KITANZI kimeandaliwa kwa mkulima mdogo nchini ategemeaye kilimo kwa maisha yake. Kitanzi kimeandaliwa anyongwe hadi kufa. Bado kitambo kidogo kamba itawekwa shingoni, mnyongaji ataivuta na huyo mkulima atakoroma, pumzi itamwishia na mwishowe kufa!
Kitanzi hiki kiliandaliwa mapema mwezi Juni mwaka huu na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Baraza la Biashara la Taifa [TNBC], uliofanyika Kunduchi Beach Hotel and Resorts, chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na kuhudhuriwa na baraza lote la mawaziri, wafanyabiashara [wawekezaji] mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi, kuzungumzia hali ya kilimo nchini na mustakabali wake.
Mkutano huo uliokuwa na washiriki karibu 380, wasomi wenye kulelewa na kulewa itikadi na sera za maendeleo za uchumi za mrengo wa nchi za ubepari wa Magharibi, ulibaini, pamoja na mambo mengine kuwa, sababu kubwa kwa Tanzania kutofanikiwa kugeuza na kuboresha kilimo, ni “kuzalisha isichotumia, na kutumia isichozalisha”; kwa maana kwamba, tunazalisha zaidi mazao ya biashara kwa ajili ya kuuza nje; na tunatumia zaidi kile tunachoagiza kutoka nje.
Kwa hiyo, mkutano huo, chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, ukaja na “mwarobaini” wa matatizo ya kilimo chetu kwa njia ya kuanzisha Programu ya “Mapinduzi ya Kijani” [Green Revolution], yaliyopewa jina la “Kilimo Kwanza”.
Swali kuu la kujiuliza: Je, ni kwa kiasi gani wale waliokutana Kunduchi Beach Hotel and Resorts, wanawakilisha matakwa au kubeba dhamana ya wakulima wanaounda asilimia 80 ya Watanzania?
Tunahoji hilo kwa sababu sera nyingi, mikataba na hata miswada ya Bunge, imepitishwa bila kuwashirikisha wananchi kikamilifu; licha ya kwamba madhara yake yanabebwa na wananchi masikini wa Taifa hili kwa uchungu mkubwa. Na ndivyo programu hii ya “Kilimo Kwanza” inavyojionyesha.
Wasomi wetu, kwa kujasirishwa na ubepari wa kimataifa, wametenda mabaya kwa watu wao bila hofu; kana kwamba wamehakikishiwa ufalme: “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa sababu baba yenu [Benki ya Dunia, IMF] ameona vema kuwapa ule [ulaji] ufalme” [Luka 12:32].
Hawa wanaoiangamiza nchi yetu kwa sera mbovu za mapokeo [ubepari, utandawazi, soko huria], ubinafsishaji usiojali, mikataba mibovu yenye kuitafuna nchi, ufisadi; lakini bila hofu ya kuhojiwa wala kuwajibishwa, si ndiyo hao ‘kundi dogo’ lenye fungate na ubepari wa kimataifa [baba yao], unaochafua sera zetu nzuri, maadili ya taifa na uzalendo?
Kama kweli hili si kundi dogo lililokabidhiwa “ufalme” [ulaji], kwa nini vigogo wa kashfa za IPTL, Deep Green, Meremeta, Tangold na baadhi ya vigogo wa EPA hawaguswi? Hao wameitafuna sekta ya umeme na madini wakaimaliza, na sasa, kwa kutuona wajinga, wanawania kuitafuna sekta ya ardhi na kilimo bila kuogopa; wakijiliwaza kwamba [kuna] amani [katika uwekezaji].
Ukweli ni kwamba amani haipo; bali wamemjeruhi mkulima mdogo kwa kumdunga sindano ya kuua maumivu na usingizi [kwa kumlewesha na njozi za injili ya Benki ya Dunia, IMF, WTO, FAO]. Itakuwaje atakapozinduka na kuyahisi maumivu hayo? Itakuwaje atakapoponyoka kuepuka kitanzi?
Angalia orodha ya walioalikwa kwenye mkutano wa TNBC/Kilimo Kwanza: Mawaziri (40) wanachama wa TNBC (125) wawakilishi kutoka Sekta ya Kilimo na sio vikundi vya wakulima wadogo (63) wawakilishi wa mabaraza ya biashara ya mikoa (35), maafisa wa Serikali (125) na wawakilishi kadhaa wa makampuni binafsi hapa nchini.
Kwa mujibu wa programu hiyo ya “Kilimo Kwanza”, nchi yetu inakusudia kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara, chenye kutumia teknolojia ya hali ya juu; na wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wenye kutumia zana kubwa kubwa za kilimo [matrekta, mashine za kuvuna, mbegu za viini tete zinazozalishwa viwandani na pembejeo za kilimo za gharama], watapewa kipaumbele katika mpango huu.
Hao watapewa ardhi, mikopo ya mabenki, misamaha ya kodi na vivutio vingine chini ya kile kinachoitwa “mazingira mazuri ya uwekezaji” kutoka nje [FDI], kama ilivyofanyika katika sekta ya madini na nishati, na kufungua mlango kwa uporaji wa rasilimali zetu na jasho la wananchi.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment