JAJI Mkuu mstaafu, Augustine Ramadhani , amelitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na
wadau wote wa habari nchini kukusanya nguvu zao na wanasheria kuhakikisha Katiba mpya inatambua uhuru wa vyombo vya habari.
Amesema, Katiba ya sasa haitambui uhuru wa vyombo vya habaribadala yake inatambua uhuru wahabari wa mtu mmoja mmoja.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Dar es Salaam jana, Jaji Ramadhani alisema, kwa sasa mchakato wa kuunda Katiba mpya unaendelea hivyo ni vyema wadau hao kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unakuwemo.
“Ingawa leo wanahabari wote wanasherehekea siku hii na miaka 20 ya Maazimio ya Windhoek, suala la uhuru wa vyombo vya habari halimo katika Katiba, nawashauri hii iwe
ajenda yenu kubwa katika mjadala wa Katiba mpya,” alisema Jaji Ramadhani.
Alitolea mfano uhuru wa Mahakama kuwa hata nao haukuwemo kwenye Katiba lakini sasa ni miaka 10 tu imepita tangu uhuru huo uingizwe kwenye Katiba, “nasisitiza kuwa bado hamjachelewa anzeni mchakato wenu sasa”.
Alisema inasikitisha Serikali kuhusishwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari au uhuru wa kitu chochote jambo ambalo pamoja na kuwa lina ukweli, lakini sababu kubwa ya ukosefu wa uhuru huo ni wanataaluma wenyewe wakiwemo wanasheria na wanahabari.
“Naomba tukubaliane hapa hakuna Serikali yoyote duniani inayotoa maelezo ya kila kitu chake, lazima kuwapo kufichaficha lakini jambo lililowazi ni kwamba wanahabari uhuru wao wanatakiwa uwe dhidi ya waajiri wao, dhidi ya wale wanaowaandika, dhidi ya umma na
nafsi zao wenyewe,” alisema.
Alisema mwanataaluma yeyote lazima awe na nafsi inayomlinda katika kufuata maadili na kwa waandishi wa habari aliwataka kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo moja kwa
moja huwanyima uhuru kuandika dhidi ya aliyewapa rushwa.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari vya Kusini mwa Afrika upande wa Tanzania (MISA-TAN), Bujaga Kadago, aliiomba Serikali kupitia maudhui ya Azimio
la Windhoek ili kuweka mazingira mazuri ya kazi ya uandishi wa habari.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawezesha waandishi wa habari kufanya kazi yao bila uoga kwani kuwapo kwa mazingira magumu kwao kunajenga hali ya uoga, kutojiamini na hatimaye wananchi hupatiwa habari zisizokamilika na kunyimwa haki yao ya msingi kikatiba.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Reginald Mengi, aliwataka waandishi wa habari kufuata maadili ya kazi yao na kuandika habari zinazohamasisha maendeleo na demokrasia na kuacha kushabikia habari za wanasiasa zinazoweza kuleta uchochezi katika jamii.
No comments:
Post a Comment