Friday, May 6, 2011

Kikwete atakiwa mahakamani

RAIS Jakaya Kikwete ameombwa kutoa ushahidi kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania
nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Ofisa Tawala wa ubalozi huo, Grace Martin katika kesi inayowakabili ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa washitakiwa hao, Mabere Marando alidai jana kuwa wamewasilisha barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi Mei 2, mwaka huu, kuelezea nia ya kumuita Rais Kikwete kama shahidi wa upande huo wa utetezi.

Marando alidai sheria inawataka kufanya hivyo kwa kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, naye anaweza kufika mahakamani ama kuwasilisha hati ya kiapo kama iliyowasilishwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Alidai ushahidi wa Rais Kikwete unahitajika kwa kuwa mshitakiwa anadaiwa kufanya makosa wakati ambao Rais Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

“Tumemfahamisha Katibu Mkuu Kiongozi pia kwamba Rais kama hatoweza kufika mahakamani, kusimama kizimbani na kutoa ushahidi, basi hati yake ya kiapo itatosha,”
alisema Marando.

Marando alisema mashahidi wengine wanaotarajia kuwaita ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha wa wakati huo, Basil Mramba na mashahidi wengine saba kufanya idadi ya mashahidi wao kuwa 10.

Hati ya kiapo ya Mkapa iliwasilishwa mahakamani hapo na wakili huyo juzi na kukabidhiwa mawakili wa Serikali.

Katika hati hiyo, Mkapa amedai kuwa kwa kipindi chote alichofanya kazi na Mahalu katika nyadhifa mbalimbali za kiserikali, mshitakiwa huyo alionesha tabia nzuri.

Mkapa amedai Mahalu alikuwa mnyenyekevu, mwaminifu na mfanyakazi hodari aliyezawadiwa heshima ya juu na Rais wa Italia Siku ya Taifa la nchi hiyo kipindi kirefu tangu aondoke nchini humo.

Pia Rais mstaafu alidai kuwa jengo ambalo Profesa Mahalu anatuhumiwa kununua la ofisi ya Ubalozi wa Tanzania mjini Rome, lilinunuliwa kipindi ambacho alikuwa Rais wa Tanzania na kudai manunuzi ya jengo hilo yalikuwa kwa mujibu wa sera ya Serikali.

Amedai katika hati hiyo kuwa sera hiyo ni ya kumiliki au kujenga ofisi za kudumu na makazi kwa mabalozi wa nje ya nchi na ililenga kupunguza gharama.

Profesa Mahalu anakabiliwa na kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni mbili kwa kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia katika Jiji la Roma.

No comments: