OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini imevionya vyama hivyo kuacha kupenyeza siasa kwenye taasisi za umma zikiwamo shule, vyuo na sehemu za kazi kwa kuwa ni kosa kisheria.
Aidha, imeiandikia barua Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuifahamisha kuhusu tatizo hilo na kuiomba ichukue hatua za dhati kwa kuwakumbusha wakuu wa vyuo na wahadhiri nchini, juu ya sheria inayozuia siasa kuendeshwa vyuoni na shuleni, ili waitekeleze pia.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Ibrahim Mkwawa, alisema, hatua hiyo ilitokana na kuzuka kwa tabia ya baadhi ya vyama vya siasa kuendesha siasa katika taasisi hizo na hivyo kukiuka sheria ya vyama vya siasa inayokataza jambo hilo katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili huyo aliyekuwa akijibu swali kuhusu kujipenyeza kwa vyama vya siasa katika taasisi za umma hasa shuleni na vyuo vya elimu ya juu na hatua zilizochukuliwa na ofisi yake kulizuia, alisema waliamua kuviandikia barua ya onyo vyama 18 vyenye usajili wa kudumu.
Kwa maelezo yake, barua hiyo ya Aprili 16 iliyojibiwa na baadhi ya vyama, licha ya kutotakiwa kufanya hivyo kwa kuwa ilikuwa ni onyo na taarifa ya kuwakumbusha wajibu wao, ililenga pia kuvikumbusha vyama vingine juu ya umuhimu wa kutoendesha siasa katika taasisi hizo ili visiige mambo hayo baadaye.
“Siasa vyuoni ni tatizo kubwa tuliloliona na kujiridhisha, kuwa linasababishwa na vyama vyetu vya siasa vinavyokiuka sheria na hivyo kupandikiza nyanja hiyo katika taasisi hizo za umma kwa kutumia vijana shuleni, mahali pa kazi na katika taasisi za elimu ya juu.
“Vyama vilipaswa kusubiri vijana hao mitaani na mahali pengine nje ya vyuo au shuleni na kuwaimbisha kuhusu siasa. Kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa kwenye taasisi hizo na kampeni za uchaguzi katika majengo ya vyuo pia, ni kinyume cha sheria ya vyama vya siasa,” alisema.
Mkwawa alifafanua kuwa kitendo cha kupandikiza siasa za vyama katika vyuo ambavyo hata hivyo sheria ya vyuo inakataza, ni kusababisha machafuko ya amani na kuchanganya wanafunzi, kwa kuwa wengi hubadilika na kuegemea kwenye itikadi za vyama badala ya elimu waliyoifuata kwenye taasisi hizo.
“Sheria inaeleza wazi, kuwa ni kosa na ndiyo maana tumeviandikia vyama vyote kuvionya na kuvikumbusha ili matatizo hayo yakijirudia visiseme kuwa havikujua. Adhabu kwa mujibu wa sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 ni Sh. milioni moja au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote mbili kwa pamoja, kwa mtu au chama kitakachoendesha siasa mahali pasiporuhusiwa, ikiwa ni pamona na vyuoni na kwenye nyumba za ibada,” Mkwawa alisema.
Alitaja sheria hiyo kuwa ni kifungu cha 12 (2) cha sheria ya vyama vya siasa iliyoongezwa uzito mwaka 2009 kwa kifungu A kinachovitamka vyama vya siasa pia badala ya mtu mmoja mmoja kama kifungu cha 2 kinavyoeleza.
Kwa pamoja, vifungu hivyo vinakataza shughuli za siasa kufanywa na mtu au vyama katika taasisi za serikali, shule, vyuo na ofisi za umma.
Kipindi cha nyuma, Profesa Idrissa Kikula wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) naye aliwaonya wanafunzi wa chuo hicho kuacha kuingiza siasa katika chuo hicho, kwa kuwa ni kosa na hivyo kuwataka washiriki wakiwa mitaani au mahali pengine nje ya chuo.
No comments:
Post a Comment