CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeamua kusimamia na kuratibu mazishi ya watu waliouawa na polisi wakidaiwa kuvamia mgodi wa dhahabu wa North Mara hivi karibuni.
Hatua hiyo inatokana na kile chama hicho kupitia kwa Mbunge wake wa Arusha Mjini, Godbless Lema inachokiita kulinda haki ya ndugu wa marehemu hao.
Lema, alilieleza gazeti hili jana, kuwa yupo Tarime kusimamia na kuhakikisha haki inatendeka, baada ya vifo vya watu watano waliouawa kwa madai ya kuvamia mgodi huo.
Pia Mbunge huyo alisema, chama chake kinaunga mkono mgomo wa familia za watu hao watano wa kutochukua maiti kwa ajili ya maziko, hadi uchunguzi wa kitaalamu utakapofanyika kubaini sababu za vifo vya watu hao.
Akizungumza kwa njia ya simu Lema alisema, tayari wanasheria wa chama hicho; Mshauri wa Mambo ya Sheria, Mabere Marando na Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, walikuwa njiani kwenda Tarime kutoa msaada wa kisheria kwa familia hizo.
“Najua watu watasema kuwa hii ni siasa, naweka wazi kuwa mimi Lema niko hapa kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi kama alivyo Kagasheki (Hamis -Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), tunachotaka hapa ni kuhakikisha haki inatendeka kwa watu hawa,” alisema Lema.
Alidai akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, alishuhudia polisi akiwamo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Constantine Massawe na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, wakizipa fedha familia za marehemu kwa ajili ya majeneza, chakula na usafiri wa maziko.
“Sasa mimi nashangaa hawa wameuawa na polisi kwa madai kuwa ni majambazi, tangu lini polisi wakahusika na mazishi ya majambazi? Familia zimekataa fedha hizo na sisi tunaunga mkono na tunasisitiza hatoki maiti wala kuzikwa hadi wachunguzwe,” alisema.
Alisema, msimamo uliopo sasa ni mgomo wa mazishi ya watu hao kutoka kwa familia zao, hadi watakapofika madaktari wa kuchunguza miili hiyo, ambayo kwa mujibu wa Lema inaaminika kuwa watu hao waliuawa.
“Hapo ndipo sasa Chadema itatoa msaada wa kisheria kwa wanafamilia hao kupitia kwa Lissu na Marando, watakapojua ni hatua zipi za kisheria za kuchukua kwa kuwa miili hiyo inaonekana kupigwa risasi kichwani na kifuani na hizo ni dalili za mauaji,” alidai.
Hata hivyo, Kamanda Massawe, alikanusha kutoa fedha kwa familia hizo zilizofiwa na ndugu zao.
“Kilichofanyika ni kuhoji wafiwa kwa yeyote anayehitaji msaada wa ama chakula, usafiri na fedha, kwa ajili ya mazishi na tunachojua sisi hawajakataa ila hakuna familia iliyojitokeza.”
Kagasheki juzi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akijibu hoja ya Polisi kusaidia mazishi kwa watu hao wanaodaiwa kuuawa wakati wakijaribu kuvamia mgodi huo wa North Mara kuwa, msaada huo unatokana na ukweli kuwa waliokufa ni Watanzania na binadamu kama walivyo binadamu wengine.
Watu zaidi ya 800 wenye silaha walivamia mgodi huo hivi karibuni wakiwa na silaha mbalimbali kwa malengo ya kupora mawe yenye dhahabu na kukabiliana na polisi ambao walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya wakashindwa na kisha kutumia risasi za moto na kuua watano.
Juzi Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, akifuatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Sagara, walishambuliwa kwa mawe na wananchi wa Nyamongo, wakati viongozi hao wakienda kuwafariji kutokana na msiba huo.
No comments:
Post a Comment