikirithiwa katika ofisi na kuifanya kuonekana kama inadidimia.
“Kwa Bunge si jambo la kuvumilia hati chafu kutokana na kwamba wamekuwa wakieleza umma juu ya madhara ya matumizi mabaya ya fedha za umma, jambo ambalo Kamati haitawavumilia wanaokiuka,” alisema Cheyo.
Alisema ujenzi wa mradi huo awali uligharimu Sh milioni 425, baadaye kuongezeka Sh milioni 388 zilizotumika kwa ununuzi wa mitambo ya umeme katika ofisi hiyo na nyingine Sh milioni 365 kwa ajili ya samani za ofisini na kwa sasa taarifa zinaonesha kufikia Sh bilioni 1.1.
Akijibu hoja hizo, Kashilila alisema jambo hilo ameliona na amekuwa akijadiliana na wenzake akisema ujenzi huo ulikuwa na sura mbili tofauti, kwani awali ilikuwa yawe maegesho ya magari na baadaye kukawa na mabadiliko ya kujenga ofisi jambo ambalo liliongeza gharama.
Hata hivyo, alisema zipo hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kudhuibiti matumizi mabaya ikiwa ni pamoja na kudhibiti usimamizi wa matumizi ya fedha, lazima kuzingatia kanuni na taratibu za fedha na manunuzi.
Aliongeza kuwa kanuni za ujenzi hazikufuatwa kwa mkataba kusainiwa Juni mwaka juzi, wakati Bodi ya Zabuni iliidhinisha Oktoba mwaka huo, kwa sababu ilionekana kuwa wasingefanya hivyo, gharama ya ujenzi ingekuwa kubwa zaidi na kuanza upya kutokana na wakandarasi kuondoka eneo la tukio.
No comments:
Post a Comment