MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete amesema, Watanzania wasimhukumu kwa kumuona akiendesha magari ya bei ghali na wazipuuze kauli zinazotolewa na wanasiasa wawili wa upinzani kuwa yeye ni bilionea.
Amekanusha tuhuma dhidi yake kuwa ni bilionea na kutoa siku saba kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, kuthibitisha tuhuma hizo.
Ridhiwani amewataka viongozi hao wakanushe tuhuma walizomtupia au kuthibitisha kwa vielelezo, vinginevyo atawaburuza mahakamani kwa kumchafua yeye na familia yake.
Ridhiwani aliwataka Watanzania wasimhukumu kwa kumuona mitaani akiendesha magari ya bei ghali kama vile Benz na kuelezea kuwa, hiyo inatokana na namna alivyolelewa na wazazi wake kuhusu namna ya kuishi na watu.
“Hapa mjini jamani tunaishi kimjini si kila kitu unachomuona nacho mtu ni cha kwake,” alieleza Ridhiwani katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumatatu Dar es Salaam.
Amesema, Dk. Slaa na Mtikila wamekuwa wakimzushia kuwa yeye ni bilionea na kwamba anamiliki kampuni ya malori 150 na ya ujenzi pamoja na ghorofa za kupangisha, jambo ambalo si kweli.
Aliita habari za viongozi hao kuwa ni za uongo na uzushi na zimelenga kumchafua yeye na mzazi wake na kupandikiza chuki dhidi ya familia yake na jamii.
“Nachukua nafasi hii kuwaeleza umma kuwa mimi nawaheshimu sana hawa wazee na ingekuwa busara kwa umri wao na mamlaka waliyonayo ndani ya jamii na vyama vyao vya siasa wajitokeze na kutoa ushahidi juu ya wanayosema dhidi yangu katika vyombo vya habari ili hatua zichukuliwe,” alisema Ridhiwani.
Alisema, akiwa kijana aliyemaliza shule hivi karibuni, haiwezekani kumiliki mali zote zilizotajwa na kama kweli anamiliki, itakuwa rahisi kuthibitisha kwa kuwa ukiwa na kampuni lazima kuwe na jina la mmiliki na akaunti ambako fedha za kampuni hiyo zinakwenda.
“Huwezi kuandika akaunti ya mtu hivi hivi ukadai kuwa una kampuni akikuibia?,” Alihoji.
Alisema, yeye si bilionea kama wanavyodai wanasiasa hao, na kutaja mali zake kuwa ni shamba lililopo Bagamoyo la ekari moja na nusu, gari aina ya Toyota Cami na akaunti mbili katika benki za Stanbic na NBC.
Aliwataka viongozi hao kama itathibitika kuwa habari walizomtuhumu ni uongo, wautangazie umma na kuliweka hilo bayana kwa sababu hiyo siyo mara yao ya kwanza kuongopa na kutoa taarifa zisizo za kweli.
Alitolea mfano habari aliyowahi kuitoa Dk. Slaa kipindi cha uchaguzi mwaka jana kuwa watu wasiopungua 50 walikutana jijini Mwanza katika Hoteli ya La Cairo pamoja na Rais Jakaya Kikwete wakati huo mgombea urais, jambo ambalo kwa mujibu wa Ridhiwani halikuwa la kweli kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa Nachingwea na Rais Kikwete Kibaha.
Alisema, pia Dk. Slaa aliwahi kudai kuwa na uthibitisho wa kontena la kura kukamatwa Tunduma mkoani Mbeya, jambo ambalo halikuthibitishwa. Kwa upande wa Mtikila, alisema amewahi kukiri kuongopewa.
Aliwataka viongozi hao wawili kuacha kuwa makanjanja wa kutengeneza habari katika njia ya kutafuta sifa za kisiasa na badala yake watoe ushahidi juu ya wanayoyasema, vinginevyo baada ya siku saba atawaburuza mahakamani.
“Kwa umri wao na nafasi walizonazo ni fikra zangu kuwa wataacha kuwa wasema hovyo na kuendeleza utamaduni unaonekana kukua kwa watu kuanza kutumia vyombo vya habari bila kuwa na ushahidi wa kutosha wala kuheshimu haki za watu,” alisema.
Akijibu swali juu ya viongozi hao kuwa huenda wanatumiwa na mafisadi wanaompiga vita Rais Kikwete, Ridhiwani alisema:
“Kuhusu suala hili kuhusishwa na ufisadi siwezi kulizungumzia, ila kama wananishambulia kwa sababu mzee anapiga vita ya ufisadi, jambo hili si la Ridhiwani au baba, bali ni la Watanzania,”
Aliongeza “haitopendeza hata kidogo na wala sitaki kuamini kuwa viongozi hao wawili wanatumiwa.”
Hivi karibuni, Dk. Slaa akiwa katika moja ya mikutano ya hadhara mkoani Tabora, alisema Ridhiwani amemaliza shule miaka michache iliyopita, lakini hivi sasa ni bilionea na kwamba ameupata utajiri huo katika mazingira ya kutatanisha.
Wakati Mtikila kwa upande wake akizungumza na waandishi wa habari alidai Ridhiwani amegeuka bilionea kwa muda mfupi “kwa mgongo wa baba yake.”
Alienda mbali na kudai kijana huyo ambaye Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), aliingiza magari makubwa ya mizigo zaidi ya 100 na yanafanya kazi ya kusomba mizigo DRC na mengine ameyauza.
Aidha, alidai pia kuwa mtoto huyo wa rais anamiliki kampuni ya ujenzi wa barabara na maeneo mengi ya ardhi kwa lengo la kujenga ghorofa za kupangisha.
No comments:
Post a Comment