WAKATI Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na wenzake saba wakipata dhamana na kutoka rumande jana wilayani Tarime mkoani Mara, polisi ameuawa wakati akifuatilia wavamizi wa hifadhi ya taifa, wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Lissu na wenzake saba juzi walilala rumande baada ya kukosa dhamana katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, wakikabiliwa na mashitaka ya uchochezi na uvunjifu wa amani wilayani humo.
Pia Mbunge huyo na wenzake hao wanadaiwa kuchochea ndugu za watu wanne katika kesi ya uchochezi inayowakabili Tarime,waliouawa na polisi wakati wakivamia mgodi wa dhahabu wa North Mara Barrick Mei 16, wasusie miili ya marehemu.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Yusto Ruboroga, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Hussein Kiria, alidai juzi kuwa kwa nyakati tofauti, Mei 23, washitakiwa walishawishi ndugu za marehemu kutochukua miili katika mochari ya hospitali ya wilaya kwa ajili ya mazishi.
Marehemu hao ni Chacha Ngoka wa Kewanja, Nyamongo, Emmanuel Magige wa Nyakunguru, Mwikwabe Marwa na Chawali Bhoke wote wa Mugumu Serengeti.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo iliyofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 24, Mwita Waitara (36), Mwita Maswi (48), Abdalah Suleman ‘Sauti’ (31), Stanslaus Nyembea (33) na Underson Chacha (35) ambao ni wakazi wa Tarime. Wengine ni Andrew Andalunyandu (63) na Irahim Juma (27) ambao ni wakazi wa Singida.
Washitakiwa hao jana walikamilisha masharti ya dhamana yakiwamo ya kuwa na wadhamini wanaofahamika, wenye mali isiyohamishika na barua za watendaji wa kata zenye picha za wadhamini. Kesi hiyo itatajwa Juni 27 mwaka huu.
Mbunge Viti Maalumu, Esther Matiko (Chadema) hakufikishwa mahakamani kama ilivyoripotiwa jana, badala yake alishikiliwa na kuhojiwa na polisi kwa muda kabla ya kujidhamini na kuruhusiwa.
Wengine walioshikiliwa na kuhojiwa Polisi ni waandishi wa habari wanne ambao ni Anthony Mayunga (Mwananchi), Mabere Makubi (Channel ten TV), Berdina Nyakeke (The Citizen) na Anna Mroso (Nipashe).
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Constantine Massawe alisema jana kwamba maiti wote wanne walichukuliwa na ndugu zao mochari na kuzikwa bila ya mikusanyiko ya aina yoyote baada ya kupigwa marufuku.
Alisema tangu juzi na jana, hali mjini Tarime ilikuwa shwari na hakuna fujo za aina yoyote zilizoripotiwa, na watu wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Akizungumzia madai ya Polisi kupora maiti kutoka kwa ndugu na kisha kumtelekeza porini, Massawe alisema picha iliyoonekana kwenye baadhi ya vyombo vya habari jana ni ya familia iliyochukua mwili wa ndugu yao na kuupeleka porini.
Alisema ndugu hao walikuwa wakishawishiwa na baadhi ya watu kususia kumzika maiti huyo, huku wakiwa na waandishi wa habari ambao wote walikamatwa kwa madai ya uchochezi.
Katika tukio la Sumbawanga, polisi walilazimika kufyatua risasi dhidi ya wananchi jamii ya wafugaji, waliovamia Kijiji cha Mfinga wilayani humo na kumwua polisi kwa kumchoma mkuki kichwani.
Licha ya kuuawa kwa askari huyo kuna taarifa kwamba raia ambao idadi yao haijajulikana, walijeruhiwa vibaya wengine wakihofiwa kufa kutokana na polisi kuwapiga risasi baada ya kuona mwenzao ameuawa.
Habari za uhakika zilizotufikia na kuthibitishwa na Polisi Mkoa wa Rukwa, zilisema mapigano hayo yalitokea jana, kwenye kitongoji cha Katekela na polisi aliyeuawa ni Sajini Elikana mwenye namba D 2148 na alipoteza maisha wakati akikimbizwa katika hospitali ya wilaya mjini humo.
Mauaji ya polisi huyo yalitokea muda mfupi baada ya kikao cha usuluhushi baina ya wananchi wa kitongoji hicho na wafugaji wanaodaiwa kuvamia baadhi ya maeneo hayo, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Katavi wakitokea wilaya za Nkasi na Mpanda.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema mauaji yalitokea baada msako ulioendeshwa na askari wanne wakifuatana na baadhi ya maofisa wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga ambao walipata taarifa ya uvamizi huo wa wafugaji katika kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, baada ya askari huyo kuchomwa mkuki na kuanguka chini, katika hali ya kujihami, polisi wengine walifyatua risasi wakielekeza kwenye kundi lililorusha mkuki huo na baadhi ya wananchi walijeruhiwa lakini akaeleza kuwa hakuna taarifa za kuuawa kwa mwananchi yeyote.
“Zipo taarifa kuwa baadhi ya wafugaji walipigwa risasi na kujeruhiwa na askari wetu katika harakati za kujihami … mwenzetu askari mpelelezi wa wilaya Mrakibu Kajala kwa hiyo wapo waliokamatwa, lakini idadi yao bado haijafahamika,” alisema.
Aidha Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Isuto Mantage na Ofisa Upelelezi wa Mkoa, Peter Ngusa, wakiwa na askari zaidi ya 20 walikwenda eneo la tukio umbali wa kilometa zaidi 100 kuendesha msako maalumu ili kuwatia nguvuni watuhumiwa wa mauaji hayo.
Hata hivyo, wengi wao wanadaiwa kukimbia maeneo hayo na kutelekeza mifugo, wake na watoto wao na kujificha kusikojulikana, huku wengine wakibaki eneo la tukio na silaha za jadi tayari kwa kukabiliana na lolote litakalowakabili.
No comments:
Post a Comment