Friday, October 23, 2009

Shahidi amkaanga Liyumba

SHAHIDI wa kwanza katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Benki Kuu Tanzania (BOT), Amatus Liyumba, amesema, mshitakiwa huyo alikuwa akifanya mabadiliko ya ujenzi wa jengo la BoT bila kuwahusisha wakurugenzi wa bodi kwenye taasisi hiyo ya Serikali.

Shahidi huyo kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Sief Mohamed (49) ameieleza mahakama kuwa, nakala ya mkataba wa ujenzi wa majengo hayo unaonyesha kipengelea kinachoeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unaweza kubalidika wakati wowote kutokana na thamani halisi ya fedha kwa wakati huo.

Mohamed alieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, Liyumba aliandika barua inayoagiza ujenzi wa upanuzi wa majengo pacha uendelee,na kwamba wajumbe wa bodi waliidhinisha ulipaji wa fedha za ujenzi huo.

Liyumba anadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 221.

Amesema, uchunguzi aliofanya umebainisha kwamba, kulingana na mkataba,ujenzi wa majengo hayo 14 ungegharimu Dola milioni 73.6 za Marekani lakini kulingana na mabadiliko ya ujenzi huo, kulikuwa na nyongeza ya Dola milioni 253.9 za kimarekani, hivyo kwa ujumla ujenzi umegharimu dola milioni 357.7 za Marekani.Mohamed amesema, cha kushangaza, ghorofa zilizojengwa katika benki hiyo ni 18 badala ya 14, na kwamba, zimeongezeka ghorofa nne.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, ghorofa zilizoongezeka hazikuwa kwenye mkataba uliosainiwa kati ya BoT na kampuni ya Afrika Kusini iitwayo Group 5 East (PTY) Ltd.

Mohamed alizitaja sehemu za majengo hayo zilizoongezeka kuwa ni kiwanja cha kutua Helkopta, kuta za majengo zilizonakshiwa, minara miwili, vigae vya ukumbi wa mikutano pamoja na sehemu za ukuta wa uzio.

Amesema, badala ya rangi ya kawaida wameweka plasta, na kwamba,vitu hivyo vilivyoongozeka havikuwa kwenye mkataba halisi wa ujenzi wa majengo hayo pacha.

Mohamed ameieleza mahakama kuwa, ana barua za Liyumba zinazoonyesha kutoa maagizo ya ujenzi huo kwenda kwa bodi ya BOT kuiomba iidhinishe gharama za ujenzi huo lakini barua hizo hazionyeshi ni kiasi gani alichokuwa akikiomba.

Wakili Upande wa Utetezi, Majura Magafu, alimtaka Mohamed aonyeshe mahakamani hapo barua anazodai Liyumba alikuwa akiandika kwenda kwa Bodi ya Wakurugenzi BOT inayotaka waridhie ujenzi wa jengo hilo na malipo yafanyike baadaye.

Mohamed alishindwa kutoa nakala ya barua hiyo kwa madai hakuwa nayo mahakamani hapo, na kwamba, shahidi mwenzake atazitoa mahakamani hapo akija kutoa ushahidi wake kama zikitakiwa.

Magafu alimuuliza Mohamed kwamba, Liyumba alikuwa na mamlaka gani ya kutaka majengo hayo yaongezeke bila bodi kufahamu.Shahidi huyo aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa kuna barua zinazoonyesha Liyumba alikuwa akiiamuru bodi hiyo kuruhusu ujenzi uendelee.

Magafu alizidi kumbana shahidi huyo kwa kumwambia inakuwaje Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi aamuru Ujenzi wa BoT uendelee bila kupitia kwenye bodi na kusababisha hasara wakati jengo ni zuri na linaendelea kutumiwa.

Magafu: Hivi umekuja kucheza mpira au kutoa ushahidi kama Liyumba aliiba au la,sema ukweli kama wewe ni mchunguzi na si kusema uongo, ni kweli Liyumba amesababisha hasara mnayodai au ni chuki zenu?

Mohamed : Mahakama ndio itajua kama kweli kasababisha hasara au la, ila kuna baadhi ya mambo aliyafanya bila idhini ya Bodi.

Magafu: Je unadai katika barua alizoandika Liyumba hakuna sehemu inyoonyesha aliomba kiasi gani cha fedha sasa hapa anashitakiwa kwa kosa gani wakati jengo ndiyo lile mnaliona ni zuri na linatumika, huoni kama ushahidi unaoutoa mahakamani hapa si wa kweli, na kwa nini BoT iliamuru ujenzi wa ghorofa hizo uongezwe.

Mohamed : Yawezekana waliamua kuongeza ujenzi huo kwa sababu ya ongezeko la wafanyakazi ,nakubali jengo ni zuri lakini halikuwa kwenye makubalino ya mkataba.

Magafu: Kwa nini mlipoanza uchunguzi wenu msimuhoji aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali ambaye hivi sasa ni marehemu na angeeleza ukweli wa majengo hayo na kutaja nani alihusika badala yake mnadai Liyumba anahusika wakati hakuwa mjumbe wa bodi, pia ni kwa nini maelezo ya awali yapishane na kiasi cha fedha cha sasa unachosema.

Mohamed:Kimya

Baada ya mawakili kumaliza kumhoji Shahidi huyo, jopo la mahakimu likiongozwa na Hakimu Edson Mkosinongwa, walimuuliza Mohamed Liyumba anashitakiwa kwa kosa lipi kati ya kuongeza jengo au yawezekana amenufaika kwa kitu chochote.

Mohamed alijibu hawezi kufahamu Liyumba ana kosa gani lakini ushahidi utaonyesha kama ana kosa au la kwa sababu hana chuki nae.

Wakati mwingine Mohamed alikuwa akiulizwa maswali ambayo yalikuwa yakimtatiza na kuwafanya baadhi ya ndugu waliokuwa mahakamani hapo kuanguka kicheko na wengine kuguna kutoka na kubanwa na mawakili upande wa utetezi kwa sababu ya majibu yake kujichanganya hali iliyomlazimu wakili wa Serikali, Juma Ramadhani kuingilia kati na kusaidia baadhi ya ushahidi kwa kumuuliza maswali Mohamed ili yarekodiwe vizuri na kutumika wenye mwenendo wa kesi hiyo.

Mei 28 mwaka huu, Liyumba alipandishwa kizimbani kujibu mashitaka mawili likiwemo kuhusika katika ujenzi wa ghorofa pacha za makao makuu ya BoT, akidaiwa kupandisha gharama. Kesi hiyo ina mashahidi 10 wakiwemo maprofesa watatu.

No comments: