UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa utafanyika kote nchini Jumapili ya wiki hii. Kwa mara nyingine mustakabali wa taifa letu utakuwa kwenye sanduku la kura.
Uchaguzi wa safari hii ni muhimu pengine kuliko chaguzi nyingine zilizopita. Tunaamini hivyo kwa sababu huu wa safari hii unafanyika wakati nchi yetu ikipitia kipindi kigumu na cha majaribu makubwa.
Si tu kwamba nchi yetu, hivi sasa, inatikisika kutokana na kushamiri kwa ufisadi nchini, lakini pia pengo kati ya matajiri na masikini linazidi kukua kwa kasi, na hivyo kutishia amani ya taifa letu.
Si siri vilevile kwamba nchi yetu imefikia hapa ilipo kwa sababu ya kuwa na viongozi dhaifu na waroho wa pesa kuanzia ngazi za chini kabisa hadi juu.
Viongozi hao dhaifu na waroho wa pesa wamefanikiwa kukamata madaraka baada ya kuwahadaa wananchi masikini kwa kuwapa vijisenti, khanga, fulana, kofia na hata wakati mwingine pilau tu! Kwa maneno mengine, wameutumia umasikini na ujinga wa wananchi kuingia madarakani.
Uzoefu umetuonyesha kwamba viongozi wa namna hiyo wanapoingia madarakani hujishughulisha tu na ufisadi na huitelekeza kabisa agenda ya maendeleo; kwa sababu wanajua kwamba uchaguzi mwingine utakapowadia watawaendea tena wapiga kura na kuwahadaa kwa vijisenti, fulana, khanga, kofia na pilau.
Kwa hiyo, kama hakuna maendeleo ya maana yanayoonekana katika mitaa yetu na vijiji vyetu, ni kwa sababu ya kuwaingiza madarakani viongozi dhaifu wa sampuli hiyo.
Ni mpaka hapo tutakapouvunja mzunguko huo wa kijinga kwa kukataa kuuza kura zetu kwa fulana, khanga, kofia na pilau; ndipo tutakapoweza kuwaweka madarakani viongozi waadilifu na wachapakazi wanaoweza kuchochea maendeleo na kuleta mabadiliko ya kweli mitaani mwetu na katika vijiji vyetu.
Ni kwa msingi huo, tunawasihi wapiga kura kutumia busara katika uchaguzi huo wa Jumapili. Wakipiga kura zao kwa busara wanaweza kuleta mapinduzi ambayo tumeyasubiri kwa muda mrefu sasa.
Tukumbushe tu kwamba kupiga kura si mchezo. Kupiga kura kunahitaji upembuzi yakinifu wa kila mgombea.
Tunawasihi wapiga kura hiyo Jumapili wasibweteshwe na vyama vyao; maana matatizo yao ni zaidi ya siasa za vyama. Wamchague mgombea aliye bora; na haijalishi ni wa CHADEMA, CUF au CCM.
Tunawasihi wajiridhishe kwamba huyo wanayempigia kura ndiye haswa anayefaa kuwaongoza; hata kama walipewe vijisenti, khanga,fulana au pilau na mgombea mwingine. Kila la heri.
Source:www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment