-Wenyeviti 19 CCM, wanataaluma wapangwa
-Lowassa aomba na kukutana na Kikwete Pasaka
-Kardinali Pengo naye anena
HATUA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka kujitenga na viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kwa ufisadi imeendelea kuibua mambo, wahusika wakiendeleza mikakati ya kujinusuru inayohusisha kumtisha Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete, Raia Mwema limeelezwa.
Duru za kiusalama zinaeleza kwamba pamoja na kuwa kuna dalili za wazi za kutapatapa kwa watuhumiwa na wafuasi wao, vyombo vya usalama vimekuwa vikiweka mkakati wa kufuatilia taarifa hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nchi inakua salama.
Uamuzi wa chama tawala kujitenga na watuhumiwa wa ufisadi ukibeba msemo mpya wa ‘kujivua gamba’ wa wiki mbili zilizopita, uliwagusa wanasiasa wazito ndani ya CCM, waziri mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambao wametakiwa kujiuzulu nafasi zao za uongozi.
Kuna habari kwamba wanasiasa hao wameanza kuunda mtandao mpya wa kuwaokoa ukihusisha watu kutoka taaluma mbalimbali na mkakati wa kwanza inasemekana ni kumtisha Rais Kikwete na watu walio karibu naye.
Taarifa zinadai kuwa katika mpango huo kundi moja la wanahabari lilikutana katika hoteli moja kubwa eneo la Ubungo, Dar es Salaam, Aprili 18, mwaka huu, chini ya uratibu wa mmoja wa watendaji waandamizi wa mmoja wa watuhumiwa hao, katika kikao kilichofanyika hadi usiku wa maneno na washiriki kupozwa na kitita cha fedha. Majina ya washiriki tunayahifadhi kwa sababu za kitaaluma, mmoja akiwa amepeleka benki mbili tofauti sehemu ya fedha hizo siku iliyofuata, Aprili 19, 2011.
Wakati hayo yakiendelea, kuna taarifa ya kuwa Lowassa ambaye alikuwa Zanzibar kwa mapumziko ya Pasaka na kukutana na marafiki zake wa siasa, aliomba na kufanikiwa kuonana na Rais katika mazungumzo ambayo Raia Mwema imeshindwa kuthibitisha yalihusu mada gani.
“Kilichozungumzwa ni siri na sidhani kama kitasemwa ila kitajulikana kwa vitendo. Hapa kuna maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na kuna Mwenyekiti kama yeye binafsi, sasa sidhani kama mazungumzo yao yatabadili maamuzi ya vikao, sana sana yatalenga kuweka msisitizo kwa kilichotokea,” kinaeleza chanzo cha habari hizo.
Imeelezwa kikao cha Kikwete na Lowassa kilifanyika juzi Jumatatu siku moja baada ya kusambazwa kwa taarifa za vitisho dhidi ya Rais Kikwete katika mtandao wa intanenti wa JamiiForums huku watu walio karibu na wanasiasa hao wakieleza kwamba maamuzi ya NEC yalizingatiwa huku Lowassa akilalamikia kauli za kuendelea kumsema hadharani.
Imeelezwa kwamba kabla ya kikao hicho kati ya Kikwete na Lowassa, watuhumiwa wengine walielezewa kutofurahia kikao hicho kufanyika kati ya watu wawili tu wakati walioathirika zaidi ni watatu, wakihofia kuhujumiwa na mwenzao.
Tayari Rais Kikwete amekwishapata taarifa za hujuma dhidi yake na hiyo inadhihirishwa na kauli yake kuunga mkono matamko ya yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Nape amenukuliwa mara kadhaa akisema kwamba watuhumiwa wamekuwa wakitumia vyombo vya habari, wanasiasa wa upinzani na viongozi wa dini kujisafisha na kumchafua Rais.
Wafuatiliaji wa harakati ndani ya CCM wameuona uungaji mkono huo wa Kikwete kwa kauli za Nape kuwa ni uthibitisho kwamba Nape hajisemei hovyo bali ametumwa na mwenyekiti wake kusema anayoyasema.
Pamoja na Rais Kikwete kuunga mkono matamko hayo ya Nape, kumekuwapo taarifa za kutatanisha kutoka kwa baadhi ya wasaidizi wake wa karibu ambao wamenukuliwa wakiwapigia watu mbalimbali simu wakibeza kauli za Nape wakisema “ni kauli zake, si za NEC”, hali ambayo inazidi kuashiria kuwa hali ndani ya CCM na serikali yake si shwari.
Sehemu ya taarifa ambayo iliingizwa kwenye mtandao wa Jamii Forums ilisema:
“Baada ya JK kupewa taarifa juzi usiku ya ni nini Rostam na Lowassa wanatarajia kukifanya baada ya Sikukuu ya Pasaka, mpango huo umemkasirisha sana JK na tayari baadhi ya vijana ndani ya idara wametumwa kuuzima mpango huo kwa njia na gharama yeyote ile.”
Taarifa hiyo iliyoashiria kumtisha Kikwete na wasaidizi wake dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, ilidai kwamba mwanasiasa mmoja mstaafu amejaribu kutoa ushauri kuwa Kikwete kutoa fursa ya usuluhisho na akina Lowassa ili kuzima kile kinachoelezwa kuwa ni mpango wa kumshughulikia yeye (Kikwete).
Mtoa taarifa huyo alionyesha kwamba kundi la kina Lowassa limejipanga “kumshughulikia” Kikwete kwa njia mbili kuu, wakianzia na ile ya kutumia viongozi wa CCM na tayari walikwisha kufanya mazungumzo na wenyeviti 19 wa mikoa ambao ‘wamewezeshwa’ tayari kwa kazi hiyo.
Mpango namba mbili umeelezwa ni kumtumia Lowassa mwenyewe ambaye atamhusisha Kikwete na kashfa mbalimbali kabla ya kushirikisha vyama vya upinzani katika kumuandama (Kikwete) kwa njia ya maandamano na matamko mazito.
Wito mbadala wa kujivua gamba
Katika hatua nyingine, Kanisa Katoliki kupitia kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, limeweka bayana kutowatenga watuhumiwa wa ufisadi na kwamba litawapa nafasi ya kuungama.
Hata hivyo, tamko hilo la Kardinali Pengo limekuja katika wakati ambao kumeibuka madai ya kutaka watuhumiwa hao si tu warejeshe chochote walichopata kwa njia za kifisadi, lakini wapandishwe kizimbani.
Chimbuko la maoni hayo ni uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kuwapa miezi mitatu watuhumiwa watatu wa ufisadi, Rostam Aziz, Andrew Chenge na Edward Lowassa, kujiuzulu ujumbe wa NEC, ikiwa ni sehemu ya kusafisha chama hicho dhidi ya tuhuma za ufisadi.
Akiongoza misa kwa wanakwaya wa Shirikisho Kwaya Katoliki (SHIKWAKA), Tabata, Dar es Salaam, Aprili 25, mwaka huu Jumatatu ya Pasaka, Kardinali Pengo alisema kanisa hilo litatoa nafasi kwa watuhumiwa hao kuungama badala ya kuwafukuza.
“Watu wakifarakana kisiasa, mimi kama Askofu au padre siwezi kusema wewe uliyefukuzwa au kutuhumiwa usinisogelee. Siwezi kumwambia mtu kwa sababu CCM imekukataa usije kwangu. Nikifanya hivyo nitakuwa nimeweka imani ya CCM katika ukatoliki.
“Muumini mwenye ugomvi na chama chake hapotezi haki yake ya kuungama kwangu au kupata mwongozo. Lakini akija kwangu kujadili kuhusu kupata silaha ni makosa lakini kupata ujumbe wa matumaini wa Mungu ni sawa,” alisema Kardinali Pengo na kusisitiza;
“Siwezi kusema wasije kwangu kuhitaji msaada. Kumekuwa na uzushi mwingi umetokea...mara maaskofu wanachochea upinzani, mara mafisadi wanachota nguvu za maaskofu ili kujiimarisha. Ujumbe wetu ni kwamba Bwana anahitajika na wote. Hatuwezi kumtupa mtu eti kwa sababu chama chake hakimpendi, tukifanya hivyo tutakuwa tumetupa ujumbe wake Bwana,”
“Bila kujali upepo unakwenda kulia au kushoto, tutabaki bila upande. Huu ni ujumbe muhimu kama hatutaki Tanzania yetu isambaratishwe katika misingi ya imani za kidini,” alisema Pengo.
Lakini wakati Pengo akitoa msimamo huo wa Kanisa Katoliki, baadhi ya viongozi wa kisiasa wametoa wito kwa watuhumiwa hao na wengine kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba naye anaungana na viongozi wenzake, akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutaka viongozi hao wafikishwe mahakamani.
Akizungumza katika mapumziko ya Pasaka, Profesa Ibrahimu Lipumba, alitaka watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Kati ya kashfa ambazo alizungumzia Profesa Lipumba ni ufisadi katika ununuzi wa rada ya kijeshi, akisema wahusika wafikishwe mahakamani kwa kutumia ushahidi wa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Ufisadi (SFO), ya Uingereza.
Mapema mara baada ya CCM kutangaza dhana ya kujivua gamba, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, alitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani na harakati hizo zisiachiwe kuishia kwenye uamuzi wa kisiasa pekee.
No comments:
Post a Comment