Sunday, October 18, 2009

Si kweli kwamba Nyerere alikuwa haambiliki: Jaji Warioba

Unafahamu siku ambayo Mwalimu Julius Nyerere alipotaka kuteleza na hatimaye kukiuka sheria? Je, unafahamu ni kwa namna gani alivyokuwa akiendesha vikao muhimu kwa mustakabali wa nchi? Katika makala haya, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wake, na baadaye Waziri wa Sheria na Katiba, Jaji Joseph Warioba, anaelezea hayo ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 10 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

KATIKA mazungumzo yake aliyoyafanya mjini Dar es salaam na waandishi wa habari, hivi karibu, Jaji Warioba alizungumza mengi kuhusu hali ya sasa ya nchi, lakini pia alimgusia kidogo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Alianza kwa kuzungumzia madai yanayoelekezwa kwa Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa haambiliki; kwa maana kwamba hakuwa akisikiliza wasaidizi wake.

Jaji Warioba anasema: “Unajua kuna watu walikuwa wanasema haambiliki, lakini Mwalimu Nyerere ni mtu aliyekuwa anasikiliza sana.

“Mimi nimefanya naye kazi kwenye serikali. Nilikuwa kwenye cabinet (Baraza la Mawaziri), nimekuwa kwenye chama, niliingia kwenye Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1976. Wakati alipokuwa mwenyekiti (wa CCM-Taifa) baada ya kutoka kwenye urais, mimi ndiye nilikuwa Katibu wake wa Ulinzi na Usalama.

“Staili ya Mwalimu, iwe kwenye cabinet, au iwe kwenye National Executive alikuwa na kakitabu kadogo. Mnaanza mjadala, mnanyoosha mikono tena anaandika… ataandika majina kisha ataita mmoja mmoja. Mnaweza kuendelea na mjadala siku nzima hamsikii akisema, anawasikiliza tu. Mkimaliza ana sum-up (anafanya majumuisho). Ni mtu ambaye alikuwa anajua, alikuwa mtaalamu kabisa wa kujenga consensus,” alisema Jaji Warioba.

“Unajua kila mahali kuna makundi. Sasa unaweza kuwa na kundi la viongozi hawa wanaona wale wenzao wanasema mambo ya ovyo ovyo hivi. Na kwenye cabinet mnaweza kumsikia mtu anazungumza, mnasema huyu anazungumza utumbo.

“Lakini Mwalimu akija ku-sum-up anasema kama fulani alikuwa amesema hivi… wote mnatoka pale mnaona uamuzi ule ni wenu wote, na ndiyo maana unaona kipindi chetu kile ilikuwa akizungumza Rais, utakuta wengine wanaozungumza walikuwa wanazungumza namna ile ile, kwa sababu ni kitu kilichozungumzwa na mnakielewa.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kauli za viongozi kupishana hazikuwapo enzi za utawala wa Mwalimu. “Baadhi wanafikiri tulikuwa parrots (kasuku) wa kuimba wimbo wa Mwalimu, lakini unawezaje kuimba exactly kama hukuelewa?,” aliuliza Jaji Warioba na kuongeza: “Ilikuwa ni kujenga ile consensus, ndiyo uongozi wake ulivyokuwa.

Jaribio la kuvunja sheria

“Na kinyume na wale wanaosema alikuwa haambiliki, si kweli. Alikuwa anakasirika kama mtu mwingine yeyote yule na aliweza kukufokea. Na wakati fulani alikuwa amemteua mtu katika nafasi fulani. Mimi kama Mwanasheria Mkuu wake nikaenda kumwambia: ‘Mwalimu hapa sheria inakataa, huwezi kumteua huyu.’

“Nikamwambia kuna kikwazo cha kisheria hapa, kwa kuwa alikuwa yule mtu (aliyepaswa kuteuliwa) alikuwa ameonewa mambo fulani. Mwalimu akakasirika, akaniambia wewe ndiye kikwazo. Wewe umezoea kila ukija hapa ni kuniambia usifanye hivi kwa sababu sheria inakataa, hapana hili sikubali.”

“Nikamwambia Mwalimu, hili ni suala la Katiba, ukifanya hivi kutakuwa na crisis (mgogoro) kwenye Bunge. Akasema si ndiyo demokrasi? Ngoja iende huko. Nikamwambia kwamba ni suala la Katiba, na yeye ndiye guardian (mlezi) wa Katiba.

“Nikaendelea kumwambia Mwalimu kwamba ikitokea crisis na yeye ndiye guardian; yaani imesababishwa na guardian, ni kitu serious. Akasema ndiyo demokrasi, haya mambo ya kufichaficha siyo mazuri; ngoja iende huko.”

Jaji Warioba anaendelea kulikumbuka tukio hilo na kusema: “Nikatoka pale, nikaenda kwa Waziri Mkuu, Sokoine (Edward) nikamwambia; ‘PM sasa kutakuwa na matatizo kwenye Bunge, boss hataki kubadili msimamo’, akasema aah hebu twende bwana tumshauri angalau asimwapishe huyu mpaka tuwe tumetoka bungeni.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, walipokwenda kumwona Mwalimu asubuhi nyumbani kwake, Msasani Dar es Salaam, yake mambo yakawa tofauti. Walikwenda kumwona Mwalimu Msasani, kwa kuwa alikuwa na ofisi yake ndogo aliyokuwa akiitumia na alikuwa akifika Ikulu kama kuna matukio rasmi, kama mkutano wa Baraza la Mawaziri au mengine.

“Alipotuona tu akaanza kucheka, akasema; ‘Edward (Sokoine), nilimfukuza huyu jana; lakini aliniambia kitu kimenisumbua sana usiku. Sasa sijui kimekuleta nini hapa? Waziri Mkuu akaelewa na akauliza, sasa nini kimekusumbua?

“Mwalimu akasema nimefuata ushauri wake. Akasema: ‘Joseph, wewe ni stubborn (msumbufu) eeh?’

Chimbuko la tukio hilo ambalo lingemweka Mwalimu Nyerere katika mgogoro wa kikatiba, lilihusu uamuzi wake wa kumteua mkuu wa mkoa.

Ilikuwa mwaka 1983, mtu huyo (jina linahifadhiwa), awali alikuwa na kesi mahakamani, na kwa mujibu wa sheria kwa wakati huo, ukifikishwa mahakamani unapoteza baadhi ya haki za kiraia kama kupiga kura kwa nyakati fulani.

Kwa hiyo kwa kuwa Mwalimu alitaka kumteua mtu huyo kuwa mkuu wa mkoa, ambaye kwa wakati huo moja kwa moja angekuwa mbunge, mgogoro ungejitokeza kikatiba kwamba, mbunge ni lazima awe na sifa kamili za kiraia (zikiwamo za kupiga kura), ambazo kama mhusika huyo angeteuliwa asingekuwa nazo.

Jaji Warioba anahitimisha simulizi ya tukio hilo kwa kusema: “Lakini sasa wakati mwingine kuwa stubborn kunasaidia; yaani usije ukaacha kusisitiza hoja yako kama unaamini uko sawa sawa. Kwa hiyo, ni kweli wakati mwingine Mwalimu alikuwa mbishi, lakini akikaa akitulia anajirudi.

“Kwa hakika, ni mtu mmoja ambaye, kwa viongozi niliowahi kufanyanao kazi, alikuwa haoni aibu kuja kusema hapa nilikosea.

“Mwalimu alikuwa giant kwenye intellectuals, no doubt about that, na he could stand his ground kwenye argument”, anasema Jaji Warioba na kuongeza: “Lakini alikuwa ni mtu ambaye yuko tayari ku-compromise. Ni mtu ambaye pamoja na kwamba alifika kiwango hicho cha juu, kimsingi alikuwa ni mtu wa kawaida.

“Kama ungefika Butiama ukakuta anacheza bao na wale wazee, na wewe humfahamu; na kisha wale wazee wakakuambia Rais yuko hapa, unaweza usiamini.

“Mimi ni Muikizu, siwezi kuzungumza Kiikizu kwa ufasaha. Nitachanganya na Kiswahili tu, lakini Mwalimu alikuwa anakaa na Wazanaki wale huku akizungumza Kizanaki kwa ufasaha.

“Alikuwa ni mtu wa kawaida. Mtaona hata msisitizo wake katika mambo ya maendeleo alipokuwa akisema people centred development ilikuwa ni hiyo ya kuwaweka mbele wananchi. Alikuwa akisema elimu ya Mtanzania ni primary school kwa sababu anawafikiria wale wananchi wa kawaida. Akisema afya ya Mtanzania ni zahanati, anamaanisha hivyo hivyo. Na alipata matatizo sana aliposema kuwa elimu ya Mtanzania ni primary school.”

Mbio za siasa baada ya Mwalimu

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kisiasa hapa nchini kuna uhuru zaidi, na hilo ni lazima Watanzania walikubali. “Ule mfumo wa chama kimoja ulikuwa na nidhamu yake, sasa uhuru ni mpana zaidi wa kutoa mawazo, lakini tofauti mimi nafikiri chama na viongozi wakati ule walikuwa kweli wanajituma”.

“Kulikuwa na kujituma katika kuutumikia umma. Hivi sasa siasa zimekuwa za ubinafsi mno; yaani msisitizo kwenye utumishi kwa umma umepungua.

“Unajua mazoea bwana ni magumu sana, unajua mimi siku hizi huwa nasahau. Wakati mwingine ninaposema sistahili kutukuzwa, ninaonekana kama wa ajabu hivi. Stahili siku hizi ni uheshimiwa. Kuna kupenda ukubwa, na hata wanapojitambulisha husema kuwa mimi ni mheshimiwa mbunge fulani.

“Acha wengine wakuite mheshimiwa, siyo wewe mwenyewe ujiite hivyo. Kwa hiyo, nadhani uhuru wa mawazo umepanuka zaidi lakini ukichukua siasa kwa ujumla commitment yake ni kama imepungua.

Mwalimu dhidi ya ufisadi

“Kama kuna kitu Mwalimu alikuwa anachukia ni rushwa, ubadhirifu, wizi matumizi mabaya ya madaraka. Kuna wakati kuna mahali alisema kwamba pamoja na kujua kwamba kumchapa mtu mzima viboko ni kitu kibaya, lakini alikubali wala rushwa wakithibitishwa mahakamani wachapwe viboko.”

“Alikuwa na msemo wake: Caesar’s wife must be above suspicion; yaani ile suspicion tu inatosha kwamba uongozi wako umefika mwisho. Siku hizi inabidi uthibitishwe na Mahakama, lakini yeye kwake uaminifu ni kitu kikubwa, kwa hiyo hata kutuhumiwa tu inatosha kupoteza sifa za uongozi.

Kuhusu demokrasia, Jaji Warioba alisema hivi: “Nadhani demokrasia yetu (pamoja na malumbano yake yote) imepanuka. Nadhani mfumo wa vyama vingi umekuza demokrasia. Tatizo nadhani lipo kwenye vyama vyenyewe; yaani hakuna demokrasia.

“Tunasisitiza demokrasia ya nchi, lakini ni kama vile tunafumbia macho demokrasia ndani ya vyama vyetu. Tumekuwa zaidi watu wa kanuni na taratibu, lakini kama tukiimarisha demokrasia, hasa katika vyama, tutafika mbali; maana sasa hivi inaonekana demokrasia ni kama kupingana hivi”.

No comments: