Thursday, May 19, 2011

Serikali yatoa tamko kashfa ya rada

Serikali ya Tanzania imepinga vikali uamuzi wa kampuni ya silaha ya Uingereza –BAE Systems wa kulipa fidia ya Paundi milioni 29.5 za Uingereza kwa Tanzania kupitia asasi isiyo ya kiserikali badala ya kulipa fedha hizo moja kwa moja serikalini kufuatia kukamilika kwa kesi ya rushwa ya ununuzi wa Rada.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Kampuni ya BAE System iliiuzia Tanzanai Rada kwa gharama ya Paundi milioni 41 za Ungereza wakati gharama halisi ilikuwa Paundi milioni 12.
Akitangaza msimamo wa serikali leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe amesema, uamuzi huu unaenda kinyume na msimamo wa serikali yetu uliotaka fidia hiyo irejeshwe serikalini.“Fedha hizo ziliibwa kutoka serikalini na hazina budi kurejeshwa serikalini,” amesema.

Tamko la Serikali limekuja miezi sita baada ya uamuzi uliotolewa na Jaji Bean wa mahakama ya Southwark ya Uingereza Desemba 21,2010 kutoa uamuzi kuwa BAE kulipa Paundi milioni 29.5 kwa wananchi wa Tanzania.

Jaji Bean alitoa uamuzi huo baada ya kutorishika na na maelezo ya makubaliano ya Ofisi ya Makosa makubwa ya jinai ya Uingereza SFO na BAE.
Kwa mujibu wa Waziri Membe, kampuni ya BAE system badala ya kulipa fedha hizo moja kwa moja kwa wananchi wa Tanzania, imeamua kuunda jopo litakalojumuisha watu kutoka ndani mwake kuishauri jinsi itakavyotumia fedha hizo kupitia kwa asasi isiyo ya kiserikali ya uingereza na sio kwa serikali ya Tanzania.

“Msemaji wa BAE amenukuliwa na Ubalozi wa tanzania nchini Uingereza akisema kampuni yake inaongozwa na sera ya kutoa misaada ya kihisani kwa asasi zisizo za kiserikali tu. Kwa msingi wa sera hiyo, kampuni hiyo haitaweza kulipa fidia hiyo moja kwa moja kwa serikali ya Tanzania,” amesema.

Waziri Membe amesema kuwa uamuzi hu wa BAE unalengo la makusudi kuonyesha sura ya kutokuamini mpango wa pamoja wa Serikali za Tanzania na Uingereza ulioelezea jinsi fedha hizo zitakavyotumika.

“Serikali ya Tanzania ilikusudia kutumia fedha hizo kununua jumla ya vitabu milioni 4.4 kwa ajili ya shule za msingi, vitabu vya miongozo ya mitaala 192,000 kwa ajili ya masomo 12 katiak shule 16,000, kununua madawati 200,000 kwenye shule zilizo na upungufu wa madawati na kujenga nyumba 1,196 za walimu katika wilaya zote nchini, kujenga vyoo 2,900’ amesema.

“BAE wanajaribu kujikosha mbele ya asasi mbalimbali zisizo za kiserikali za Uingereza baada ya kukosolewa sana kwa kashfa ya rushwa na kutoka sasa kuonekana kwamba inawajali zaidi Watanzania kukliko serikali yetu,” ameseam.
Waziri Membe ameeleza kuwa kampuni hiyo silaha ikikaidi kutoa fedha hizo moja kwa moja kwa serikali ya Tanzania, hakuna asasi isiyo ya Kiserikali ya Uingereza itakayopewa fedah hizo na kuruhusiwa kuja nchini.

Imeandikwa na Joseph Ishengoma
MAELEZO, DAR ES SALAAM

No comments: